Tuesday, January 22, 2013

Mnyika: Spika aelezee ufisadi Urafiki


MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutoa kauli kwa umma kuhusu hatua alizochukua kuhusu ufisadi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki ambao mpaka sasa hajatoa idhini ya kushughulikiwa.
Mnyika alieleza kuwa majibu ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, kuwa anafuatilia suala hilo wizarani hayajitoshelezi, kwani zaidi ya nusu mwaka umepita toka atoe ahadi ya kufuatilia.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema waziri ameshuhudia matumizi mabaya ya mali za kiwanda hicho alipotembelea Mei 28, mwaka jana.
“Nilimpa wito wa kutembelea kiwanda hicho baada ya kuteuliwa kwake, ili ashughulikie udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa ubinafsishaji,” ilieleza taarifa hiyo.
Mnyika pia aliitaka serikali iweke hadharani ripoti ya matumizi ya mkopo wa dola milioni 27 (sh bilioni 40) ambazo zilitumika kununua mitambo chakavu kutokana na mianya ya ufisadi.
“Spika wa Bunge Anne Makinda aeleze sababu za kutoruhusu mpaka sasa kuundwa kwa kamati ndogo ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchunguza na kuchukua hatua kwa kuwa kuchelewa kufanya hivyo ni sawa na kulea ufisadi na kukwamisha wabunge kutimiza wajibu wa Kikatiba wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi,” alieleza Mnyika katika taarifa yake.

No comments:

Post a Comment