Sunday, January 13, 2013

Chadema chamuundia kamati diwani wa Kunduchi


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeunda kamati ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili diwani wa Kunduchi, Janeth Rite, anayedaiwa kuuza viwanja vya wazi pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyopigwa marufuku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Mkoa wa Kinondoni na Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Henry Kilewo, alisema tayari kamati hiyo imeanza kazi ili kujiridhisha dhidi ya tuhuma hizo.
Alisema awali ngazi ya jimbo ilifanyia kazi tuhuma hizo na kujiridhisha kuwa anahusika na kutolewa kwa mapendekezo kuwa avuliwe uanachama.
Kilewo alisema kutokana na suala hilo wasingeweza kuchukua maamuzi ya moja kwa moja kama ngazi ya mkoa na kuamua kuunda kamati ambayo itakuja na majibu kuanzia Februari 15, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo ikibaini tuhuma hizo ni za kweli watawasilisha mapendekezo kwenye kamati kuu ya chama ili hatua zichukuliwe.
Alisema chama chake hakitavumilia dhuluma yoyote ile wala kumlinda mtuhumiwa ambaye atakiuka taratibu za kiuongozi ama zile za kiutendaji.
Kilewo amewataka wananchi kutoa vielelezo vyao vya kutosha katika ngazi ya mkoa ili waweze kuandaa ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma hizo.
Kilewo alisema kamati iliyoundwa ipo chini ya watu watatu ambapo mwenyekiti wake ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Mkoa, Suzan Lyimo, katibu Kilewo na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa, Mzee Erasto Sindila.
Hivi karibuni kumeibuka malalalamiko mengi dhidi ya uuzwaji wa viwanja vya wazi pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyopigwa marufuku katika kata ya kunduchi kwenye jimbo la Kawe.
Maeneo hayo ambayo diwani huyo anadaiwa kuyauza ni kiwanja namba 465 kilichopo mtaa wa Pwani (Tegeta Masaiti) ambalo ni eneo la wazi pamoja na Mabwepande kwenye eneo la umma.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment