Thursday, December 13, 2012

CHADEMA yaibwaga CCM


KIWIA ATETEA UBUNGE WAKE ILEMELA
KWA mara nyingine tena, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimezidi kukitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kesi za kupinga matokeo ya ubunge zilizokatiwa rufaa Mahakama Rufaa.
Hatua hiyo imejitokeza jana baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania, kuitupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na wanachama watatu wa CCM dhidi ya Mbunge wa Ilemela jijini Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA).
Wanachama hao; Yusuph Lupilya, Nuru Nsubuga na Beatus Madege, walikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupitia kwa Jaji Gadi Mjemas, ambayo ilidaiwa haikutenda haki.
Uamuzi huo wa jana unakuja zikiwa ni siku chache tangu mahakama hiyo, iifute rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Ubungo dhidi ya mbunge wa sasa, John Mnyika (CHADEMA).
Jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Januari Mssofe na wenzake Benard Luanda na Salum Masati, walitoa uamuzi huo wakisema rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo ilikuwa na upungufu.
Kwamba haikuambatanishwa na maombi ya rufaa, hati ya madai ya msingi na kiapo, ambapo vitu hivyo ni muhimu kwa sababu ndiyo vinaonyesha wanachokiona ni kipi.
“Mahakama kupitia kifungu cha 96 (1) (c) mpaka (f) cha kanuni za Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa hiyo na wkata rufaa walipe gharama za kuendeshea rufaa hiyo,” alisema Jaji Mssofe.
Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata ambaye anamwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alidai vitu hivyo ambavyo havikuambatanishwa katika kumbukumbu ya rufaa hiyo vinainyima uhuru mahakama kujua nini kilikuwepo kwenye madai.
Alidai kuwa, hata mrufani mwenyewe hajui pa kusimamia kwa sababu hajui nini mkata rufaa anadai katika maombi yake, pia alidai vitu hivyo vinasaidia kujua nini kilichoamuliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Malata alidai rufaa iliyokuwa mbele ya jopo hilo ilikuwa ni batili kisheria na inatakiwa itupiliwe mbali, kutokana na kutokamilika.
“Rufaa hiyo itupiliwe mbali kwa sababu hajafuata taratibu za kisheria na walipe gharama za rufaa hiyo, tulitumia muda mwingi kuwasilisha nyaraka mbalimbali mahakamani,” alidai Malata.
Hata hivyo, Wakili wa Kiwia, Tindu Lissu alidai nyaraka hizo ambazo hazikuambatanishwa katika kumbukumbu za rufaa hiyo, ni muhimu kwa sababu Mahakama ya Rufaa ingeweza kujua kuwa kesi ya msingi ilifunguliwa lini.
Alidai kila shauri la uchaguzi linafunguliwa ndani ya siku 30 baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa na kuhoji kama shauri hilo lilifunguliwa kihalali.
“Mahakama hii inatakiwa kujiridhisha, kama mambo hayo yalifanyika kihalali, kwa hiyo nyaraka ambazo hazikuambatanishwa katika rufaa hiyo zilikuwa ni muhimu,” alidai Lissu.
Pia alidai hati ya madai ambayo haipo mahakamani, kama ingekuwepo mahakama ingejua kama kesi ya msingi ilifunguliwa ndani ya siku 30, kwa hiyo mahakama haina sehemu ya kuegemea kutokana na nyaraka hizo kutokuwepo.
Lissu alidai kuwa, mleta maombi anatakiwa ndani ya siku 14, tangu kupeleka maombi mahakamani ajue gharama ya maombi hayo.
“Rufaa hii ni batili, hamna budi kufutwa kwa gharama, kwa sababu hawakufuata taratibu za kisheria,” alidai Lissu.
Wakili wa wakata rufaa, Luhigo Andrew, alikubali kuwepo kwa upungufu huo na kuiomba mahakama wafanye marekebisho kwa sababu rufaa hiyo ina maslahi kwa jamii.
“Hata kama, hatuwezi kuvunja sheria kwa sababu ina maslahi kwa umma, pia hatuwezi kupitia dirishani badala ya mlangoni, hapa tunataka haki itendeke,” alisema Msoffe.
Hata hivyo, wakili huyo aliiomba mahakama kama rufaa hiyo itatupiliwa mbali, basi wanaomba wapate punguzo la kulipa gharama hizo, kwa sababu wakata rufaa hawana uwezo wa kulipa.
Lakini Lissu alipinga akadai kuwa si kweli kuwa hawana uwezo wa kulipa wakati katika kesi ya msingi walikuwa na mawakili wawili, na hata katika rufaa hii wana mawakili wawili kwa hiyo wana uwezo wa kulipa gharama hiyo.
Awali katika kesi hiyo ya madai namba 12 ya mwaka 2010, wanachama hao walimlalamikia Kiwia, msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Walidai kuwa sababu ya kukata rufaa ni wapiga kura wengi kutopata fursa ya kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ambapo walitishwa na wafuasia wa CHADEMA.
Pia walidai uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki, na sababu ya tatu ni msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria mkuu kutotoa sababu ya wananchi wenye sifa ya kupiga kura Ilemela kushindwa kufanya hivyo.
Machi 9 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupitia kwa Jaji Gadi Mjemas ilitupilia mbali malalamiko hao, ambapo walalamikaji waliamuliwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi dhidi ya Kiwia.
Akizungumza nje ya mahakama hiyo jana, Kiwia ambaye katika uchaguzi huo alimwangusha Antony Diallo ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, alisema kuwa kuondolewa kwa rufaa hiyo kutamsaidia kuwatumikia wananchi kwa muda wa kutosha.
Aliwataka wananchi wa Ilemela waendelee kuwa na imani naye ili malengo yao yatimie.
“Kwa kweli hii kesi imenichukua muda mrefu, ni miaka miwili sasa, kuondolewa kwa rufaa hii itanipa muda wa kutosha kuwatumikia wananchi,” alisema Kiwia.

No comments:

Post a Comment