KATIKA kile kinachoweza kutafsirika kama chenga ya mwili kwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), serikali jana ilitoa kauli bungeni kuhusu mpango wake maalumu wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam, huku mbunge huyo akiwa amewasilisha hoja binafsi kuhusu suala hilo katika mkutano wa Bunge unaoendelea.
Jumatatu wiki hii, Mnyika aliwasilisha maelezo ya ziada kwa Spika Anne Makinda, kuhusu hoja yake hiyo ili iweze kukidhi vigezo na kanuni na hivyo kujadiliwa.
Hatua hiyo ya serikali, ilimlazimisha Mnyika kuomba muongozo kwa kiti cha Spika, akihoji uhalali wa serikali kutoa kauli wakati tayari akiwa amewasilisha hoja binafsi kwa Spika akitaka suala hilo lijadiliwe bungeni.
Pamoja na hilo, Mnyika ambaye hata hivyo alisema hana tatizo na serikali kutoa kauli, lakini alisisitiza kuwa hatua hiyo inazua mjadala mkubwa.
Mnyika aliongeza kuwa, kauli ya serikali inazua mjadala hasa kutokana na kutoeleza mradi wa mabomba ya China ambao unagharimu karibu sh bilioni 240 na haufanyi kazi sawa sawa.
Pia alisema jambo jingine ambalo linazua mjadala ni visima vya maji ambavyo vimejengwa, lakini maji ambayo yanapatikana yana chumvi kupindukia na hayajawafikia wananchi wengi.
Baada ya hoja ya Mnyika, Kiti cha Spika kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Jenister Mhagama, kilisema kauli ya serikali imekuja kwa mujibu wa kanuni na kueleza kuwa na mbunge amepeleka hoja yake kwa mujibu wa kanuni.
“Kama Spika atakuwa ameona hoja yako imemezwa na kauli ya serikali, hiyo ni Description ya Spika…hata hivyo Mnyika uwe na amani,” alisema Mhagama.
Hata hivyo, akizungumza nje ya Bunge, Mnyika alisema kuwa Spika asikubali kuyumbishwa na mkakati wa serikali kuzima hoja yake na kumtaka asimamie Bunge.
Alisema kitendo cha serikali kutoa kauli na endapo itazuia hoja yake, itasababisha kusiwe na maazimio jambo ambalo ni muhimu.
Awali akiwasilisha kauli hiyo ya serikali, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Magembe, katika kauli yake hiyo, alisema serikali inaonyesha kuwa katika mipango yake mingi, tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam litapungua kwa kiasi kikubwa ifikapo mwaka 2015 au kuisha kabisa ifikapo mwaka 2020.
Maghembe alielezea hatua mbalimbali zilizotekelezwa na serikali, ikiwa ni pamoja na kukamilisha visima 16 kati ya 29 vilivyokuwa vimeahidiwa na Rais Jakaya Kikwete.
No comments:
Post a Comment