Sunday, January 27, 2013

Arfi ashangaa wanaojadili urais Chadema

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Said Arfi, amewashangaa baadhi ya viongozi wenzake ndani ya chama hicho wanaojadili suala la urais.

Arfi, ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alisema huu siyo muda mwafaka wa kubishania hoja ya mgombea urais kwa sasa, kwa kuwa muda wa jambo hilo haujafika.

Amesema kwamba, kitendo cha kuendelea kufanya hivyo ni kutafuta migogoro isiyo ya lazima ndani ya chama hicho, badala ya kuanza kujipanga na kujijenga zaidi kwa wananchi.

Arfi alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na MTANZANIA, alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Ltd, zilizopo Sinza, Kijiweni, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, katika maelezo yake, mbunge huyo alisema Katiba ya CHADEMA ipo wazi kuhusu haki za wanachama wanaotaka kugombea nafasi yoyote.

“Katiba yetu ipo wazi, sisi kila mwanachama anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa, ndiyo kusema kuwa kila mwanachama anayo haki ya kugombea nafasi yoyote kwa sababu ni haki yake kama mwanachama.

“Sipo hapa kuzungumzia nani anayefaa, ninachosema ni kwamba, nafasi ya mgombea urais siyo hoja kwa sasa kwa sababu muda wake bado haujafika.

“Muda ukishafika, chama kina utaratibu wake wa namna ya kuwapata wagombea wa nafasi zote hadi hiyo ya urais, sioni haja kwa nini tushughulishwe na jambo hilo sasa,” alisema Arfi.

Wakati huo huo, Arfi alirejea kauli ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi wenzake wa juu, kwamba Chadema itashinda urais wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Alisema kwamba, hali ya kisiasa ndani ya chama chake bado ni shwari na kwamba migogoro iliyopo inayohusisha Baraza la Vijana (BAVICHA), haiwezi kukiyumbisha chama.

“Chadema ni chama makini, tunajua wapi tulipotoka, wapi tunapoenda, baadhi ya watu wanaitabiria kifo Chadema, mimi nasema wanajisumbua, hao wanapoteza muda wao kutabiri vitu wasivyovijua.

“Chadema inazidi kuimarika kila kukicha, tutachukua dola katika uchaguzi wa mwaka 2015, watu hawa wanaoiombea mabaya Chadema hawataamini kitakachotokea,” alisema.

Alipoulizwa chama chake kitawezaje kuchukua dola wakati kimepata mafanikio kidogo kisiasa, ikiwamo kutopata wabunge na madiwani wengi, alisema:

“Wewe unajua Chadema tulikuwa na wabunge watano mwaka 2000, leo tunazungumzia wabunge 50 ndani ya Bunge.

“Lakini suala la idadi ya viti peke yake siyo kigezo, kuchukua dola ni suala la utayari wa Watanzania, tukijipanga vizuri na kwa kutumia utayari huu walionao wananchi, naamini hakuna wa kuzuia tusichukue dola,” alisema.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment