Tuesday, December 11, 2012

Ntagazwa: Dk. Slaa ni tishio kwa CCM


ASEMA WAMEBAKIA KUBABAIKA NA KUPOTOSHA
MWANASIASA nguli aliyewahi kuitumikia nchi katika nyadhifa mbalimbali wakati wa utawala wa awamu ya kwanza hadi ya tatu, Arcado Ntagazwa, amekishukia Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema kinababaishwa na nyota ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.
Ntagazwa ambaye alijiengua CCM miaka michache iliyopita na kujiunga na CHADEMA, alisema kuwa kutokana na tishio hilo la kasi ya Dk. Slaa, viongozi wa chama tawala na serikali yake wamejikuta wakibabaika na kufanya vitendo vya ajabu wakidhani wanaweza kumzuia.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ntagazwa alieleza kushangazwa na kiwewe wanachokipata viongozi wa serikali na CCM kwa Dk. Slaa ambaye alidai nyota yake inazidi kung’ara kwa wananchi.
“CCM wanamwona Dk. Slaa ni tishio kwao, hivyo katika kubabaisha watu wanadhani watapunguza imani kwake, wameibua mambo ya ajabu na kupoteza muda kama alivyofanya Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kusema hajarudisha kadi ya CCM,” alisema.
Ntagazwa ambaye amewahi kuongoza wizara tofauti na vile vile kitengo cha Usalama wa Taifa, alifafanua kuwa kwa sasa CCM wanashindwa kutambua kwamba mambo yamebadilika na si kama ilivyokuwa zamani.
“Hili jambo la kupotoka na kushindwa kusimamia misingi na kuwatetea wanyonge, ndilo Dk. Slaa pia amekuwa akilikemea kwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA ambao wamegeuka kucheza ngoma ya mafisadi wa CCM,” alisema.
Ntagazwa kwa kujiamini alisema kuwa Katiba za TANU na CCM ziliandikwa vizuri na kuwekwa mambo ya msingi lakini akasikitika na kuhoji ni pepo gani amewaingilia viongozi wa CCM sasa na kushindwa kusimamia mambo hayo.
“Wanachokifanya CCM sasa ni tofauti kabisa; yaani sawa na ardhi na mbingu. Wanafanya mambo ya ajabu kwa wananchi na hadi kufikia kuibua mambo ya ajabu kama alivyofanya kijana wao (Nape),” alisema.
Kama alivyopata kusema Dk. Slaa na wanasheria mbalimbali, Ntagazwa naye alirejea msimamo huohuo akisema kuwa kadi ya chama ni mali ya mtu na haipaswi kurejeshwa popote isipokuwa akitaka mwenywewe.
“Kwanza jinsi ninavyoenzi misingi ya TANU kadi yangu ya CHADEMA nimeiwekea kava la TANU ili kuilinda isichafuke. Lakini misingi hiyo hawa viongozi wa CCM wa sasa hawawezi kuirejesha hata wangebadili uongozi mara ngapi,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanamshukuru Mungu kwani wananchi wanajionea jinsi CCM ilivyoshindwa kurejesha misingi na badala yake imehamia kushirikiana na serikali kufanya vitendo vya hovyo kwa kushirikiana na polisi na vyombo vingine vya dola.
Ntagazwa alihoji akisema kuwa hata kama ingekuwa ni vigezo kuruhusu, haiji hata kidogo kwa Rais wa nchi kumteua shemeji yake kuongoza Jeshi la Polisi.
“Inawezekana kweli huyo aliyeteuliwa kuwa IGP akawa kitaaluma ana sifa lakini haileti maana hata kidogo kwa mahusiano hayo, huko ndiko kukiuka misingi yetu ya TANU ya maadili ya uongozi,” alisisitiza.
Nyerere, Lema wamvaa Mangula
Naye mwandishi wetu Sitta Tumma kutoka Musoma, anaripoti kuwa Mjumbe wa Balaza Kuu CHADEMA,
Godbless Lema, na mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, wamemtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, kujiuzulu nafasi yake hiyo wakidai alichaguliwa na wajumbe walioshinda kwa rushwa.
Makada hao walirusha kombora hilo juzi wakati wakihutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Mukendo mjini Musoma, ikiwa ni mwendelezo wa Harakati za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
Lema ambaye ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, alieleza kushangazwa na kauli ya Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdullrahman Kinana, ya kutaka kuwafuta viongozi wote waliochaguliwa kwa rushwa ndani ya chama hicho, akisema kuwa mkakati huo hawawezi kuutekeleza kwani asilimia 90 ya wajumbe waliomchagua walishinda kwa rushwa katika chaguzi huo.
“Mangula na mwenzake Kinana eti wametoa miezi sita kwa wana CCM wenzake walioshinda kwa rushwa. Huu mkakati hauwezekani kwani asilimia 90 ya wajumbe waliomchagua Mangula wametokana na rushwa. CCM haina jipya kwa sasa ni kelele tu,” alisema.
Naye Nyerere aliishukia serikali ya CCM likiwemo jeshi la polisi kwa kushindwa kudhibiti mauaji ya raia yanayofanywa na makundi ya kihalifu.

No comments:

Post a Comment