UMATI mkubwa wa wakazi wa Jiji la Arusha, jana walijitokeza kwenye Uwanja wa mpira wa Ngarenaro, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka miwili ya mauaji ya watu watatu waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Maandamano hayo yaliyofanyika Januari 5 mwaka 2011, yakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na wabunge kadhaa wa chama hicho, yalilenga kupinga uvunjwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizotumika kumweka madarakani Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo.
Wanaodaiwa kuuawa siku hiyo kwa kupigwa risasi na polisi wakiwa kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ni Denis Shirima, Omary Ismail na raia wa Kenya, Paul Juguna.
Awali kabla ya mkutano huo wa jana kuanza majira ya saa nne asubuhi, viongozi wa CHADEMA wilaya na mkoa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walitembelea vituo mbalimbali vya yatima na kutoa msaada wa mchele kilo 20 na mafuta ya kula lita tano kwa kila kituo.
Katibu wa CHADEMA wilayani hapa, Martin Sarungi alisema wamepanga kuendelea na kazi hiyo hadi Januari 21 ambapo kwa siku ya jana walifanikiwa kutembelea kituo cha Huruma Group kilichopo Kata ya Ngarenaro kinachohudumia waathirika wa virusi vya ukimwi, kituo cha watoto yatima cha Ansaar Muslim Youth Center kilichopo Kata ya Sombetini kinachohudumia watoto wa kike zaidi ya 30, kituo cha watoto yatima cha Kibowa kilichopo Kata ya Lemara na kile cha Karama kilichopo Kata ya Olorien.
Sarungi alisema kuwa katika kipindi hicho wanatarajia kutembelea jumla ya vituo vya watoto yatima 12, wafungwa na mahabusu kwenye gereza kuu la mkoa la Kisongo na wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa lengo la kuwasaidia, kuwafariji na kuwatia moyo.
Kwa upande wake diwani wa viti maalum, Viola Likindikikoki (CHADEMA) alisema kuwa yeye na madiwani wenzake wataendelea na msimamo wa kutomtambua meya kwani licha ya kuingia kwenye wadhifa huo kinyume na sheria, pia kiti anachokalia kinanuka damu ya wananchi watatu wa Jiji la Arusha waliouawa bila sababu.
Naye kiongozi wa madiwani wa CHADEMA kwenye Halmashauri ya Jiji la Arusha, Isaya Doita aliwataka wananchi wa jiji hilo kuhakikisha wanashiriki kwenye vikao vya shule wanazosoma watoto wao ili waweze kuzibana bodi za shule na walimu wakuu juu ya michango mbalimbali wanayokusanya, lakini haina tija.
Alisema kuwa walimu wakuu wamejikita kwenye kukusanya michango pekee na kusahau majukumu ya kufundisha jambo linalothibitishwa na matokeo mabaya ya matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba na yale ya kidato cha pili ambapo amewataka wazazi kuwa wakali kuhoji fedha wanazochanga zinafanya nini kwani hazisaidii kuboresha taaluma kwenye shule hizo.
Doita ambaye pia ni diwani wa Kata ya Ngarenaro alitaka wananchi wanaofanya biashara chini ya miti wasitozwe ushuru kwani hawapati huduma yoyote kwenye maeneo hayo, hivyo hakuna sababu za msingi za kuwatoza kodi.
“Ebu tumchokoze Mungu kwa kutoa sadaka kwa yatima na wajane ili Mungu aamue kama Gaudensi anatakiwa kuendelea kukaa pale au hastahili, tunafanya jambo hili kwa uoga kwani ni gumu mno mpaka naomba Mungu amrudishie akili aweze kutubu na kugundua aliingia kwa hila ili baraka hizi tunazompa zisigeuke laana kwake,” alisema.
Alisema hata kama leo wakikubaliana na Lyimo kukaa madarakani, haimaanishi kuwa itabadili mfumo wa wananchi wa Arusha kuhudumiwa na serikali yao, bali itaendelea kujenga mfumo mbovu wa kuchakachua haki na sheria nchini kwani ni haki kwa serikali kuhudumia wananchi wake, hivyo haki hiyo wataendelea kuipata wakati wakiendelea kupinga uovu wa uvunjifu wa sheria za nchi bila aibu.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA mkoani hapa, Amani Golugwa alisema inasikitisha polisi kuua raia wasio na hatia ambao hata hawakuwa kwenye maandamano ya CHADEMA, huku ikiwaacha wengine wakiwa na ulemavu wa kudumu na kutolea mafano wa raia wa Kenya, Njuguna ambaye anadaiwa kuuawa muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi.
Baada ya kumuua, walimchukua wakampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mount Meru na kumbandika jina Chacha Mwita, lakini mimi na Lema tulipokwenda kuikagua maiti hiyo tulimkuta na kitambulisho kinachoonesha kuwa ni Paul Juguna kutoka Kajiado nchini Kenya,” alisema.
Naye katibu wa CHADEMA wilayani Arusha, Sarungi alisema kuwa wameanza maandalizi ya kupata ushindi kwenye chaguzi mbalimbali zijazo kwa kuanza kuorodhesha majina ya wanachama wake kwenye maeneo ya Jiji la Arusha.
Kwa upande wake, Mbunge Lema amesema kuwa hayuko tayari kuona Meya Lyimo akiongoza kikao wakati kuna watu walikufa, kuna yatima wameachwa, kuna wajane wameachwa kutokana na maandamano ya kumpinga.
“Tukiacha hili lipite wanaweza kufikia hatua ya kunyang’anya wananchi mali zao. Msivunjike moyo katika harakati za kupigania haki kwani hata Nelson Mandela alivumilia kukaa jela, leo tunaona Afrika Kusini iko huru basi na nyie msikate tamaa ili haki iweze kutendeka ndani ya taifa hili,” alisema Lema.
Alisema kuwa kuanzia sasa atahakikisha hakuna kikao cha baraza la madiwani wa jiji kinaitishwa bila wananchi kutangaziwa kama sheria inavyotaka ili waweze kuhudhuria kusikia kile kinachojadiliwa kwa mustakabali wa maendeleo ya jiji la Arusha jambo lililoamsha shangwe kwa wananchi hao.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment