LICHA ya tuhuma mbalimbali za ufisadi ambazo zimekuwa zikimkabili aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, ametaka Katiba mpya iipe meno Tume ya Maadili ili kuwadhibiti wala rushwa.
Chenge ambaye kabla Rais Jakaya Kikwete hajamsafisha, kwa muda mrefu pia alikuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE- System.
Hiyo ilimfanya awekwe kwenye orodha ya vigogo wanaodaiwa kuficha fedha nje ya nchi.
Licha ya tuhuma hizo zote jana wakati akitoa maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alitaka Katiba mpya iipe madaraka Tume ya Maadili ili rushwa iondoke.
Alisema tume hiyo lazima ipewe meno na kufanya kazi kwa uchunguzi bila kuingiliwa wala kuwa na woga wa mtu au kiongozi yeyote ili kutoa weledi kwa taifa.
Mchakato wa ununuzi wa rada, ambao uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, ulimuacha Chenge kwenye tuhuma nzito za rushwa.
Kuhusika kwa Chenge kulitokana na nafasi ya uanasheria mkuu wa serikali aliyokuwa akiishikilia, hivyo kutajwa kuwa kiungo muhimu aliyefanikisha ununuzi wa rada hiyo kwa gharama kubwa kupita kiasi ya shilingi bil. 40.
Chenge ambaye huko nyuma alipata kuzungumzia suala hilo ikiwa ni pamoja na kumiliki kwake akaunti nje ya nchi zinazohusishwa na mlungula wa ununuzi wa rada, hata hivyo alisafishwa na Rais Kikwete, ambaye alisema kuwa hakukuwa na rushwa kwenye ununuzi wa rada.
Mbali ya Rais, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, alipata mara mbili kunukuliwa akisema Chenge hakuwa na kesi ya kujibu katika kashfa hiyo ya rada.
Mbali ya hilo la rushwa, katika maoni yake hayo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani, ametaka Katiba mpya pia iweke sheria ya kuwa na mgombea binafsi.
Chenge ambaye ni msomi wa sheria amependekeza sheria hiyo ya mgombea binafsi iwaguse wanaotaka kuwa wagombea binafsi katika ngazi ya rais, ubunge na udiwani, lakini alitaka ziwe tofauti na vyama vingine vya upinzani.
Akizungumza baada ya kuwasilisha maoni yake katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana jijini Dar es Salaam, Chenge alisema wagombea binafsi kama wataachiwa kuwa huru wanaweza kukiuka msingi ya Katiba hasa katika suala la dini na ukabila.
Kuhusu suala la madaraka ya rais, Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi alitaka madaraka ya rais kutopunguzwa huku akidai kuwa katika kazi za uteuzi asaidiwe na tume mbalimbali.
Kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othuman M. Othuman, aliwataka waandishi wampe muda ili aweze kuzungumzia alichikitoa katika tume hiyo.
“Nimeongea matatizo ya muungano wa sasa, kipi cha kuzingatia, misingi na namna ya kurekebisha, lakini siwezi kuzungumza nanyi kwa dakika tano hazitatosha kabisa, matokeo yake mtaandika kitu sicho, kama mnaweza nipigieni simu kuanzia kesho (leo) maana sasa hivi nawahi boti, kama humo ndani nimeongea kwa masaa mawili na bado wamekuwa na maswali mengi je, dakika tano zitatosha kwenu?” alihoji mwanasheria huyo.
Katika hatua nyingine, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi amewasilisha maoni yake ambapo tume hiyo ilimfuata nyumbani kwake.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment