POLISI WAMSAIDIA KWA KUPIGA MABOMU, RISASI
HALI bado ni tete kwa safu mpya ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochaguliwa hivi karibuni kwa tambo kuwa watakabiliana na vuguvugu la upinzani linalokikabili chama hicho.
Zikiwa ni wiki chache tangu sekretarieti mpya ya chama hicho na baadhi ya mawaziri wazomewe katika mikoa ya Mtwara na Rukwa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, naye ameonja kadhia hiyo mkoani Mara juzi.
Bulembo alizomewa kwenye mkutano wa hadhara kiasi cha Jeshi la Polisi kulazimika kutumia nguvu kwa kufyatua mabomu ya machozi hewani ili kutuliza munkari wa wananchi mkutanoni hapo.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC), alikumbana na zomea zomea hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo mjini hapa na kudai kuwa madiwani wa Manispaa ya Musoma wanatumia vibaya fedha za halmashauri hiyo.
Alisema serikali ya CCM imepeleka fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya manispaa hiyo na kwamba madiwani wa CHADEMA inayoongoza manispaa hiyo wamehamisha na kuzipeleka kwenye ujenzi wa barabara bila kufuata taratibu.
“Serikali yetu ya CCM imeleta fedha nyingi hapa Musoma kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya manispaa, lakini madiwani wa CHADEMA wamezipeleka fedha hizo kwenye ujenzi wa barabara bila kufuata utaratibu.
“Kwa maana hiyo, uamuzi wa madiwani wa CHADEMA wa kupeleka fedha hizi kwenye ujenzi wa barabara utawatokea puani si siku nyingi, na mtakuja kuona,” alisema Bulembo kisha akazomewa na wananchi.
Wakati zomeazomea hiyo ikiendelea, makundi ya vijana, kina mama na wazee waliokuwepo mkutanoni hapo, walisikika wakiimba…Nyerere, Nyerere, Nyerere jembe huku wakihoji ni kipi bora kati ya mpango wa serikali ya CCM kujenga ofisi au mpango wa CHADEMA kujenga barabara kwa ajili ya wananchi?
Hata hivyo, zomeazomea hiyo ilionekana kumkera Bulembo, ambapo alisema kuwa hata wakizidi kushangilia vitendo hivyo kwa kipindi kifupi kijacho hawatapata maendeleo kwani serikali ya CCM haiwezi kupeleka fedha kwa kulenga mradi fulani halafu madiwani wakahamisha matumizi yaliyokusudiwa.
“Baada ya miaka miwili mtalia na kusaga meno. Hakuna fedha mtakazozipata hapa kwa maendeleo na watu watafikishwa mahakamani. Mfano mzuri huyu Meya wenu Kisurura (Alex), ameletewa milioni 96 za barabara yeye akapeleka milioni 70 na kujenga barabara chini ya kiwango na mitaro hivyo hivyo,” alidai na kuzomewa tena.
Baada ya kuona hali imekuwa tete, Bulembo alijaribu kutaka kubadilisha upepo kwa kumshambulia mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, akisema aheshimu uamuzi wa mahakama.
Bulembo alidai kuwa Lema aliandika kwenye kitabu cha wageni nyumbani kwa Mwalimu Julius Nyerere kuwa ni mbunge wa Arusha Mjini wakati akijua si kweli, lakini kauli hiyo ilizidisha jazba kwa wananchi na kumtaka aondoke.
“Ondoka zako nyie wezi wakubwa, mmetuletea umaskini mkubwa leo mnatuambia nini hata kwa Mwalimu Nyerere hamuoni haya kwenda wakati mmefilisi nchi?
“Hivi leo mnakwenda nyumbani kwa Mwalimu mnajieleza vipi...iko siku Nyerere atakuja kufufuka, na akiwakuta mko katika kaburi lake mtajuta!” alisikika mmoja wao huku akiungwa mkono na wenzake, jambo lililomfanya Bulembo kuchukua kama dakika tatu hivi akisema CCM oyeee.”
Aidha, alitoa onyo kwa wanasiasa kuacha kusimama majukwaani kumshambulia kwa maneno Rais Jakaya Kikwete, akidai kuwa kuanzia sasa uvumilivu umewashinda.
Bulembo katika hali ya kubabaika alijipachika wadhifa wa serikali kwa kuwaagiza wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na jeshi la polisi kuwachukulia hatua wanasiasa watakaotumia majukwaa kumshambulia Rais Kikwete.
Alipokaribisha maswali, aliulizwa kuhusu baadhi ya vigogo wa CCM wanaodaiwa kuficha mamilioni ya fedha nchini Uswisi, ambapo alisema madai hayo ni uzushi wa Zitto Kabwe kwani alishindwa kuwataja wahusika.
Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Mkuu wa wilaya ya Musoma Mjini, Jackson Msome, alikataa kupanda jukwaani baada ya kuitwa na mwenyekiti huyo.
Baada ya mkutano huo kufikia hatua za mwisho majira ya saa 12:30 jioni, polisi walianza kuwakamata vijana waliokuwa wakiimba na kumsifu mbunge wa Musoma mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA).
Baada ya askari polisi hao kuanzisha kamatakamata hiyo, baadhi ya wananchi walianza kuwarushia mawe polisi hao, jambo lililowalazimu kufyatua hovyo mabomu na risasi hewani na hivyo kuondoa utulivu eneo hilo.
No comments:
Post a Comment