Saturday, January 5, 2013

Chadema yaihofia CCM kuchakachua Katiba mpya


MNADHIMU Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, ameilalamikia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa mikakati ya kupanga kuchakachua rasimu ya mabadiliko ya Katiba mpya. Kauli hiyo aliitoa juzi mjini hapa, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho Mkoa wa Iringa, na kusema kuwa pamoja na hatua hiyo ipo haja kwa Rais Kikwete, kuingilia jambo hilo.

Lissu alimtaka Rais Kikwete, atoe maelezo yenye majibu kwa Watanzania kuhusu mkanganyiko wa kisheria uliopo katika sheria ya tume ya mabadiliko ya katiba.

Kutokana na hali hiyo Lissu, alitangaza mbele ya mkutano huo kupeleka hoja binafsi bungeni wakimtaka Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aeleze ni nani kati ya wajumbe wake anayempelekea ujumbe Rais hali ya kuwa mchakato huo bado haujakamilika.

“Tunataka Rais atoe ufafanuzi wa mambo matatu makuu kama ambavyo amezungumza katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka jana.

“Atoe majibu ya kueleweka hadi kufikia Januari 14 la sivyo pale bungeni patawaka moto tutakapoanza vikao mwezi huu,” alisema Lissu.

Alisema jambo la kwanza wanalotaka Rais Kikwete alitolee ufafanuzi na majibu sahihi kuhusu mamlaka ya kuisemea Tume ya mabadiliko ya katiba, wakati yeye si msemaji wa tume hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, (CHADEMA), alisema CCM hawana haki ya kuzungumzia juu ya kulikomboa jimbo hilo, kwa kuwa wananchi walipiga kura zao halali, licha yakuwa CCM walitumia fedha nyingi.

"Ndugu zangu nimewasikia hawa viongozi wa CCM wanasema eti wanajipanga kulikomboa jimbo hili, kwani mlinikopesha? Si mlinipa wenyewe kwa ridhaa yenu.

“Mimi niwahakikishie hawa CCM wanaojinadi kulikomboa jimbo hili wanapoteza muda wao bure, walitumia mamilioni ya fedha na nguvu binafsi lakini nyinyi kwa maamuzi yenu mlinipa mimi, kwa hiyo waache kabisa maneno neno yao ya kuwa eti watalikomboa jimbo hili," alisema Mchungaji Msigwa.

No comments:

Post a Comment