AITUHUMU KUWAPA VYEO MAJANGILI
BAADHI ya maofisa wa taasisi nyeti za serikali ikiwemo Ikulu, wametuhumiwa kula njama kuwaficha watu waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ujangili na wengine kuwapandisha vyeo vikiwemo vya ubalozi.
Tuhuma hizo zimetolewa jana na Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, alipozungumza na waandishi wa habari na kueleza kusudio lake la kupeleka hoja binafsi bungeni ili kuunda tume ya kuchunguza sakata zima la tuhuma za ujangili.
Hata hivyo, mbunge huyo hakuweza kutaja majina ya maofisa wanaotuhumiwa, lakini akafafanua kuwa alipokuwa katika kamati ndogo ya kufuatilia utoroshwaji wa twiga, kuna majina ya watu yalitajwa kwa ajili ya kuchunguzwa na ikibidi wachukuliwe hatua, lakini kilichofanyika ni wahusika kupewa vyeo vya utumishi, ukiwemo ubalozi.
Msigwa alisema tayari Januari 8 mwaka huu katibu wa Bunge amemtaka awasilishe maelezo ya hoja yake kwa Spika kufuatia barua aliyoandika Desemba mwaka jana juu ya dhamira ya kuwasilisha hoja binafsi.
“Nitaomba iundwe kamati teule ya Bunge kufuatilia huu ujangili unaoendelea nchini, kwani tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa robo ya pembe na meno ya faru na ndovu duniani zinatoka Tanzania.
“Idadi ya tembo wanaouawa ni wastani wa 67 kwa siku, na hali hiyo ni hatari kwa rasilimali asili za taifa na pia inahatarisha maliasili na urithi wa nchi,” alisema.
Alisema mtandao wa ujangili nchini ni mkubwa kuliko inavyofikiriwa, na kwamba hata wanaojitoa mhanga kushughulikia hali hiyo maisha yao yanakuwa hatarini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, alikana kuhusika kwa Ikulu, lakini akadai kuwa mtandao wa biashara hiyo ni mkubwa, na kwamba mazingira yaliyopo yanatia shaka kuwa baadhi ya viongozi wanahusika.
“Haiwezekani kontena linapitishwa bandarini Dar es Salaam bila mtu yeyote kujua nini kimebebwa, halafu ufike Indonesia au China ndipo pembe hizo na meno yakamatwe, kuna kuzembea hapo na rushwa ndani yake,” alisema.
Alikiri kudokezwa na Mchungaji Msigwa kuhusu kusudio la kupeleka hoja binafsi na kudai kuwa ni hatua nzuri inayotokana na ukereketwa na uzalendo alionao kwenye rasilimali za taifa.
Hata hivyo, Kagasheki alisema idadi ya tembo inayotajwa kuuawa nchini si ya kweli kwa kuwa juhudi za udhibiti zinazofanywa na wizara yake zimepunguza kasi hiyo hadi kusifiwa na Jumuiya ya Ulaya.
“Hizi pembe za ndovu zinazokamatwa si kwamba tembo wote wameuawa wakati huu, haya ni makusanyo ya muda mrefu huko nyuma. Lakini vile vile watu wanapaswa kuelewa kuwa tembo wengi si kweli kuwa wanauawa Tanzania,” alisema.
Kagasheki alisema kuwa pembe hizo na meno ya tembo yanatoka kwa wingi katika nchi za Malawi na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako wanyama hao wanauawa zaidi, lakini usafirishaji wake unapitia katika bandari ya Tanzania.
Alisema nchi hizo hazina bandari na hivyo hutumia Tanzania hali inayofanya nyara hizo zinapokamatwa nje ya nchi kuonekana kuwa zimetoka hapa, hivyo kuonekana kama kitovu cha biashara hiyo.
Lembeli apigilia msumari
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imepigilia msumari kwa kuanika namna hoteli za kitalii zilivyoongoza kwa hujuma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, alisema wamiliki wa hoteli hizo wamekuwa wakiilipa serikali dola 4 tu, kwa kila mgeni wanayempokea, wakati wao wamekuwa wakitoza dola 350.
Lembeli alisema hujuma hiyo, imetokana na mikataba ya ovyo iliyopo, na hivyo akaagiza serikali kuwasilisha mikataba yote ya hoteli zilizoko ndani ya hifadhi, kuchunguza kwanini zinalipa kiasi kidogo cha fedha ilhali wanakusanya zaidi.
Lembeli alisema kumekuwepo na mzozo na malumbano katika hoteli za Ngorongoro, Seronera na Noro, ambazo kwa mujibu wa mikataba iliyopo pesa inayolipwa dola 4 ya kila mgeni kwa siku ni ndogo.
“Tulipowahoji walisema kuwa mikataba inawafunga. Je, ni kwanini watu hawa wanatengeneza pesa ndani ya hifadhi, lakini hawachangii kile wanachokipata?” alihoji Lembeli.
Alisema kuna mchezo mchafu unafanywa ndiyo maana zilitolewa kwa bei ya kutupwa, kiasi kwamba kama Mwalimu Julius Nyerere angefufuka leo na kushuhudia ufisadi huo angetoa machozi.
Alishangaa kuona kuwa, mtu anayeweka ‘tenti’ ndani ya hifadhi analipa dola 60 kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa) iweje hoteli hizo kubwa zilipe dola nne mpaka sita?
Katika hatua nyingine, Lembeli amemshukia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira kwamba ndiye tatizo kubwa la wananchi kuishi katika maeneo ya malisho ya wanyama.
Lembeli aliyasema hayo jana mbele ya Waziri Kagasheki na Naibu wake Lazaro Nyalandu wakati wa kujadili ripoti ya wabunge wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Alisema Wassira ni tatizo na amemtaka kukaa naye ili wananchi katika jimbo lake waache kuingia katika maeneo ya Ushoroba ambayo ni sehemu sahihi ya malisho ya wanyama katika hifadhi hizo.
No comments:
Post a Comment