Wednesday, November 7, 2012

Lissu kumshtaki JK bungeni


MBUNGE wa Singida Mashariki Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, amesema anakusudia kuleta hoja binafsi bungeni kumshitaki Rais Jakaya Kikwete kwa madai kuwa amevunja katiba kwa kuteua majaji wasio na sifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Lissu alisema anakusudia kufanya hivyo katika Bunge la Februari mwakani baada ya rais kuendelea kuteua majaji wasio na sifa.
Alisema anakusudia kuwasilisha hoja ya kumsitaki rais bungeni kwa kutumia kanuni za kudumu za Bunge sehemu ya 11 na Ibara ya 46A na 46B ya katiba ya sasa kifungu cha 121,122,123,124,125 na 126 ya azimio la kumwondoa rais madarakani.
Lissu alisema pamoja na mambo mengine, rais amekuwa kiongozi wa kuvunja katiba ya nchi kwa kiasi kikubwa kwa kitendo chake cha kuendelea kuteua majaji ‘vihiyo’.
Aidha, alisema hata kama Bunge litashindwa kufanya maamuzi ya kumwondoa rais madarakani kutokana na uvunjifu wa katiba kwa uteuzi mbovu wa majaji, ataangalia utaratibu wa kumshitaki katika vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine, Lissu alimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, kusoma ripoti ya Tume ya Ngwilizi iliyokuwa ikimchunguza na kumhoji kwa madai kuwa alitoa kauli ya kuwadhalilisha majaji na kudhalilisha muhimili wa mahakama kwa kile alichosema kuwa, majaji wengi hawafai kwani hawana sifa.
Alisema kutokana na kauli yake ya Julai 13, mwaka huu ambayo aliitoa bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Waziri kivuli wa Katiba na Sheria, Lissu aliwataja majaji walioteuliwa na rais kwamba hawana uwezo na sifa za kuwa majaji jambo ambalo lilimfanya Spika Makinda kuunda kamati ya kumshitaki katika Kamati ya Bunge ya Maadili na kinga bungeni ili atoe maelezo na ushahidi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment