Saturday, January 19, 2013

Jaji Lubuva: wajumbe tume ya uchaguzi wachaguliwe na wadau


MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametoa maoni mbele ya Tume ya Katiba akipendekeza kuwa Katiba Mpya iunde Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba itambulike kwa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Jaji Lubuva aliyekuwa akitoa maoni hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisema kuwa tume huru ni inayokubalika na wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa jumla, ambayo katika utekelezaji wa majukumu yake, itafanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Uhuru wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume yenyewe…; Kubadilishwa kwa jina na kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau juu ya Tume ya Uchaguzi,”alisema Lubuva.
Lubuva alifafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inapaswa kuanzishwa chini ya sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizo na tume huru za uchaguzi kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Ghana, Zimbabwe na Botswana.
Alipendekeza pia uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ufanywe na wadau mbalimbali na kuteuliwa na rais kabla ya kuthibitishwa na Bunge. “Na kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa wajumbe wa tume hiyo na viongzi wengine tumependekeza pia Katiba Mpya itamke kwamba wadau mbalimbali watashiriki kupendekeza majina, ambayo mwisho wake Rais atashiriki kuteua majina, lakini siyo rais ateue moja kwa moja,” alisema Jaji Lubuva.
Mbali na hayo, Jaji Lubuva pia alipendekeza Katiba Mpya itambue Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini akataka isiunganishwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika utendaji wake wa kazi.
“Pia tunapendekeza Katiba iipe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kugawa kata katika maeneo ya uchaguzi wa madiwani,” alisema.
Alisema kuwa mamlaka hiyo hivi sasa iko chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), jambo alilosema lina athari kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa huathiri uchaguzi wa madiwani, ambao hufanywa na Tume.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Akizungumzia utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na NEC, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema: “Tumependekeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itambulike kikatiba. Tumetaka pia kazi za ofisi hiyo zifanyike kwa kujitegemea na zisichanganywe na NEC.”
Tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992, NEC imekuwa ikilaumiwa kuwa siyo huru na kwamba inaegemea chama tawala.
Madai hayo yamekuwa yakitolewa na vyama vya upinzani, wanaharakati na baadhi ya asasi za kiraia, ambao kwa pamoja walikuwa wakidai kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayotoka katika mfumo tofauti na ulivyo sasa ambapo inateuliwa na rais.
Katika hatua nyingine, Jaji Lubava alisema wamependekeza pia mbunge akihama chama cha siasa, asipoteze haki yake ya kuwa mbunge kwa sababu yeye amechaguliwa na wananchi.
Jaji Lubava alisema kwamba NEC pia imependekeza Katiba Mpya iunde mahakama itakayokuwa ikipokea malalamiko kutoka katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo itafanya kazi ya kupokea malalamiko hayo kabla ya uchaguzi kufanyika.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nayo imetoa maoni yake mbele ya Tume ya Katiba inayokusanya maoni kutoka kwa taasisi mbalimbali.
Akizungumza baada ya kuwasilisha maoni yao jana, Kamishna Mkuu TRA, Harry Kitillya alisema kuwa wamependekeza kuwa misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kwa kampuni na taasisi mbalimbali nchini itambulike kikatiba, ili iwe wazi kwa wananchi.
Kitillya alisema kuwa hata taarifa za mawaziri zinazopelekwa bungeni, zinapaswa kuonyesha matumizi ya wizara husika zikiambatanishwa na taarifa za misamaha hiyo ya kodi.
‘’Hali hiyo itaongeza ufanisi katika suala la ukusanyaji wa mapato kwa kuwa taarifa hizo za mawaziri zilizoambatanishwa na misamaha ya kodi, zitaweza kukaguliwa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serilkali (CAG),’’alisema Kitillya.
Aliongeza kuwa CAG anapaswa kuwa na nguvu kikatiba ya kwenda kukagua taarifa za misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali katika kampuni na taasisi binafsi, hali aliyosema italeta uwazi katika misamaha hiyo kwa wadau mbalimbali.
Kitillya alisema kuwa TRA imependekeza mkwepa kodi, mla rushwa na mtoa rushwa wapewe adhabu ya kifungo pamoja na kutaifishwa kwa mali zao kama mkakati wa kujenga taifa la watu wenye maadili na uaminifu.
Kamishna huyo pia alisema pia kwamba uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uendelee kufanywa na rais, lakini uthibitishwe na Bunge ili kuleta ufanisi zaidi.
‘’Hatusemi kwamba rais apunguziwe madaraka yake, ila tunaona sasa ni busura kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania akishateuliwa na rais, aweze kuthibitishwa bungeni,’’alisema Kitillya.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi katika muungano, TRA imependekeza katika Katiba ijayo kuwepo na chombo kimoja cha ukusanyaji kodi katika Jamhuri ya Muungano, ambapo alisema kuwa kinachotakiwa ni Katiba kuainisha kodi za muungano, ieleze nani atatoza, atazisimamia na mgawanyo wake uwe wazi ili kuondoa malalamiko kwenye suala la mapato.
Wadau mbalimbali wakiwamo wabunge na wachumi wamekuwa wakipinga misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa, ambayo Waziri wa Fedha alipewa mamlaka ya kuitoa aonapo inafaa.
Hatua hiyo imekuwa ikizua mjadala mara kwa mara, huku ikielezwa kuwa inatoa mwanya wa kulihujumu taifa kimapato.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment