Monday, September 10, 2012

Video mauaji ya Mwangosi yaliza Kamati Kuu Chadema


Wajumbe washindwa kujizuia
'Muuaji' kufikishwa mahakamani
Picha za video ya tukio la kuuawa kwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyeuawa kinyama na polisi Jumapili iliyopita, jana ziliwaliza wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokutana jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine kujadili tukio la kadhia iliyotokea Iringa katika operesheni yao ya Vuguvugu la Mabadiliko nchini (M4C).

Picha hizo zilionyeshwa katika ufunguzi wa kikao hicho zikiwamo za mnato ambazo zilizorekodi matukio ya vurugu zilizosababisha mauaji ya Mwangosi, zilisababisha wajumbe wengi wa CC kuangua kilio na wengine kububujikwa na machozi.

Mwangosi aliuawa kwa kupigwa na bomu na polisi, wakati wakizuia viongozi na wafuasi wa Chadema kufungua tawi la chama hicho, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Jumapili wiki iliyopita.

“Tumeingia katika mgogoro mpya kama taifa, mgogoro, ambao raia hatuliamini Jeshi la Polisi, jeshi lenye dhamana kubwa ya kulinda raia na mali zao. Jeshi, ambalo ndiyo kimbilio kubwa la kila mmoja anayedai haki linakuwa sasa ni jeshi la kuogopwa na kila mtu,” alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kuongeza:

“Na tunaona kwa makusudi kabisa jeshi lenyewe, taasisi nyingine za kiserikali kama Msajili wa Vyama vya Siasa, wanakazana kila njia itumike kufunika ukweli, ambao umefanywa kwa misingi ya kiovu sana na jeshi letu la polisi.”

Alisema taifa limeingia katika mgogoro mpya wa raia kutoliamini Jeshi la Polisi, ambalo amesema badala ya kuwa kimbilio la watu wanaodai haki zao, sasa limekuwa la kuogopwa na kila mtu nchini.

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema mgogoro huo umehamishiwa sasa kuwa wa kati ya Jeshi la Polisi na Chadema.

Alisema mbali ya mgogoro huo kuwa kati ya polisi na raia, pia unakusudia kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote kuzima Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) linalosimamiwa na chama hicho.

Mbowe alisema Chadema wana taarifa za kina na za undani kwamba, baadhi ya viongozi wa serikali, ambao hawajajitokeza hadharani wamekuwa wakifanya kazi ya makusudi ya kuwasukuma polisi kuzuia mikutano ya chama hicho isifanikiwe.

Hata hivyo, alisema maazimio ya nini Chadema watafanya yatatolewa na CC, lakini akasema mkakati wowote wa kukizuia chama hicho kisiendeleze M4C hautafanikiwa.

Alisema Chadema wanaipenda sana Tanzania na kuithamini amani ya nchi na kwamba, wana uwezo wa kutafakari mustakabali wa taifa kuliko uwezo alionao Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.

Hivyo, akamtaka Tendwa asitoe vitisho vya kukifutia usajili chama chochote cha siasa nchini, na kuongeza kuwa kama anataka kufanya hivyo, aanze kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Na tunamwambia Tendwa kauli zake zinahatarisha usalama wa taifa. Chadema siyo chama cha mfukoni. Chadema ni chama kinachoaminiwa na Watanzania kwa mamilioni. Anapofikiri yeye ana mamlaka ya kuifuta Chadema ama chama kingine, acheze na vyama vingine, lakini asicheze na Chadema, Chadema is a way of life (Chadema ni njia ya maisha). Tunaipenda nchi yetu, hatupendi Tendwa atuingize kwenye matatizo,” alisema Mbowe.

Alisema msajili wa vyama vya siasa na sheria mbovu zilizotungwa kudhibiti vyama zisitumike kuvrugua amani ya taifa na kumtaka Tendwa kutolewa madaraka ya kuwa msajili wa vyama kwa kuwa kiranja wa CCM.

Mbowe alisema wanachotaka kukifanya ni kutengeneza ushindani wa kisiasa uliokuwa wa haki kwa faida na mustakabali mwema wa taifa.

Alisema bila kujali wataingizwa kwenye matatizo kiasi gani, operesheni za M4C zitaendelea kama kawaida nchi nzima sambamba na hatua, ambazo baada ya kikao hicho watakuwa wamekubaliana na viongozi wenzake kuchukua ili kuhakikisha amani, haki ya kusema na kusikilizwa zinapatikana.

Aliwapa pole na kuwapongeza wanahabari wote waliokuwa kwenye eneo la tukio wilayani Mufindi wakati matukio yote ya vurugu hizo yanatokea.

Alisema wanahabari hao walionyesha ujasiri uliosaidia kuliokoa taifa, Chadema na dhamira yake nzuri iliyokuwanayo dhidi ya mkakati wa makusudi uliokuwa umepangwa wa kukichafua chama hicho.

Mbowe alisema wanahabari hao walipiga picha katika mazingira ya vita na picha hizo zimeokoa usalama wa taifa.

"Polisi wameua mfululizo kwa muda mrefu, lakini wamekuwa wana-get away with it (bila kuwajibishwa). Wanaunda tume ambazo zinawalinda wao wenyewe huku wakiendelea kuiua Chadema na kuua viongozi wa Chadema. Lakini tunashukuru sana,” alisema Mbowe.



TUZO KWA WANAHABARI

Hata hivyo, alisema wanashukuru sana waandishi wa habari safari hii kwamba, pamoja na kumpoteza mwenzao waliyekuwa naye kwenye msafara, bado waliendelea na ujasiri wa kupiga picha.

“Hakika wale wanahabari wote waliokuwa katika matukio ya kupiga zile picha wanastahili kutafutiwa tuzo kwa sababu watasaidia sana historia ya nchi yetu. Kwa hiyo, sisi kama chama tutafanya kazi maalum ya kuwatambua wale mashujaa waandishi wa habari wote tuliokuwa site wakati ule kwa kazi kubwa waliyoifanya,” alisema Mbowe.

Alisema utawala wa Rais Jakaya Kikwete na chama chake vimeshindwa bila hofu yoyote kupambana na ufisadi, kwani wizi umeendelea katika taifa na umekuwa chanzo cha kutengeneza mustakabali usiyo mwema kwa taifa.

Pia alisema ufisadi umeendelea, pia kumekuwa hakuna mpango wowote wa kudhibiti uchumi wa nchi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwatesa Watanzania na maisha ya wengi wao kuendelea kuwa magumu.

Alisema wakati hali ikiwa hivyo, viongozi wa serikali na CCM wamekuwa wakisahau kuwa mambo hayo ndiyo yanajenga chuki na utayari wa wananchi kuwaondoa katika madaraka, badala yake wanajaribu kutumia Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na vyombo vingine vya dola ili kuwahakikisha wao wana usalama katika utawala wao.

Hata hivyo, alisema watakwenda kupambana kwa kuwashawishi wananchi na kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali propaganda alizosema zinafanywa na polisi, usalama wa taifa na vyombo vya habari vya serikali kwa sababu bila kuiondoa CCM, nchi inakwenda kuingia kwenye machafuko mwaka 2015.

KUSITISHA M4C


Awali, Mbowe alisema baada ya tukio la kuuawa kwa Mwangosi na matukio mengine yaliyotokea baada ya msiba wake, walilazimika kusitisha operesheni M4C mkoani Iringa na kuomba timu ya viongozi na wasaidizi wao kurejea Dar es Salaam kisha wazungumze katika kikao cha CC kujadili mustakabali wa operesheni za chama hicho na kufanya maamuzi laini au magumu kwa faida ya demokrasia ya taifa.

Alisema katika kikao hicho watajadili kwa kina nini yaliyojiri, taarifa za polisi za awali kuhusiana na msiba huo, kauli za Tendwa, za Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, mustakabali wa uhuru wa vyombo vya habari, haki, wajibu na amani ya wanahabari kama kundi muhimu katika jamii, ambalo halistahili kufungamana na siasa ya upande wowote. 

MKONO WA POLE

Aliwapa pole wanahabari kwa msiba mkubwa na wa kudhalilisha uliomkuta Mwangosi  na kuomba mauaji yale yasiwe mwanzo wa kufifisha nguvu za vyombo vya habari, badala yake iwaimarishe wanahabari kwa kuwa wana dhamana kubwa kwa Watanzania na kwamba, maisha yao yako hatarini hasa pale serikali haichukui hatua za makusudi na za haraka.

Alisema Rais Kikwete ana sifa kubwa ya kuwa mshiriki mkubwa wa misiba, mwepesi wa kuhudhuria, kutoa pole na kushiriki kwa njia zote masuala ya misiba.

Hata hivyo, alisema kama chama wanasikitika kwamba, katika msiba huo wa wanahabari uliotokea katika mazingira ya kutatanisha, Rais Kikwete akiwa Amiri Jeshi Mkuu, mkuu wa serikali na nchi, ambaye majeshi yote yanawajibika kwake, anaweza kuona tukio kubwa kama hilo limetokea, limegusa hisia za Watanzania na raia wengi, wanadiplomasia, wanaharakati ndani na nje ya nchi, vyombo vya habari vya kimataifa, lakini hajatoa kauli.

Alisema Rais Kikwete yuko Kampala, nchini Uganda anasuluhisha mgogoro wa Kongo, ni sahihi afanye hivyo, lakini akasema anaposuluhisha migogoro ya nchi nyingine ni vyema akafanya hivyo katika migogoro iliyoko ndani ya jamii ya Watanzania.

Aliitaja migororo hiyo kuwa ni pamoja na ile iliyohusu madai ya madaktari, walimu na wanahabari, ambao ulitokana na kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi katika muda usiojulikana.

Wakati Chadema ikieleza hayo, serikali imetakiwa kuacha kupendelea baadhi ya vyombo vya siasa na dini badala yake irejeshe amani na kukemea mauaji ya raia wasio na hatia ikiwamo cha Mwangosi.

MAPUNDA: AISHUKIA POLISI

Kadhalika, imetakiwa kuacha kukaa kimya kutokana na mauaji hayo ambayo tangu yametokea Rais Jakaya Kikwete hajasema chochote.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Kiroho wa Shirika la Familia Nchi za Afrika Mashariki, Padri Baptiste Mapunda, wakati akiwahutubia waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kongowe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa uwezo wa Mungu wauaji wa raia wasiokuwa na hatia wamebainika sasa Jeshi la Polisi limekuwa likifanya mauaji katika mikutano au maandamano ya Chadema na kukisingizia chama hicho.

“Mungu amewaumbua sasa polisi ndiyo wauaji wakuu wa raia na wanapofanya hivyo wanavipaka matope vyama vya upinzani ikiwemo Chadema … kumbe polisi wanajisahau kuwa majukumu yao ni kulinda usalama wa raia na mali zao badala ya kuwaua Mungu amewaumbua kuwa ndiyo wauaji wakubwa wa raia katika mikutano ya siasa hapa nchini,” alisema.

Alisema Taifa sasa liko Chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) linaugua hivyo linahitaji kuokolewa na viongozi wa dini wote kwa pamoja washirikiano waache woga.

“Viongozi wenzangu wa dini tuache woga tumepakwa mafuta ya ushujaa ili tuokoe maisha ya familia zetu…kama huwezi kupambana kuhusu familia basi ninyi ni waoga au mafisadi mimi siogopi kwa sababu hakuna wa kuning’oa wala kunifuta mafuta niliyopakwa ya ushujaa wakati wa kupata upadri wangu sikuchaguliwa kwa kidole bali nilipakwa mafuta hivyo tukemee familia zinapoingiliwa na mauaji, ” alisema padre Mapunda huku akimtaja mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina moja  Regina kuwa anampenda sana.

Alisisitiza kuwa wanasiasa watumie mbinu za kisiasa na siyo kila kosa ni la kupiga mabomu na risasi kwa kuua wasiokuwa na hatia kama Mwangosi aliyekuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi.

“Kumuua mwandishi wa habari ni doa kubwa sana nimepokea barua pepe nyingi kutoka kwa rafiki zangu duniani wakinihoji imekuwaje na mimi nilikuwa naisifia nchi yangu kuwa kisiwa cha amani…nimehuzunika nikawaambia habari ndiyo hiyo,” alisema.

Alisema amesikia Tendwa akitishia atavifutia usajili baadhi ya vyama vya upinzani aanze na CCM.

'MUUAJI' KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Wakati hayo yakijiri, kuna kila dalili kwamba pamoja na viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa na hata makao makuu kukwepa kuzungumizia kushikiliwa kwa aksari wake mwenye cheo cha PC kwa mauaji ya Mwangosi, huenda akafikishwa mahakamani leo.

PC huyo ambaye bado jina tunalisetiri, ndiye alimfyatulia bomu Mwangosi na kumuua kunyama kwani mwili wake ulitawanyika vipande vipande wakati huo akiwa chini ya mikono ya polisi.

Askari huyo anadaiwa kutumia bomu hilo linalotoa kishido kikubwa kinyume kabisa cha matumizi yake, na inaelezwa kuwa wiki iliyopita alikwenda kwa mlinzi wa amani kutoa maelezo yake.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment