WANAFUNZI wa Elimu ya Juu ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaso) katika Tawi la Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), mkoani Mbeya, wamelalamikia viongozi wa chama hicho kwa kutotembelea tawi hilo tangu lilipozinduliwa.
Imeelezwa kuwa tawi hilo lilizinduliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe Mei mwaka jana, akiwa amefuatana na viongozi wengine wa chama hicho.
Wanafunzi hao walitoa malalamiko yao juzi wakati wa mahafali ya pili ya wanachama wa Chaso, Tawi la Teku, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kiwira, jijini Mbeya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akisoma risala ya wanafunzi hao, Joseph Mlundi alisema tangu tawi hilo lilipozinduliwa mwaka jana, hakuna kiongozi hata mmoja katika ngazi ya mkoa na wilaya, aliyewahi kulitembelea na kuzungumza na wanachama.
“Tangu kufunguliwa kwa Tawi la Chaso kwenye chuo chetu hatujawahi kumwona kiongozi yeyote si wa ngazi ya wilaya wala mkoa, aliyewahi kuja kututembelea na kuzungumza na wanachama kwa nia ya kujenga chama,” alisema Mlundi.
Alisema licha ya wanafunzi hao kushiriki katika harakati mbalimbali za nje na ndani ya chuo hicho, inasikitisha kuona hakuna anayeonekana kuwajali hata kwa kuwatembelea.
Mlundi alisema pamoja na mafanikio waliyoyapata, Chaso Tawi la Teku bado linakabiliwa na matatizo kadhaa likiwemo la ukosefu wa fedha za kulipia pango la ofisi.
Alikiomba chama hicho ngazi ya taifa, kutoa ruzuku hadi ngazi ya matawi ili kuwaepusha katika hatari ya kutimuliwa kwenye jengo la ofisi.
Akizungumzia tatizo la kutotembelewa na viongozi hao, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala aliwawarushia vijembe viongozi wa wilaya na mkoani kuwa baadhi yao wanaogopa kuzungumza na wasomi.
Alisema hali hiyo ndiyo inayosababisha wanafunzi hao kutotembelewa na hivyo kudumaza mwamko wa mabadiliko ya kisiasa ndani ya vyuo hivyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment