Sunday, December 2, 2012

‘CHADEMA wajengeeni ujasiri wanachama’


VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wametakiwa kuwajengea uwezo wa ujasiri wanachama wao ili kuondokana na uoga wa kuwaogopa wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ama Jeshi la Polisi.
Wito huo ulitolewa mjini hapa jana na Mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi (CHADEMA) alipozungumza na viongozi wa chama hicho wilayani Chato, Geita.
Profesa Kahigi alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wanachama wa chama hicho kuwa pamoja na viongozi wengi wa CHADEMA, wanatishiwa na baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.
Wanachama hao walisema licha ya kujitahidi kujenga chama, lakini bado o wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa na kuonewa na baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na askari.
“Tunafanya kazi katika mazingira magumu, mtu anayeonekana muelewa wa mambo mbalimbali na kuhoji anabambikiwa kesi na wakati mwingine kutishiwa kupelekwa polisi.
“Pia viongozi wa CCM wamekuwa wakiwatishia wananchi kwa madai kuwa vyama vya upinzani vipo kwa ajili ya kuleta fujo, hivyo kuwafanya wananchi wengi kuogopa kujiunga navyo,” alisema mmoja wa wanachama hao.
Kwa upande wake, Profesa Kahigi aliwataka viongozi kusimama kidete kuhakikisha wanatoa elimu kwa raia na kuwaeleza kuwa vyama vingi havikusajiliwa kwa ajili ya kuleta fujo.
“Ngoja niwaambie ndugu zangu, hao maaskari wanaowatishia wao kama nani? Waambieni kuwa nyinyi mnakaa nao mitaani na kila siku mnakutana nao, Jeshi la Polisi linatakiwa kuhakikisha linalinda usalama na mali ya raia, lakini siyo kufanya kazi ya siasa,” alisema.

No comments:

Post a Comment