Sunday, January 20, 2013

Zitto aikaanga Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Aitaka isigeuzwe na serikali kuwa TRA ndogo
Asisitiza isikubali serikali ichukue fedha bila mikataba
Hadi sasa mifuko hiyo inaidai serikali Sh trilioni moja
Asema hiyo inahatarisha fedha za wanachama


KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imeitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii isikubali kugeuzwa na serikali kuwa Mamlaka ndogo ya Mapato Tanzania (TRA).

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe ameonya kuwa serikali imekuwa ikijichukulia fedha kwenye mifuko hiyo bila kuingia nayo mikataba yoyote ya sheria.

Onyo hilo limetolewa na kamati hiyo baada ya kugundulika kuwa serikali imejilimbikizia madeni kwa kuiagiza mifuko hiyo kutekeleza miradi yake (serikali) bila kurejesha fedha hizo ambazo sasa zimefikia zaidi ya Sh trilioni moja hali inayohatarisha usalama wa fedha za wanachama wa mifuko hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye kikao cha kamati hiyo kilichokuwa kikipitia hesabu za Mfuko wa Pensheni ya Serikali za Mitaa (LAPF) Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alisema serikali inapaswa kutambua fedha hizo ni za wanachama.

Serikali imekuwa ikiiagiza mifuko hiyo kutumia fedha zake kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo bila kuwapo mikataba yoyote ya sheria, alisema.

“Yaani serikali imeigeuza mifuko ya hifadhi ya jamii kama TRA ndogo… hii ni hatari kwa sababu sasa inaonyesha inadaiwa zaidi ya Sh trilioni moja.

“Kama ninyi LAPF sasa mnaidai Sh bilioni 34 ukijumlisha na zile za ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 40… bado mifuko mingine kama NSSF na PSPF tunaona hali inazidi kuwa mbaya.

“Serikali imekuwa ikiendelea kuagiza wakurugenzi wa mifuko hiyo wajenge miradi hiyo; kwa mfano LAPF pia mmejenga Chuo cha Mandela kwa njia hii hii ambayo siyo sahihi hata kidogo.

“Tunataka kuanzia sasa serikali itakapoiagiza mifuko hii kujenga vyuo au kutekeleza miradi yake lazima iingie kwanza mkataba wa awali wa makubaliano kulinda fedha za mifuko hii.

“Hili ni suala ambalo pia tutalifikisha bungeni ili litiliwe mkazo kwa sababu fedha hizi ni jasho la wanachama siyo za serikali wala mifuko hiyo,” alisema.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa LAPF, Eliud Sanga, alisema katika hesabu za mwaka jana, mfuko huo unaidai serikali Sh bilioni 34 kutokana na ujenzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo.

Pamoja na mambo mengine mfuko huo ulipata hati safi kutokana na hesabu zake za mwaka 2011/12.

Wakati huohuo, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA) ametangaza nia ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu tatizo la ujangili nchini kuibana serikali kuchukua hatua stahiki kudhibiti tatizo hilo. 

Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, alisema tatizo hilo limeendelea kuwa sugu kutokana na baadhi ya vigogo kutoka Ikulu na viongozi wengine wa siasa wakiwamo mawaziri na wakurugenzi kujihusisha na biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu.

“Mnamo Desemba 31 mwaka jana niliwasilisha barua ya kusudio la kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu suala la tatizo la ujangili nchini.

“Lengo la hoja hiyo ni kuitaka serikali kulinda katiba ya nchi kwa kutekeleza matakwa ya katiba juu ya wajibu wa serikali katika kulinda rasilimali za nchi na haki ya wananchi kushiriki katika utunzaji wa rasilimali za nchi.

“Nimekwisha kupokea barua iliyoandikwa Januari 8 mwaka huu kutoka kwa Katibu wa Bunge ikiniarifu niwasilishe maelezo ya hoja yenyewe kwa Spika aweze kupata nafasi ya kujadiliwa katika mkutano ujao wa 10 unaotarajiwa kuanza mwezi huu.

“Takwimu zilizofanyiwa utafiti zinaonyesha kuwa robo ya pembe na meno ya faru na tembo duniani zinatokea Tanzania na taarifa zinazopatikana katika vyanzo mbalimbali nchini zinathibitisha kuwa ni takriban tembo 23,000 wanauawa kila mwaka sawa na wastani wa tembo 67 kwa siku.

“Hii ni hatari kwa rasilimali asili za taifa na pia kuhatarisha maliasili na utalii… ninayo dhamana na wajibu kwanza kama Mtanzania pia mwenye dhamana ya kusimamia serikali katika kulinda maliasili yetu na kudhibiti vitendo vya ujangili,” alisema.

Alisema kutokana na vitendo hivyo atalitaka Bunge kuunda kamati maalum kwa ajili ya kuchunguza tatizo hilo nchini.

“Hili tatizo linagusa watu wakubwa, hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wote tuweze kuwashughulikia wananchi hawa,” alisema.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment