MWAKA 1995 Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu irejeshe mfumo wa vyama vingi na Chama cha CHADEMA kilikuwa kimeshiriki uchaguzi huu bila ya kuweka mgombea urais hivyo kulazimika kumuunga mkono mgombea wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Augustino Lyatonga Mrema.
Katika uchaguzi huu wa mwaka 1995 CHADEMA ilipata asilimia sita ya kura zote za wabunge nchini na kupata majimbo matatu ya Kigoma Mjini, Karatu na Rombo. Kilishika nafasi ya tatu katika vyama vya upinzani baada ya Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Mwaka huo CHADEMA iliingia kwenye uchaguzi chini ya viongozi waasisi wa chama mzee Edwin Mtei kama Mwenyekiti, Brown Ngwilulupi kama Makamu Mwenyekiti na Bob Nyanga Makani kama Katibu Mkuu.
Mwaka 2000 Tanzania ilifanya uchaguzi Mkuu wa pili, na CHADEMA kilikuwa kimeshiriki uchaguzi huu kwa mara nyingine bila ya kuweka mgombea urais. CHADEMA ilishirikiana na CUF kuweka mgombea mmoja Prof. Ibrahim Lipumba.
Mwaka huo chama chetu kilipata asilimia tatu ya kura za wabunge na jumla ya wabunge wanne na kushika nafasi ya nne katika vyama vya upinzani baada ya vyama vya CUF, TLP na UDP.
Katika uchaguzi wa mwaka 2000 Mzee Makani alikuwa Mwenyekiti, Dk. Willibrod Slaa Makamu Mwenyekiti na Dk. Amani Kabourou kama Katibu Mkuu. Miongoni mwa wabunge wapya wa CHADEMA waliochaguliwa mwaka 2000 ni pamoja na Freeman Mbowe kutoka Jimbo la Hai.
CHADEMA ilipoteza Jimbo la Rombo, ikaongeza Hai na Moshi Mjini na kulinda Karatu na Kigoma Mjini. Ni vema ieleweke kuwa tangu mfumo wa vyama vingi uanze mikoa ya Kigoma, Arusha na Kilimanjaro imeweka rekodi ya kutoa mbunge angalau mmoja wa chama hiki. Karatu ni wilaya iliyoweka rekodi ya kuchagua CHADEMA mara nne mfululizo tangu mfumo wa vyama vingi uanze.
Mazingira haya ya chama cha tano kwa wingi wa kura katika vyama vyote vya siasa nchini ndiyo mazingira iliyoingia nayo CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka 2005. Mazingira ya kukatisha tamaa, kwani ujanja mjini haukuwa kwa CHADEMA; bali CUF au TLP na zaidi CCM. Mazingira ya kijana ukisema upo CHADEMA vijana wenzako wanakuangalia jicho la mshangao na hata kuchekwa.
Haya ndiyo mazingira ambayo alirithi Freeman Mbowe, kama mwenyekiti wa CHADEMA.
Mbowe alianza harakati zake za kuimarisha CHADEMA kwa kukusanya vijana mbalimbali, wanachama wa CHADEMA na wasio wanachama, kutoka makundi mbalimbali ya jamii kama wanafunzi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari, wanasiasa kutoka vyama vingine na hata vijana wanaharakati katika NGOs nk.
Moja ya msingi wa CHADEMA ni ‘kujenga chama chenye kutoa fursa ambapo kila mtu, bila kujali asili na hali yake, anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake. Kwa mwanasiasa mwingine yeyote nafasi hii ilikuwa ni nafasi nzuri ya kujitengenezea fursa yeye mwenyewe kwa kuhamasisha ufuasi wa watu badala ya ufuasi wa misingi ya chama. Badala yake, Mbowe alitoa fursa kwa kila mwanachama kuchangia katika kuendesha na kuimarisha chama. Na hii ndiyo ilikuwa kauli ya Mbowe kila wakati kwamba ‘chama ni fursa’.. Tuone ni namna gani Mbowe alitumia misingi ya CHADEMA kwa kujenga na kuimarisha chama.
Kazi hii ya kukusanya watu mbalimbali na mikakati ya kuanza kusambaza chama kwa kufanya ziara za wabunge na baadhi ya viongozi wa chama ilianza mwaka 2003 ambapo wanasiasa wengi vijana waliokata tamaa na siasa za vyama vyao walianza kuona matumaini ndani ya CHADEMA.
Mwaka 2004 mwezi Machi, Mbowe akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tatu wa CHADEMA, hivyo kuwa na mamlaka zaidi ya kuleta mabadiliko katika chama. Wanasiasa vijana kama Shaibu Akwilombe, Antony Komu na Msafiri Mtemelwa (aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Vijana wa NCCR-Mageuzi) walijiunga na CHADEMA.
Wanasiasa wanataaluma kama Mwesiga Baregu nao pia walijiunga na CHADEMA kipindi hiki. Kuna kipindi tulikuwa tunajiita ‘Real Madrid’ maana tulikusanya ‘mastaa’ wote kutoka vyama vya upinzani.
Chama, kwa kupitia misingi yake, kiliwapa wanachama hawa nafasi kubwa sana ya kuchangia kwa mawazo katika kuimarisha chama na Mbowe alijitahidi sana kutoa fursa hii kwa kila mwanachama aliye tafuta nafasi ya kuchangia.
Hata Mbunge wa sasa wa Mtera, Livingstone Lusinde, alijiunga na CHADEMA kipindi hiki. Freeman Mbowe aliifanya kazi hii ili kutoa fursa kwa Watanzania wengine kujenga chama imara cha siasa nchini ili si tu kuimarisha demokrasia nchini bali pia kutoa mbadala kwa chama tawala na hata vyama vingine vya upinzani. Utekelezaji wa msingi huu wa chama umelipa. Haikuwa kazi rahisi, bali ni kazi makini yenye ujasiri wa kuepuka kujifanya Mbowe ndiye chama na badala yake kujenga chama taasisi ambapo wanachama wanaweza kusema demokrasia ndiyo CHADEMA.
Chini ya uongozi wake, Mbowe ameshirikiana na viongozi wenzake kupandisha chama kutoka chama cha tano mwaka 2000 mpaka chama cha pili mwaka 2010. Miongoni mwa Watanzania waliopata fursa ya kuchangia mabadiliko katika nchi kupitia juhudi hizi za Mbowe ni pamoja na mwandishi wa makala hii na makumi ya wabunge katika Bunge la Kumi, mamia ya madiwani walio katika halmashauri mbalimbali nchini na maelfu ya viongozi katika serikali za vijiji sehemu mbalibali nchini. Sisi kama wanachama tulipewa nafasi nzuri ya kukichangia chama kwa mawazo mbalimbali, na ni umoja wa mawazo yetu yote, matendo yetu sote, kila mmoja kwa nafasi yake, kwa uwezo wake, ndio ulisaidia chama kwenda mbele.
Wakati huo, na hadi leo, vyama mbalimbali vilionekana kuwazuia wanachama wao kutoa maoni huru kuhusu uendeshaji wa chama au hata uendeshaji wa taifa. CHADEMA kilikubalika kama chama chenye demokrasia, na haki za kila mwanachama ziliheshimika. Haki ya kupendekeza maoni binafsi na kuyatetea hadi mwisho ni haki ya msingi inayochangia katika kutofautisha CHADEMA na vyama vingi nchini.
Pamoja na kwamba haki hizi zipo katika misingi ya asili ya CHADEMA, ni haki ambazo ziliimarishwa zaidi katika kipindi cha Mwenyekiti wa tatu wa CHADEMA, Mbowe. Hii ndiyo misingi ambayo kila mwanachama wa CHADEMA anapaswa kujivunia na kuiendeleza ili kuendelea kutoa fursa kwa Watanzania kujenga upya nchi yao kupitia CHADEMA.
Iwapo Mbowe angeendekeza ufuasi wa watu au angetumia nafasi yake kama mwenyekiti kuwashawishi wanachama wawe na ufuasi wa watu, angepofuka na kamwe asingeweza kufikia mafanikio makubwa na ya kutiliwa mifano kama haya ya kujenga asasi imara ya chama cha siasa. Mifano dhahiri ipo kwenye vyama fulani fulani hapa nchini ambapo vyama vilipoanza tu kuwa ‘chama mtu’ badala ya ‘chama asasi’ vilianza kuporomoka mporomoko usiozuilika.
Dhumuni mojawapo la kisiasa la CHADEMA, kwa mujibu wa katiba yake ni kuendeleza na kudumisha demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kujenga utamaduni wa demokrasia katika jamii kwa kutambua haki za wengi katika maamuzi na pia kutambua haki za wachache kusikilizwa, kuheshimiwa na kulindwa, sambamba na kukubali ushindani huru, wa haki na wa wazi katika uchaguzi.
Dhumuni hili ni ushahidi tosha wa nia ya CHADEMA kujenga taifa la kidemokrasia lenye uvumilivu wa kisiasa na kurutubisha mawazo tofauti. Msingi huu na msingi wa ‘fursa’ imekuwa nguzo kubwa sana iliyoifikisha CHADEMA katika mwelekeo usiosimama wa kilele cha mafanikio ya chama cha siasa, kushika dola kufanya mabadiliko makubwa yenye maendeleo kwa wananchi wa Tanzania. CHADEMA, kama chama kinachopendekeza misingi hii kinajivunia pia kua mstari wa mbele katika vyama vinavyoendeshwa kwa kuheshimu misingi hii.
Utekelezaji wa dhumuni na misingi hii na misingi iliyoelezwa katika makala zilizotangulia (kuhakikisha rasilimali za nchi zinawafaa wananchi, kupinga ufisadi) unahitaji uumini wa misingi na si uumini wa watu. Ujasiri wa kuamini misingi ya chama na kuitekeleza kwa vitendo kama alivyofanya Freeman Mbowe ni ujasiri wa kuigwa na mwana demokrasia yeyote mwenye uzalendo, umakini, uadilifu na utu kwa Tanzania.
Chama kilichojaa ufuasi wa watu kitapasuliwa na nyufa za uongo, fitna, chuki, majungu na kujipendekeza. Chama cha misingi ndiyo chama tunachopaswa kujenga na kujivunia nacho.
Ni ujasiri wa kufuata misingi ndiyo unaweza kumfanya kiongozi mwenye timu iliyojaa watu wenye vipawa mbalimbali na uwezo mkubwa wa kuvutia ‘wafuasi’ kama CHADEMA kuweza kumudu jahazi na kuliendesha vema. Freeman Mbowe ameuweza mtihani huu mpaka sasa na kuendelea kufaulu mtihani huu ni moja ya silaha kubwa kwa CHADEMA katika juhudi zake za kuchukua uongozi wa taifa letu.
Misukosuko ya hapa na pale, inayosababishwa na wafuasi wa watu badala ya wafuasi wa misingi ya chama, haitakwisha. Hata hivyo, kipimo cha uwezo wa uongozi ni namna kiongozi anavyoshughulikia misukosuko. Ufuasi wa misingi ya chama ndio dawa ya kukabili misukosuko. Ufuasi wa watu ni sumu ya kukimaliza chama.
Makala inayo fuata itazungumzia namna gani CHADEMA ilishinda uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge wa Arumeru kwa kupitia misingi ya chama.
Mwandishi wa Makala hii ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
No comments:
Post a Comment