CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Sikonge, kimeendelea kuitesa CCM kufuatia Katibu wa Chama cha UDP wilaya hiyo Kazimoto Elias Kazimoto, kujiunga na chama hicho.
Kazimoto amehamia CHADEMA na wanachama wapatao 241 kutoka vyama vya UDP, CUF na CCM akiwemo mwenyekiti wake, Phillipo Elicado Kayumba.
Baada ya kuhamia chama hicho, Kazimoto sasa ni Mwenyekiti wa Kata ya Misheni na Kayumba ni Katibu Mwenezi wa kata hiyo.
Alisema kuwa, aliamua kujiunga na CHADEMA mapema mwezi Agosti akiwa na idadi hiyo ya wanachama akidai hiyo ndiyo siri ya chama hicho kushinda kiti cha udiwani Kata ya Ipole, Wilaya ya Sikonge.
Kazimoto alisema kuwa, baada ya kujiunga na CHADEMA sasa anajipanga kugombea udiwani Kata ya Misheni ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Robert Kamoga (CCM).
Aliongeza kuwa baada ya kuhama na wanachama hao, pia amejipanga kuhakikisha CHADEMA kinakuwa na nguvu kubwa ili kushinda kiti cha ubunge na udiwani kwa kata nyingine zaidi.
Aidha, alisema kazi nyingine ni kuhakikisha CHADEMA kinakuwa na wanachama walio hai wenye misimamo thabiti ili kukibeba chama.
Alisema siri ya ushindi na kupata idadi ya wanachama wengi kwa sasa ndani ya CHADEMA kutasaidia chama chake kuimaliza CCM kwenye uchaguzi.
“Wananchi walio wengi kwa sasa wako hoi kimaisha, hivyo ushindi wa CHADEMA katika nafasi mbalimbali za uongozi kutasaidia kuondoa kero nyingi zilizopo,” alisema.
Alisema ana imani kubwa mwaka 2015 ambao ni mwaka wa uchaguzi mkuu, CHADEMA Sikonge itakuwa ni moto wa kuotea mbali na wananchi wataiunga mkono.
No comments:
Post a Comment