MUUNDO WA MUUNGANO WAPASUA VICHWA WANANCHI
KUNA dalili za kila aina kuwa maoni ya wananchi na makundi mbalimbali yanayoendelea kutolewa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu aina ya Muungano unaotakiwa, yanaweza yakaleta mtikisiko mkubwa katika taifa, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Wakati tume ikiendelea kupokea maoni ya makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, kumejitokeza mgawanyiko wa wazi kuhusu aina gani ya Muungano itamkwe kwenye katiba mpya.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kusimamia mtazamo wake wa kutaka muungano uliopo wa serikali mbili uendelee wakati vyama vya upinzani, wanaharakati pamoja na makundi kadha ya kijamii yakitaka muungano wa serikali tatu.
Hata hivyo, pamoja na tofauti hiyo ya maoni, hakuna ufafanuzi unaotolewa na makundi hayo kuelezea faida na hasara za muundo wanaoupendekeza, jambo ambalo wachambuzi wa kisiasa wanadai linaweza kuwapumbaza wananchi na kuwakosesha mwelekeo.
Mathalani wakati CCM ikitaka muungano wa sasa uendelee, CUF wanataka muundo wa serikali tatu.
CUF wanasema kuwa wanapendekeza kuwa na mkataba katika masuala mbalimbali yanayohusu Muungano.
Kwamba kuwe na katiba tatu zinazoongoza Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano.
Wanasema: “Tumependekeza kuwa na serikali tatu ambazo zitasaidia kuondoa migogoro ya masuala ya Muungano kwa sababu kila moja itakuwa inajitegemea.”
CUF wanaamini kuwa katika sera hiyo, itawezesha kuainisha mambo mbalimbali ambayo yataweza kuondoa migongano ya kimaslahi yatakayojitokeza.
Kwa mujibu wa CUF, kuwepo kwa serikali tatu kutatoa nafasi kwa Serikali ya Tanganyika kusimamia mambo yake ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Serikali ya Muungano na Zanzibar kuona wanaonewa.
Kwa upande wao CHADEMA, wanapendekeza kuwa ili kuepusha kuvunjika kwa Muungano, kuwe na Serikali ya Tanganyika na Zanzibar na zote ziwe na rais, Bunge na serikali yake, na kuwe na serikali ndogo ya Muungano itakayoshughulikia mambo saba tu.
Baadhi ya mambo hayo ni ulinzi na usalama, mambo ya nje na upande wa diplomasia. Pia Rais wa Muunagano achaguliwe na mamlaka kama wabunge, mameya na magavana wa majimbo.
Wakati maoni hayo ya muundo wa Muungano yakiwa hivyo bila ufafanuzi wa kina, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk. Benson Bana, anawakosoa kuwa hawatoi sababu za msingi.
“Haya maoni ni mazuri kwa kila upande, lakini tatizo ni kwamba wanayatoa kisiasa, hawatoi sababu za msingi za watu kupima kwenye mizani na kuchagua ni wapi waelekee katika mchakato huo,” alisema.
Dk. Bana aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa, pande hizo zilipaswa kubainisha wazi mazuri na mabaya yaliyomo kwenye muundo wa serikali hizo ili wananchi wapime, waelimike na kuchagua wapi pa kuelekea.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, ili kuwasaidia wananchi kwenye mkanganyiko huo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa kumtafuta mshauri mwelekezi awasaidie kuwafafanulia faida na madhara ya miundo hiyo inayopendekezwa ili mwisho wa siku wachague kwa kutambua wapi wanaelekea.
No comments:
Post a Comment