CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kinatarajia ushindi mnono katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho, katika Jimbo la Muleba Kaskazini.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Muleba, Katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) wa jimbo hilo, Robert Rwegasira, alisema wanatarajia ushindi kwani wananchi wameshagundua umuhimu wa kuchagua wawakilishi makini ili kusimamia rasilimali za nchi na kuboresha huduma za jamii.
Alisema uchaguzi huo mdogo unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuhama vyama, vifo na wengine kujiuzulu.
Rwegasira alisema vijiji vitakavyokuwa katika uchaguzi kesho ni Katoke, Kahumulo, Rwazi, Rwanganilo na Malele.
Vitongoji vinavyofanya uchaguzi ni Bukomo, Rwanganilo, Bugasha, Kitubi, Mushenyi, Mbango, Malele, Katoke, Rwazi, Kamachumu, Kahumulo, Ilundu, Kamushenya na Kalele.
Rwegasira aliwataka wananchi wa maeneo husika yenye uchaguzi kujitokeza kwa wingi.
No comments:
Post a Comment