Monday, January 28, 2013

CHADEMA yapanga mikakati ya urais 2015


KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana katika kikao maalumu kutafakari na kupanga mikakati katika mambo makuu manne, likiwamo la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014/2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Blue Pearl, ambako kikao hicho kinaendelea leo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wameamua kujifungia na kupanga mikakati ya Uchaguzi wa Serikali na Mitaa mwaka 2014 na ule Mkuu wa mwaka 2015 ili kujiweka sawa.
Hatua hiyo ya CHADEMA imekuja wakati ambapo vita ya urais imeendelea kushamiri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vigogo wanaotajwa kuwania nafasi hiyo nao wakionekana kujipanga na kuandaa mikakati kuelekea mwaka 2015.
CHADEMA kinaonekana kuwa ndicho chama pekee cha upinzani ambacho kimejizolea umaarufu mkubwa kwenye medani ya siasa katika miaka ya hivi karibuni, kikichukua nafasi iliyokuwa imekaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), hivyo kuonekana kuwa tishio dhidi ya chama tawala.
Upepo wa CHADEMA ulionekana kuvuma vema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambapo kilishika nafasi ya pili nyuma ya CCM, hali ambayo imesababisha macho na masikio mara zote kuelekezwa kwenye chama hicho kikuu cha upinzani, hasa linapokuja suala zima la kuangalia jinsi kilivyojipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika mkutano huo wa jana na wanahabari, Mnyika alisema kikao hicho cha siku mbili ambacho kinamalizika leo kimekuwa maalumu kwa sababu ya unyeti wake, lakini pia kimeshirikisha wabunge wa chama hicho na kuahidi kueleza namna uamuzi utakavyofikiwa mara baada ya kikao hicho.
Wakati wakipanga mikakati ya 2014/2015, pia vigogo hao wa CHADEMA wanaangalia namna ya ujenzi wa oganaizesheni ya chama nchi nzima wakati ambapo mwaka huu watakuwa na uchaguzi mkuu wa ndani.
Katika kujipanga huko, CHADEMA pia imesema kuwa imejiweka sawa kuangalia namna ya utekelezaji wa kile ambacho chama kiliahidi kukifanyia kazi kutoka katika maeneo ambayo ina wabunge sambamba na kutafakari namna ambavyo kambi rasmi ya upinzani bungeni inatekeleza majukumu yake.
Baada ya kikao hicho cha Kamati Kuu, Mnyika pia alisema CHADEMA inajiandaa kutoa kauli nzito kuhusiana na migogoro inayoendelea nchini, ikiwamo ya wafugaji na wakulima mkoani Morogoro, wanafunzi wa vyuo vya St. John, IFM pamoja na suala zima la gesi ya Mtwara mara baada ya kukutana na Baraza Kuu kesho, ambapo pamoja na mambo mengine watapatiwa taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wao Mtwara, ikiwa ni pamoja na mapendekezo yao.
Akisisitiza kuhusu suala hilo la gesi, Mnyika alisema kuwa mgogoro unaoshamiri wa gesi mkoani Mtwara ni matokeo ya sera mbovu ya usimamizi wa rasilimali za umma, na udhaifu wa kiongozi kushughulikia migogoro.
Katika hilo, Mnyika alisema wao kama CHADEMA wanatoa wito kwa rais pamoja na serikali yake kurekebisha kauli za vitisho zilizotolewa dhidi ya wananchi wa Mtwara, kwani ndiyo sababu ya kuendelea kuchochea mgogoro huo.
CHADEMA mbali na kumtaka rais kutoa kauli zinazojenga muafaka, pia wamewataka wananchi wa Mtwara wawe watulivu wakati kiongozi huyo wa nchi pamoja na serikali watakapokwenda kurekebisha kauli.
“Baraza kuu la chama litakutana na wilaya zote Tanzania na tunahitaji taarifa kutoka Mtwara na hatua wanazozipendekeza tuchukue, hii ni pamoja na migogoro mingine…hatua ambazo CHADEMA itachukua itatolewa baada ya mkutano wa Baraza Kuu la chama,” alisema.
Kuhusu suala la baadhi ya wabunge kuhongwa na kwamba wao ndio wamewachochea wananchi kufanya vurugu, Mnyika alisema jambo hilo kamwe lisipotoshwe na kuitaka serikali ijibu hoja za wananchi.
Aidha, akifafanua kuhusu hilo Mnyika alikwenda mbali zaidi akisisitiza kuwa wabunge pia wametofautia mitizamo, lakini akasisitiza kuwa wananchi wamesukumwa kudai masilahi yao.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment