Saturday, January 19, 2013

Dk. Kafumu akata rufaa Igunga


ALIYEKUWA Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), ambaye alivuliwa ubunge na Mahamaa Kuu Kanda ya Tabora Agosti mwaka jana, amekata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Mary Shangali, alitaja vipengele sita alivyotumia kutengua matokeo ya ubunge wa Dk. Kafumu.
Alisema vipengele hivyo vilikuwa ni pamoja na matukio yaliyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi huo ambapo ni kutolewa kwa ahadi ya kutojengwa daraja kama hatachaguliwa Kafumu.
Hata hivyo, katika rufaa yake hiyo aliyoiwasilisha mahakamani juzi, Dk. Kafumu alisema anaamini atashinda kutokana na sababu zilizotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu kuwa dhaifu na zisizomhusu yeye.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Dk. Kafumu alisema kuwa atawakilishwa na mawakili watatu ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Dk. Masumbuko Lamwai, Kayaga na Kanyama.
Dk. Kafumu alisema sababu za kutaka rufaa mbali na kwamba ni haki yake Kikatiba lakini pia anaamini kuwa mahakama kuu ilikosea kumhusisha na vurugu zilizosababisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Igunga, Fatuma Kimario, kuvuliwa Hijab na wafuasi wa CHADEMA.
Alisema kitendo cha Magufuli kutoa ahadi ya daraja ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na yeye binafsi hakuhusika kutoa ahadi hiyo.
Katika mahojiano hayo, Dk. Kafumu alilalamika kuwa baadhi ya waandishi wa habari walimlisha maneno kuhusu uamuzi wake huo wa kukata rufaa na hivyo kufafanua upya kile alichokisema baada ya hukumu.
“Nilisema nimetoka mahakamani, bado mapema nawasiliana na chama changu, lakini hata kama nikipoteza ubunge na ukamishna wa madini, mimi bado ni mtaalamu nitafanya kazi nyingine, sikusema sitakata rufaa,” alisisitiza.
Katika kesi hiyo mlalamikaji alikuwa Joseph Kashindye, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CHADEMA.
Katika hukumu yake Jaji Shangali alisema ahadi hiyo ilikiuka mwenendo wa kampeni za uchaguzi.
Aidha Jaji alisema pia kitendo kilichofanywa na upande wa walalamikiwa cha kwenda kutembelea hospitali na kutoa misaada mbalimbali kilikiuka taratibu na hivyo kuathiri zoezi zima la uchaguzi huo.
Kipengele kingine alichokitaja kukiuka taratibu za uchaguzi ni pamoja na kitendo cha ugawaji mahindi ya msaada siku chache kabla ya upigaji kura katika jimbo hilo na hivyo kuwafanya wananchi kupiga kura kutokana na ushawishi wa misaada hiyo.
Pia kupanda katika majukwaa ya kampeni kwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), akiwa amening’iniza silaha kiunoni nako kuliathiri mwenendo mzima wa uchaguzi huo.

Tanzania Daima

1 comment:

  1. unapoteza tu pesa kafumu mlisha kosea cha msingi jitafakari achana na siasa imeonyesha siasa huwezi mpaka ugawe mahindi mh! pole sana

    ReplyDelete