Monday, January 28, 2013

TAMKO LA SHURA YA MAIMAMU MKOA MTWARA KUHUSU SAKATA LA GESI ASILIA ILIYOPO MSIMBATI –MKOANI MTWARA

TAMKO LA SHURA YA MAIMAMU MKOA MTWARA KUHUSU SAKATA LA GESI ASILIA ILIYOPO MSIMBATI –MKOANI MTWARA, TAREHE 18/01/2013.
Yaliyomo:

1. Utangulizi
2. Tatizo la Gesi Mtwara
3. Majibu ya Serikali kwa madai ya WanaMtwara na Athari zake
4. Ukweli kuhusu Tatizo la Gesi Mtwara
5. Maoni na Msimamo wa Shura ya Maimam Mtwara Juu ya Kadhia ya Gesi
1. Utangulizi
Sifa zote njema zinamstahili Allah (Subhanahuwata’ala) ambaye uhai wa nafsi zetu umo mikononi mwake naye ni msimamia kila jambo na Ambaye ametuteremshia mwongozo ili tuweze kusimamia haki katika ardhi na hatimaye kuishi maisha ya wema na uadilifu. Rehma na Amani zimuendee Mtume wake mtukufu Muhammad (Swalallahu-alaihi-Wasalaam).
Allah(s.w) anasema:
“(Vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ni vya MwenyeziMungu.Na kama mkidhihirisha yaliyomo katika nyoyo zenu,au mkiyaficha,MwenyeziMungu atakutakeni hesabu ya (yote) hayo;kisha amsamehe amtakaye(kwa kuwa katubia) na amuadhibu amtakaye(kwa kuwa hakutubia).Na MwenyeziMungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu”( Qur an 2:284)

Sote tunafahamu kuwa kwa sasa wananchi wa Mtwara wanaendelea kuilalamikia serikari kuhusu mpango wake wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam. Wananchi wa Mtwara walijitokeza kama kundi Tarehe 27 mwezi wa 12 mwaka jana (2012) kuieleza serikali kuwa wanapinga mpango huo wa kusafirishwa gesi unaotekelezwa kupitia mradi wa bomba wa gesi ambao kwa mujibu wa serikali ujenzi wake utakamilika katika kipindi cha miezi kumi na minane.
Baada ya maandamano hayo makubwa sasa suala la gesi limechukua sura ya mjadala wa kitaifa kwani kila kona ya Tanzania sasa inajadili suala hili kwa namna mbalimbali na kwa hapa Mtwara hali inazidi kuwa ngumu zaidi kwani wananchi wanazidi kujizatiti zaidi kimisimamo kuwa gesi haitoki na ikibidi basi wako tayari kufa na hilo likikaririwa katika kauli mbiu maarufu kwa sasa ya GESI KWANZA UHAI BAADAE.

Sisi shura ya Maimam Mkoa wa Mtwara tumeona ni vema tutoe Tamko letu baada ya uchunguzi wa kina juu ya Kadhia hii ya gesi kwa lengo la kuishauri na kuinasihi serikali juu ya nini kifanyike ili kuleta hali ya amani katika misingi ya haki na uadilifu. Kuna sababu kuu nne (4) ambazo zimetusukuma kutoa Tamko hili.

Kwanza, tumeona kuwa sisi ni sehemu ya jamii ya WanaMtwara na ni watanzania ambao kwa uelewa wetu juu ya kadhia hii tuna haki na wajibu wa kutoa msimamo wetu juu ya kadhia hii ili dhima na wajibu ya kulinda amani katika nchi hii tuwe tumeitekeleze kwani ni haki yetu.

Pili, Mpaka sasa kumekuwa na upotoshaji mkubwa juu ya kile kinachoendelea katika kadhia hii ya gesi kuanzia kwa viongozi wa serikali na hata baadhi ya watu binafsi wanojitokeza kutoa maelezo, misimamo au maoni yao kuhusu kadhia hii.

Tatu, mpaka sasa serikali haijaonesha dhamira ya dhati ya kulipatia ufumbuzi suala hili na kuamua kulipuuza kitu ambacho ni hatari kwani kwa hali jinsi ilivyo amani inaweza kuvurugika wakati wowote kama hali itaendelea kuwa kama ilivyo sasa.
Nne, sisi tuna uelewa mkubwa wa misimamo na hisia za WanaMtwara juu ya suala la gesi kwani tunaishi nao na tunaona na kusikia hisia zao wanazozidhihirisha kwa vinywa vyao endapo wataendelea kupuuzwa. Hata hayo maandamano ya tarehe 27 si mwanzo wa malalamiko ila ni kilele tu cha kile ambacho kimekuwa kikaendelea chini kwa chini tangu pale ambapo wananchi walihakikishiwa kuwa sasa gesi inasafirishwa na kupelekwa Dar es Salaam. Kwa hiyo tunaona wazi kuwa kwa namna serikali yetu ilivyo haitaweza kukabiliana na hali hiyo pale machafuko yatakapoanza.

2. Tatizo la Gesi Mtwara
Kimsingi, tatizo la gesi Mtwara ni fupi kueleweka na liko wazi. Serikali ndio kiini cha tatizo hili na sio wananchi wa Mtwara. Serikali imekuja na mpango wa kuisafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Imetangaza na kuzindua mradi wa bomba la gesi litakalojengwa kwa miezi kumi na nane (18) kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam. Wananchi wa Mtwara wanapinga mradi huo na wazo au uamuzi mzima wa kuisafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na kuipeleka sehemu yeyote ile Tanzania na Dar es Salaam ikiwepo bila Mtwara kunufaika kwanza na gesi hiyo asilia. Kwa msingi huu wanachotaka wao ni kwamba kituo cha kuchakata gesi hiyo asilia kijengwe Mtwara badala ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Msingi wa dai hili ni kwamba wananchi wa Mtwara wanaamini kuwa kituo hicho cha kuchakata gesi asilia kama kitajengwa Mtwara kitatoa fursa kubwa ya kushawishi wawekezaji ambao wataweza kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi ya gesi asilia na hivyo kuchochea maendeleo ya Mtwara kwa ujumla. Kwa hiyo kama gesi hii itaanza

kufanyiwa kazi mkoani Mtwara kwanza kwa namna hii, hapo wananchi wataridhia baadaye gesi hiyo kusafirishwa katika mikoa mingine ya nchi ikiwa imechakatwa kwa ajili ya matumizi ya Kitaifa ambayo WanaMtwara hawayapingi.
Kwa hiyo hii ndio HOJA ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kwamba kwa hoja hii, ni wazi kwamba wananchi wa Mtwara si wabinasfi na wala sio wachoyo na hawapingi watu wengine katika maeneo mengine ya nchi kunufaika na gesi hii. Pia kwa hoja hii wananchi wa Mtwara hawapingi tu kusafirishwa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa UJINGA. Huu sio ujinga bali wananchi wamesimamisha HOJA ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi kwa uzito uleule wa namna HOJA ilivyosimama
.
3. Majibu ya Serikali kwa madai ya WanaMtwara na Athari zake
3.1 Majibu ya Serikali
Kwa mujibu wa WanaMtwara, mpaka sasa serikali haijatoa jibu la msingi wala ufafanuzi unaoeleweka dhidi ya HOJA ya WanaMtwara kuhusu gesi kuanzia katika mkoa, wizara yenye dhamana na masuala ya gesi na hata mheshimiwa raisi.
Mkuu wa mkoa yeye hakutaka kuwa na maneno mengi bali aliongea kwa ufupi tu na kurudiarudia kauli yake. “Alisema kuwa watu wa Mtwara ni wapuuzi kwa madai yao hayo”. Akaendelea tena kidogo kwamba “tena amewasamehe kuwaita wapuuzi walistahili kuitwa wahaini”. Kwa hiyo HOJA madhubuti iliyotolewa na wananchi wa Mtwara ilijibiwa kirahisi tu kiasi hicho kwa kejeli na jeuri lakini hatimaye kejeli na jeuri hizo za mkuu wa mkoa wa Mtwara hazikujaribu hata chembe kujibu HOJA nzito ya wananchi. Yeye akawa amemaliza kazi na kuwaachia wakubwa wake.

Waziri wa Nishati na madini naye akaja na mlolongo mrefu wa maelezo yasiyoshikana na hata kuelewaka kwa mnasaba wa HOJA ya wananchi wa Mtwara. Kasema Dar es salaam kuna viwanda vingi kuliko Mtwara. Matumizi ya gesi Mtwara ni madogo kuliko Dar es Salaam. Gesi imegunduliwa mbali na Mtwara kwa hiyo wananchi wa Mtwara hawapaswi kulalamika na mengine mengi mfano wa hayo. Kimsingi na Mheshimiwa waziri nae akapita njia ileile ya mkuu wa mkoa na hatimaye na yeye hakujibu HOJA ya wananchi kama ilivyosimama.

Mheshimiwa raisi naye akatoa maelezo yake katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa kumi na mbili mwaka jana (2012). Kubwa alilolifanya ni kusisitiza tu kwamba suala la kutosafirishwa gesi kwenda Dar es Salaam HALIKUBALIKI. Naye katika maelezo yake aligusagusa tu vitu fulanifulani kama vile umuhimu wa Dar es Salaam kwa kuwa inachangia sehemu kubwa ya pato la taifa (asiliamia 80) na kwamba viwanda vingi vipo Dar es salaam. Pia alisisitiza kuwa sera ya rasilimali iko wazi kwamba lasirimali zote ni mali ya taifa.

Maelezo yake yote ilikuwa ya kujaribu kuhalalisha mpango wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na hatimaye hakuweza kutoa majibu ya HOJA ya wananchi Mtwara.
Kwa hiyo mpaka sasa tangu alipoanza kuongea mkuu wa mkoa wa Mtwara, waziri wa Nishati na madini na Mheshimiwa raisi wananchi wa Mtwara hawajapata jibu la msingi kwa HOJA yao nzito juu ya Gesi.
3.2 Athari za Majibu ya Serikali
Kimsingi, wananchi wa Mtwara baada ya kuchambua Majibu ya Viongozi wa serikari hawajaona maelezo yanayojibu HOJA yao. Kwa sababu zifuatazo:





Kwanza, majibu yote tangu ya mkuu wa mkoa, waziri na raisi yanajaribu kueleza vitu vinginine na sio hoja yenyewe ya wananchi wa Mtwara. Majibu yote yanajikita katika kuelezea upingaji wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam lakini sababu ya wananchi wa Mtwara kupinga kusafirishwa gesi haiguswi. Wananchi wanataka kituo cha kuchakata gesi asilia na ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MEGAWATT 300 kijengwe Mtwara na sio Kinyerezi Dar es salaam kwa sababu kikijengwa Mtwara kitachochea maendeleo. Kwa upande mwingine, kwa kuwa wananchi wanaamini kuwa gesi ghafi hiyo ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam wao hawatanufaika (kwa msingi ule wa kujengwa kituo cha kuchata gesi Mtwara), serikali ilitakiwa ijikite katika kuwaonesha wananchi kinaga ubaga namna gesi hiyo itakavyoendelea kuchochea maendeleo ya Mtwara hata kama ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam na sio kusema sema tu kwamba wananchi watanufaika bila kuweka wazi watanufaikaje. Kwa Majibu haya, wananchi wa Mtwara wanaona kuwa serikali yao haikujipanga kuona Mtwara wananufaika na gesi na ndio maana wanaikwepa HOJA yao.

Pili, serikali pamoja na kushindwa kutoa majibu ya msingi katika hoja ya wanaMtwara, imekuwa ikitumia muda mwingi kuwaeleza wananchi wa maeneo mengine ya nchi kupitia vyombo vya habari kama vile, vipindi vya televisheni, magazeti na hotuba na kuwaacha wahusika wenyewe ambao ni wakazi wa Mtwara. Rais, na sio Waziri wa Nishati na madini, alitakiwa aje azungumze na wananchi ili wananchi wajibiwe HOJA yao kama ilivyo.

Tatu, serikali imetoa shutuma zisizo za kweli kwa wananchi wa Mtwara. Hata kama serikali haipendezwi na madai ya WanaMtwara bado ilipaswa ieleze kile wanachokidai na sio kuwabambikia hoja tofauti. Serikali imesema wananchi wa Mtwara WANAPINGA gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam na kuishia hapo. Kufanya hivyo kumeongeza chuki kwa wananchi wa Mtwara na wanaona kuwa serikali inatafuta uhalali wa kupitisha jambo lake. Inajenga mazingira ya wananchi wa Mtwara waonekane wabinafsi, wachoyo na hatimaye waiunge mkono katika kupuuza dai la wananchi wa Mtwara. Lakini kinyume chake hata wananchi wa maeneo mengine wameona dosari hiyo ya serikali na wao kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari wanajaribu kuwaelewesha watanzania wengine kuhusu HOJA ya msingi ya wananchi wa Mtwara. Kwa hali hii serikali tunaiona inapoteza heshma yake na uaminifu si tu kwa wananchi wa Mtwara bali kwa kila Mtazania makini anayeitakia heri nchi yake.

Nne, serikali imekosea kuona kuwa msingi wa madai ya WanaMtwara ni uchochezi wa wanasiasa. Serikali inapaswa kufahamu kuwa wanasiasa ni wadandiaji wazuri wa hoja mbalimbali za kijamii baada ya kuibuka kwake. Kilichoanza hapa ni manung’uniko ya wananchi juu ya kusafirishwa kwa gesi na baada ya wanasiasa kuona kuwa hakuna anayewasemea wananchi ndio wakapenya hapo na kuwahamasisha juu ya namna ya kupaza sauti zao lakini tatizo lilikuwepo hata kama tungekuwa tunaongozwa na chama kimoja. Kwa hiyo hili ni dai la WANANCHI WA MTWARA sio dai la wanasiasa.

Kwa hiyo kwa ujumla majibu ya serikali kwa wananchi yamezidi kuongeza tatizo na wananchi wa Mtwara wameona kuwa serikali yao imeamua kuwapuuza. Na kwa sababu serikali imeshindwa kutoa majibu sahihi kwa HOJA ya wananchi ya Mtwara, kwa kufanya hivyo imehalalisha kila fikra itakayokuja katika kichwa cha Mwananchi wa Mtwara kuhusu hatua za serikali kusafirisha gesi iwe sahihi. Na fikra kubwa waliyonayo wananchi wa Mtwara kwa sasa ni kwamba serikali imeamua kuwadhuluma neema iliyopatikana katika maeneo yao na inawapelekea walewale wachache wakanufaike na neema hiyo. Na kilele cha mtazamo huu ni ile kauli mbio yao ya GESI KWANZA UHAI BAADAYE. Yaani kwao wao ni bora kufa kuliko kuona gesi inasafirishwa kwenda Dar es salaam katika namna ambayo wao hawakubaliani nayo. Wanaona baada ya hapo wataendelea kunyanyaswa na mwisho watajinyonga kwa udhalili kwa hiyo wanaona ni bora wafe na GESI.

Kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuszi bwana James Mbatia mjini Mtwar hivi karibuni pamoja na kuwekewa magogo naibu waziri wa Nishati na madini Bwana Simbachawene kule Msimbati ni ishara tu ya madhara ya serikali kupuuzia madai ya WanaMtwara.

4. Ukweli kuhusu Tatizo la Gesi Mtwara
Kwa uzoefu tulio nao kwa wananchi wa Mtwara tangu ukoloni hawajawahi kufaidi matunda ya maendeleo ya kijamii na wamebaki kuwa duni ukilinganisha na mikoa mengine. Serikali za kikoloni (ya Wajerumani na ya Waingereza) zilitumia nguvu kazi ya wananchi wa Mtwara pamoja na rasilimali zao kwa ajili ya kuendeleza maeneo mengine ya Tanzania na kuwaacha watu wa mikoa ya kusini wakiwa hoi kwa umasikini wa kutupwa. Baada ya Uhuru, serikali pia imefuata nyayo zilezile za kulipuuza eneo hili la kusini mwa Tanzania na kulifanya liwe msindikizaji wa maendeleo kwa mikoa mingine.

Katika sura hii, tafsiri ya haraka waliyokuwa nayo wananchi wa Mtwara kuhusu hatua ya serikali kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam bila kujali madai ya wananchi wa Mtwara ni kuwa huu ni muendelezo uleule wa kubeza maendeleo ya mikoa ya kusini. Kwao wao hapa hawaoni jipya ila wao ndio wameamua kuja na staili mpya ya kudai maendeleo yao na KUPINGA HUJUMA ya kimaendeleo ambayo wamekuwa wakifanyiwa kipindi kirefu sasa. Wananchi wa Mtwara wanamlolongo ufuatao wa Mashaka na MATATIZO waliyoyapata katika historia ya maisha yao tangu ukoloni:
 Katika kipindi cha ukoloni wa wajerumani (1885-1917), wananchi wa mikoa ya kusini walitumika kama nguvu kazi ya kuendeleza maeneo mengine yenye migodi na mashamba. Wengi walinyang’anywa ardhi zao na kulazimishwa kuacha familia zao na kwenda Kufanya kazi kwa nguvu katika maeneo mengine. Katika sura hii, mikoa ya kusini iliachwa bila kuendelezwa ili iwe kitovu cha kutoa wafanyakazi (manamba) wa kutumika katika mashamba ya wakoloni katika maeneo mengine ya nchi. Ushiriki wa watu wa Mtwara katika vita ya majimaji ilikuwa ni kielelezo cha kupinga dhulma dhidi yao.

 Katika utawala wa waingereza, mwendo ulikuwa ni uleule ambapo waingireza Walipewa jukumu la kuitawala Tanganyika wakati huo na League of Nations kwa hiyo hakukuwa na mkakati wowote wa kuendeleza mikoa ya kusini kwa uchumi. Mikoa ya kusini ilitengwa na kubaguliwa kiuchumi. Mwandishi wa Kifaranza Libenow (1971) katika kitabu chake Colonial Rule and Political Development in Tanzania: The Case of Makonde ukurasa wa 11 anaandika kwamba waingereza waliita Mtwara kuwa ni “Cinderella Region of a Cenderalla Territory” yaani eneo lililotengwa/kubaguliwa la ukanda uliotengwa/kubaguliwa. Waingereza waliweka msimamo kuwa Mtwara na kusini kwa ujumla si sehemu ya kuendelezwa kiuchumi na walifuata nyao zilezile za wajerumani.

 Baada ya Uhuru, wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wakapata bahati mbaya nyingine kwani ndoto zao za kudhani kuwa wataendelezwa kiuchumi Ndani ya Tanzania huru ziliota mbawa. Serikali ya Tanganyika na baadaye Tanzania ilifuata nyayo zilezile za wakoloni wa kijerumani na waingereza. Kwanza, mikoa ya kusini ikatengwa tena kwa shughuli nyingine ya uslama wa nchi. Kipindi hiki Mikoa ya kusini ikawa ni uwanja wa mapambano ya kuzikomboa nchi za kusini mwa Afrika ili wapate Uhuru. Miundombinu ikazidi kuwa mibovu na hakukuwa na maendeleo yeyote ya maana. Kwa ujumla wananchi wanalalamika juu ya haya:

 Mtwara ina Bandari yenye kina kirefu katika Afrika ya mashariki yote lakini mpaka sasa mipango ya kuiendeleza imekuwa ni kizungurumkuti. Wananchi wana taarifa kuwa mipango ya kuiendeleza Bandari ya Mtwara imepindishwa na kupelekwa Bagamoyo.
 Wananchi wanakumbuka kwa uchungu zao lao la biashara la muhogo ambalo serikali ya Tanzania huru imeliacha linakufa kuwa zao la biashara. Wakulima wengi wanalima mihogo mingi na wanaishia kuitupa tu baada ya kuoza maana si tu kwamba haina soko bali hata teknolojia ya kulitunza kwa muda mrefu hawana. Mashamba wanayo na wanalima kwa bidii wanavuna mihogo mingi lakini wa kumuuzia tayari serikali ilishampoteza na haina mpango wa kulifufua zao hili kama zao la biashara.

 Wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wana kilio cha muda mrefu cha zao la korosho na mpaka sasa serikali inababaisha tu haina mpango wowote wa kuboresha soko la zao hili. Wananchi sasa wanapomaliza kuvuna korosho zao wanaambulia vikaratasi tu na kutakiwa wasubiri pesa zao kwa muda mrefu bila kuzipata. Ingawa ni jambo liliowazi kuwa zao la korosho linachangia kiasi kikubwa tu cha fedha katika serikali. Kwa mfano, kuna takwimu zinaonesha kuwa Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni sawa na shingi billion mia mbili arobaini na moja na million mia sita (TZsh241,600,000,000). Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola 130 milioni sawa na bilioni mia mbili na nane (208,000,000,000) wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu sawa na shingi billion themanini na nne na milioni mia nane (84,800,000,000).

 Wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wanazidi kulia tu na kusuasua kwa ujenzi wa Barabara ya Mtwara-Lindi-Dar es Salaam. Wanazidi kuumia wanapoona ile mikoa inoyoheshimiwa na serikali ikiwa na Barabara nzuri zinazopitika tena ujenzi wake umekamilika kwa muda mfupi sana. Miaka minane ya Mh. Rais Kikwete zile kilomita 60 za barabara kutoka Ndundu mpaka Somanga hazijaisha lakini gesi anataka kuiwekea bomba na mradi ukamilike kwa miezi 18.  Wananchi wameshuudia reli ya kusini iking’olewa bila sababu za msingi na huku ikijulikana kuwa reli ni moja ya miundombinu muhimu katika kuchochea uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Reli haikung’olewa katika mikoa ambayo serikali inaiheshimu.  Wananchi wa Mtwara wameshuhudi mashine ya maji kitangali Newala ikiondolewa na kupelekwa Dodoma ambayo ilikuwa msaada kutoka Finland.  Wananchi wa Mtwara wameshuhudia kiwanda cha samaki Mtwara kikiondolewa na kupelekwa Dar es Salaam.

 Wananchi wa Mtwara wameshuhudia taa za mwanga mkali za uwanja wa ndege Mtwara ziking’olewa na kupelekwa Arusha.  Wananchi wa Mtwara wameshuhudia mkataba wa kutumika bandari ya Mtwara na Malawi kibiashara ukipindishwa na kupelekwa Bagamoyo.  Wananchi wa Mtwara wamekaa na giza kwa muda mrefu na giza hilo limechangia kutokuwepo kwa kichocheo cha uchumi kwa kukosekana umeme wenye uhakika. Ni hivi karibuni tu baada ya kugunduliwa gesi na kumekuwepo na nishati ya umeme ambao hautoshi kwa maana ya kumfanya mjasriamali mwenye mtaji kuweza kuwekeza Mtwara katika sekta ya viwanda. Mwenyezi Mungu anasema:- “Kwa hakika MwenyeziMungu anaamrisha uadilifu,na kufanya ihsani,na kuwapa jamaa(na wengineo),na anakataza uchafu na uovu,na dhuluma.Anakunasihini ili mpate kufahamu(mfuate)”(Qur’an 16:90)

Amesema Mtume(s.a.w) “Mwenye kuuona uovu mmoja wenu basi na auondoshe kwa mkono wake ,kama akishindwa basi atumie ulimi wake kushajiisha uovu uondoke na akishindwa basi achukie moyoni mwake na huko kuchukia ni udhaifu wa imani”(Bukhari na Muslim)

Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa muda mrefu wamekuwa wakichukia tu mioyoni mwao maovu na madhila yote waliyokuwa wakifanyiwa na serikali lakini sasa imefika wakati tuseme na tudhihirishe maovu hayo waziwazi ili asaa viongozi wajirekebishe na wawafanye uadilifu kwa watu wao kama si hivyo hatua inayofuata kwa mujibu wa hadithi ni kutumia mkono kuondosha uovu.

Kwa hiyo, huu ndio mlolongo wa madhila ambayo wamekumbana nayo wananchi wa Mtwara. Wao wanaamini kwamba kutoendelezwa kwa maneo yao ni matokeo tu ya kiubaguzi kwa kuwa serikali tangu ile ya kikoloni mpaka hii ya leo inaliona eneo hili kama ni eneo ambalo si muhimu na hivyo ni haki yao kubaki nyuma. Katikati ya mashaka hayo Mwenyezi Mungu amejaalia kuwepo kwa gesi asilia. Kwa Ugunduzi huu wa gesi watu wa Mtwara waliamini kuwa sasa hivi serikali itaona aibu na kuwa waadilifu na kwamba itatumia gesi hii kama kichocheo kilicholetwa na Mwenyezi Mungu ili kukuza maendeleo ya Mkoa wa Mtwara na Lindi. Walikuwa na matumaini hayo kupitia kauli na ahadi za viongozi mbalimbali akiwemo rais mstaafu wa awamu ya tatu na hata Mh.Rais Kikwete mwenyewe kwamba ukombozi wa kiuchumi sasa umefika kwa mkoa wa Mtwara pia Ilani ya chama cha mapinduzi(2010) katika ibara ya 63(h) na (k) ilianisha miradi ya kinyerezi(240MW) na mradi wa Mnazi bay(300MW) kama miradi miwili tofauti inayojitegemea. Mwenyezi Mungu nasema:

“Na timizeni ahadi mnazozitoa kwa jina la MwenyeziMungu mnapoahidi;wala msivunje hizo ahadi baada ya kuzithubutisha,hali mmekwisha mfanya MwenyeziMungu kuwa shahidi wenu.Hakika MwenyeziMungu anayajua yote mnayoyayafanya”(Qur’an 16:91)
Sasa ghafla, wanakutana na mpango wa kustukiza wa serikali kutaka kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam bila kueleza kwa nini kituo cha kufulia umeme unaotokana na gesi asilia inakopatikana gesi hiyo kisijengwe Mtwara?. Wanapojaribu kuihoji serikali wanaambulia matusi, kejeli na kupuuzwa kutoka kwa viongozi wao waliowategemea kuwatetea. Kwao wanaona ni hujuma tu wanataka kufanyiwa kama walivyofanyiwa huko nyuma na ndio maana wameamua KUFA na GESI indepo na mara hii serikali itawapuuza. Serikali imefikia upeo wa juu wa kuwapuuza wana Mtwara na WanaMtwara nao wamefikia upeo wa juu wa uvumilivu na ndio maana wanasema GESI KWANZA UHAI BAADAYE. Haya ndio mazingira halisi ambayo ndiyo KIINI cha mgogoro wa gesi Mtwara. Sio wanasiasa bali ni historia ya kudharauliwa ndio yaliyoibua mgogoro huu wa gesi kama tulivyoeleza hapo juu. WanaMtwara wana mfano wa gesi ya Songosongo inayopelekwa Dar es Salaam. Zipo taarifa zinazoelezea kwamba kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa asilimi 0.3 (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ni baada ya juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa.

5. Maoni na Msimamo wa Shura ya Maimam Mtwara
5.1 Msimamo wa Shura
Shura ya Maimam Mtwara imesikitishwa na kuwepo kwa mgogoro kati wa wananchi wa Mtwara na serikali katika sula la gesi. Msimamo wetu kuhusu Kadhia hii ya gesi ni kwamba serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake kuhusu suala la gesi kwa wananchi wa Mtwara katika maeneo yafuatayo:
 Kwanza, serikali imekosea kufikiria kujenga kituo cha kufulia umeme unaotokana na gesi asilia Kinyerezi Dar es Salaam badala ya Mtwara. Uamuzi huu haujazingatia historia ya wananchi wa Mtwara iliyowatumbukiza katika umasikini wa kutupwa. Kwa mantiki hiyo, serikali hajaweza kujenga hoja ambayo itawafanya wananchi wa Mtwara waridhike na mradi huo wa serikali.

 Pili, serikali haijatoa elimu na maelezo ya kutosha kuhusu Matumizi ya gesi hiyo iliyogunduliwa Mtwara ili WanaMtwara wapate fursa ya kuhoji kama mradi huo utakuwa na manufaa kwao au la. Wakati umepita wa kuwachukua wabunge tu na kuwalipa posho lukuki halafu kuwataka wapitishe mradi. Katika mazingira haya wabunge hukosa ujasiri wa kukosoa mradi. Kwa hiyo serikali ilitakiwa kushuka chini kwa wananchi wenyewe kwa jambo zito kama hili.
 Tatu, serikali imeshindwa kutumia busara na hekima katika kushughulikia madai ya WanaMtwara kuhusu gesi. Badala yake, imetumia lugha chafu ambayo imejenga chuki kubwa miongoni mwa wananchi kwa serikali na Viongozi wake.

 Nne,serikali imeendeleza hali ileile ya kudharau mambo ya mikoa ya kusini. Majibu ya serikali kwa wananchi wa Mtwara yamekuwa rahisi mno tofauti na hoja waliyoitoa wananchi. Mpaka sasa serikali imeshindwa kuona kuwa jambo hili ni zito na hatima yake sasa hivi limefikia hatua mbaya ambayo serikali haiwezi kuitatua.

 Tano, serikali imeendeleza utaratibu uleule wa kutumia propaganda katika masuala mazito kama hili la gesi. Imetoa kauli za uwongo kama kusema kwamba wananchi wa Msimbati wanapatiwa umeme bure, wamejengewa barabara mzuri ambazo hata Mwananchi wa kawaida anapata picha mbaya juu ya serikali yake na kupoteza Imani ya serikali.

 Sita,Shirika la Maendeleo ya Petroli(TPDC) wanasema moja ya mafanikio yao ni kuishauri serikali juu ya mradi wa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dares-Salaam,haya yalielezwa katika warsha ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kamati ya ushauri ya mkoa wa Mtwara(Rejea kitini ya warsha hiyo tarehe 20 Julai,2012-Mtwara).Hii nayo ni hujuma kubwa kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Kwa hiyo, hizi ndizo nukta muhimu ambazo serikali imefanya sivyo kwa wananchi wa Mtwara na kwa lugha nyepesi ni kwamba misingi ya uadilifu, uwazi na utawala bora katika kusimamia rasilimali za nchi kwa maslahi ya wananchi haijazingatiwa.

5.2 Maoni ya Shura kwa Serikali
Baada ya kutafakari kwa kina namna mgogoro huu ulivyochukua sura mpya, shura inaishauri serikali kama ifuatavyo:
 Kwanza, serikali iachane na mpango wa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam kwa sababu inaonesha dhahiri kwamba katika hili ilikurupuka na haikujipanga na badala yake itumie muda wa kutosha kutafakari madai ya wananchi na kuona namna iliyo bora ya kuvuna gesi ya Mtwara.

 Pili, serikali iache kupuuzia mgogoro huu na badala yake iratibu namna itakavyokutana na wananchi wa Mtwara ili isikilize hoja za wananchi na kuzijibu kwa kutoa maelezo ya kina.

 Tatu, ingawa kuna usemi kuwa mkubwa hakosei lakini serikali haina budi kurudi nyuma na kuona kuwa katika hili la gesi ya Mtwara haijatenda vema. Ikubali udhaifu huo na izingatie maoni ya wananchi kwa sababu wao ndio walinzi namba moja wa rasilimali za taifa.

 Nne, serikali ijue kwamba haina namna nyingine ya kuendelea na mradi huu kinyume na kutumia nguvu za kijeshi kwani wananchi wamedhamiria kufa kwa ajili ya gesi. Kwa hiyo tafsiri rahisi ya hatua yeyote ile ya kuendelea na mradi huu ni kwamba serikali imeamua kumwaga damu za wananchi wa Mtwara. Sasa serikali ipime yenyewe kati ya
manufaa yatakayopatikana kwa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam na roho za wananchi zitakazopotea kwa kupinga mradi huo kipi ni cha heri?.

 Tano, Mkuu wa mkoa Mh.Joseph Simbakalia na Mh.waziri wa nishati na madini Pro Dr Sospeter Muhongo wawaombe radhi wananchi wa Mtwara kwa maneno yao ya kejeli kwa kuwaita wahaini wananchi wa mkoa wa Mtwara wanaopinga gesi kusafirishwa katika bomba hadi Dares-Salaam.
Mwisho kabisa serikali haina budi kubadilika kimawazo na kuona kuwa mikoa ya kusini ina haki ya kuendelezwa kiuchumi. Serikali iachane na kasumba ya KILA KITU Dar es Salaam. Umefika wakati sasa wa kuendeleza mikoa mingine ili mrundikano wa watu Dar es Salaam upungue na usawa wa maendeleo upatikane kati ya mikoa mbalimbali ya nchi yetu. Hii hali ya kupendelea maeneo Fulani tu na kulazimisha kuwa kila jambo liende huku na maeneo mengine ni ya kuendeleza maneo ya wenzao ndio itaifanya nchi hii siku moja IPASUKE vipande vipande wakati kila watu watataka wabaki na mikoa yao.

TAMKO – SHURA YA MAIMAM INAUNGANA NA WANANCHI WA MIKOA YA KUSINI KUITAKA SERIKALI ISITISHE MPANGO WA KUSAFIRISHA GESI ASILIAYA MTWARA KUPELEKWA DARES-SALAAM NA BADALA YAKE MTAMBO WA KUFUA UMEME WA MEGAWATT 300 UJENGWE MTWARA KAMA ULIVYOKUSUDIWA AWALI KABLA YA USHAURI MBAYA WA TPDC KWA SERIKALI. NA KWA KUWA TUNAAMINI KUWA SERIKALI YETU NI SIKIVU ITATUSIKILIZA WANANCHI WA MIKOA HII YA KUSINI kama ilivyowasikiliza wananchi wote wa Tanzania tulipoitaka serikali kuwa na mjadala kuhusu kuandikwa kwa KATIBA MPYA ingawa msimamo wa serikali mwanzo ulisema katiba iliyopo inakidhi haja za wakati huu.
Ee ALLAH shuhudia kuwa tumefikisha na tumetekeleza wajibu wetu
.

No comments:

Post a Comment