SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kukituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa si chama cha kizalendo kisichozingatia demokrasia, Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), wilaya ya Kahama, limeibuka na kumtaka avue gamba kisha akishinikize chama chake kuwafichua mafisadi walioficha fedha Uswisi.
Ushauri huo ulitolewa mjini hapa jana na mratibu wa BAVICHA Kahama, Ahmed Nambo, alipozungumza na Tanzania Daima ambapo alieleza kushangazwa na Mgeja kusahau uozo ulio ndani ya chama chake.
Mgeja hivi karibuni alipozungumza na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali na wazee wa wilaya ya Kahama, alisema kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman MBowe, kuhusu gombea urais kupitia CHADEMA inazuia uhuru wa demokrasia katika chama.
Nambo alisema Mgeja anatapatapa juu ya anguko lililo ndani ya CCM kwa Watanzania na kudhamiria kuipotosha kauli ya Mbowe kwa kuijengea hoja yenye propoganda, lengo likiwa ni kuidhoofisha CHADEMA katika mboni ya Watanzania.
“Mgeja asiudanganye umma, kwani alama yake popote pale ni joho la Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga wala si hiyo; taasisi yake hivyo inampasa kuwaeleza Watanzania kwa nini katika miaka 51 ya uhuru taifa bado ni maskini huku likiwa na rasilimali nyingi, tena kukiwa na tofauti kubwa ya kipato baina ya wananchi wa kawaida na viongozi walio madarakani?” alihoji Nambo.
Aidha alimtaka Mgeja na viongozi wenzake wajadili hatima ya chama chao kinachoendelea kukuosa nuru kwa Watanzania badala ya kupoteza muda kwa hoja hiyo.
Hata hivyo, Mgeja akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana kutoka Zanzibar, alisisitiza kauli yake hiyo na kufafanua kuwa hakuiongea kama kiongozi wa kisiasa bali ulikuwa msimamo wa taasisi anayoiongoza ambayo haifungamani na upande wowote wa itikadi za kisiasa au dini.
“Mimi niliongea kama Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Mzalendo Foundation, taasisi inayohusika na demokrasia, utawala bora na haki za binadamu na hawatasita kukosoa katika nyanja hizo pindi wakiona maeneo hayo yanachezewa pasipo upendeleo hata kama CCM itateleza katika nyanja hizo tutasema bila kuogopa,” alisema Mgeja.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment