Saturday, January 26, 2013

KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 26 NA 27 JANUARI 2013


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


‘KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 26 NA 27 JANUARI 2013”
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) itafanya mkutano maalum wa siku mbili tarehe 26 mpaka 27 Januari 2013 Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo wa Kamati Kuu utajadili  ajenda mbalimbali ikiwemo Taarifa ya Fedha kwa mwaka 2012, Mpango Kazi na Bajeti kwa mwaka 2013, Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa chama na Operesheni ya M4C, Maudhui na Mchakato wa Katiba Mpya, Taarifa ya Katibu wa Wabunge wa CHADEMA, Maandalizi ya ajenda za Baraza Kuu la Chama.
Itakumbukwa kwamba mara ya mwisho, Kamati Kuu ya CHADEMA mkutano wake wa kawaida kwa siku mbili tarehe 15 mpaka 16 Disemba 2012 Jijini Dar es salaam ambao ulifanya maamuzi mbalimbali.
Kamati Kuu iliazimia kwamba Rais akumbushwe mwezi Disemba 2012 kujibu barua kuhusu haja ya kuundwa kwa Tume ya Kimahakama/Kijaji kuchunguza mauaji ya raia kama alivyoahidi na mwendelezo wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) utumike kuishinikiza Serikali iwapo hatua stahiki zitakuwa hazijachukuliwa; kwa kuzingatia kwamba 2013 ni mwaka wa “nguvu ya umma”.
Kamati kuu iliazimia kwamba uongozi wa CHADEMA katika maeneo ambazo chaguzi za marudio za udiwani, mitaa, vijiji na vitongoji zinacheleweshwa kwa makusudi uunganishe umma kufanya shinikizo la kisiasa kwa mamlaka zinazohusika kutangaza nafasi kuwa wazi na vyombo vinavyosimamia chaguzi katika ngazi hizo ili haki za kikatiba na kisheria za wananchi kupata uwakilishi ziweze kupatikana kwa wakati.
Kamati Kuu iliazimia kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA ichukue hatua za kibunge kuhakikisha kwamba daftari la wapiga kura linaboreshwa mwaka 2013 ikizingatiwa kuwa daftari hilo hilo litatumika kwenye kura za maoni za katiba mpya.
Kamati Kuu iliazimia kwamba Kamati Ndogo ya Kamati Kuu ikutane kwa haraka na kufanya tathmini kuhusu mchakato wa katiba mpya na kamati hiyo iwasilishe mapendekezo kwa tume ya mabadiliko ya katiba juu ya maoni ya CHADEMA ya kuzingatiwa katika katiba mpya na mapendekezo kwa Serikali juu ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba awamu ya pili na ya tatu kwa pamoja ili nchi ipate katiba mpya na bora yenye muafaka wa kitaifa.
Kamati Kuu iliazimia kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA itumie njia mbalimbali za kibunge kupitia hoja binafsi au miswada binafsi kuwasilisha bungeni mapendekezo ya marekebisho ya katiba mpito kuhakikisha tume huru ya uchaguzi na marekebisho ya sheria zinazosimamia uchaguzi yanafanyika kabla ya katiba mpya kwa kuzingatia kuwa kwa mujibu sheria ya mabadiliko ya katiba kura ya maoni ya katiba mpya itasimamiwa na tume ya sasa kwa mfumo wa kikatiba na kisheria usio huru.
Imetolewa tarehe 25 Januari 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

1 comment: