Monday, September 10, 2012

CHADEMA wamshukia JK


 MKANDA WA MAUAJI WAWALIZA WAJUMBE
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemshukia Rais Jakaya Kikwete kikieleza kushangazwa na ukimya wake kuhusu mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, yaliyofanywa na Jeshi la Polisi.
Akifungua kikao cha Kamati Kuu cha dharura jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema chama hicho kimeshitushwa na kusikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa rais ni Amiri Jeshi Mkuu na kwamba moja ya chombo chake cha dola kimehusika katika tukio la kinyama la mauaji ya mwandishi wa habari.
Alisema inafahamika kuwa Rais Kikwete ni mwepesi kushiriki, kuhudhuria na kutoa salamu za rambirambi katika misiba mbalimbali, lakini katika tukio hili la mauaji ya kusikitisha na kutisha, amekuwa kimya kana kwamba hakuna jambo lolote lililotokea ndani ya nchi anayoiongoza.
“Tunasikitika kama chama katika msiba huu wa mwanahabari ambao umetokea katika mazingira ya kutatanisha na yeye akiwa amri jeshi mkuu, mkuu wa serikali, mkuu wa nchi ambaye majeshi yote yanawajibika kwake, ameweza kuona tukio kubwa kama hili lililogusa hisia za Watanzania mbalimbali, wanadiplomasia, wanaharakati ndani na nje ya nchi na vyombo vya habari vya kimataifa CNN, Al Jazira, lakini Rais Kikwete hajathubutu kutoa kauli.
“Rais yupo Kampala anasuluhusisha mgogoro wa Kongo wakati tuna migogoro ndani ya jamii yetu,” alisema.
Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka migogoro mbalimbali hapa nchini ikiwamo ya madaktari na walimu na kwamba sasa imeingia kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Mbowe alisema katika hali hii ya huzuni na hofu kubwa miongoni mwa waandishi wa habari na Watanzania wengi kutokana na kukithiri kwa mauaji ya raia yanayofanywa na polisi, CHADEMA imeshangazwa na kushitushwa na matamshi ya baadhi ya watendaji serikalini ambayo yanajaribu kuficha ukweli wa mauaji na uvunjaji makusudi wa haki za binadamu.
Aliongeza kuwa wakati watu wakiwa katika taharuki kutokana na mauaji hayo, ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya watendaji wa serikali wakiibuka na kutoa kauli zilizojaa uchochezi na kuvunja amani.
Mbowe alitaja moja kwa moja matamshi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, aliyotoa hivi karibuni akitishia kukifuta CHADEMA kwa kile alichosema ni kusababisha mauaji, kuwa ni za hatari na zilizolenga kuonesha kuwa mauaji hayo yanatokana na mgogoro kati ya polisi na chama hicho.

Wamwambia Tendwa ole wako
Mwenyekiti huyo wa taifa na Mbunge wa Hai, alibainisha kuwa wanazo taarifa sahihi zinazoonesha kuwepo kwa mbinu chafu zenye lengo la kukihujumu CHADEMA zinazopangwa na viongozi wa serikali.
Alisema kauli ya Tendwa ya kudai atafuta chama hicho, ni ushahidi tosha wa kuwepo kwa mbinu hizo na kuonya kuwa asijaribu hata sekunde moja kutekeleza mpango huo.
“Kauli za Tendwa zinatishia amani ya nchi na asitishie kukifuta CHADEMA.
“Tendwa acheze na chama chochote kingine, lakini si CHADEMA,” alisema Mbowe.
Walimtaka Tendwa kutambua wajibu wake na kutenda haki ili asiingize nchi katika machafuko.
“Tunataka kutengeneza ushindani wa haki bila kujali tunaingizwa katika matatizo kiasi gani. M4C itaedelea nchi nzima,” alisema.
Wanahabari watiwa moyo
Mbowe aliwataka wanahabari kutokata tamaa kutokana na mauaji hayo, bali tukio hilo liwape ujasiri zaidi katika utendaji wao wa kazi.
“Tukio lile lisiwe mwanzo wa kufifisha juhudi zenu, ila likawaimarishe wanahabari mkijua kwamba mna dhamana kubwa kwa taifa. Na ni sahihi kwamba maisha yetu yapo hatarini hasa pale serikali yetu inapokuwa haichukui hatua za makusudi na za haraka,” alisema.
Pamoja na hilo, aliwapongeza wanahabari waliokuwapo mkoani Iringa wakati wa tukio hilo la mauaji na kuonyesha ushujaa kwa kuendelea kuchukua picha.
“Kwa ujasiri waliouonesha wameiokoa Chadena katika mpango wa kutaka kuchafuliwa…picha hizi ndio zimekuwa salama si kwa CHADEMA tu bali kwa taifa na wanahabari kwa ujumla.
“Tunawashukuru wanahabari pamoja na kumpoteza mwenzao waliendelea kutimiza wajibu wao, wanastahili kupatiwa tuzo nasi kama chama tutawatambua kwa kazi kubwa,” alisema.
Aidha, alisema serikali inasahau kuwa mambo yanayojenga chuki na wananchi kwa serikali yao ni ugumu wa maisha, badala yake wanatumia dola kupambana na wananchi.
Alisema CHADEMA kitaendelea kuwaunganisha Watanzania, kwani bila kuing’oa CCM mwaka 2015 nchi itaingia kwenye machafuko makubwa.
Picha zawaliza wajumbe
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walishindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya kuonyeshwa picha za mnato na video za mauaji ya Mwangosi.
Picha iliyowaliza wajumbe ni ile inayoonekana mabaki ya mwili wa marehemu Mwangosi baada ya kupigwa bomu la machozi tumboni ambalo lilisababisha utumbo kutoka nje.
Kutoa tamko leo
Mbowe alisema baada ya kikao hicho kujalidili suala hilo kwa undani, chama hicho leo kinatarajia kutoa tamko lake.
Alisema katika kikao hicho watajadili kauli za awali za polisi kuhusu tukio hilo, kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Tendwa, Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na mustakali wa uhuru wa vyombo vya habari.
Pia alisema watajadili utendaji kazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambalo alieleza sasa linatumika kama kipeperushi cha serikali.
“CHADEMA hatutegemei TBC kutengeneza habari, kwani baada ya kuondoka Tido Mhando sasa imekuwa kipeperushi cha serikali. tutajadili mahusiano yetu na TBC na kutoa tamko zito kuhusu hatma yetu na TBC.
“Hakuna ugomvi na waandishi na wapigapicha wa TBC, kwani tunajua wao wanatumwa, bali uongozi. Tukio hili limetokea wao wanapindisha ukweli, wangekuwa na nia nzuri na busara wasingechukua habari za upande mmoja,” alisema.
CUF: Kuuawa mwandishi ni aibu kwa taifa
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa tukio la kuuawa kwa mwandishi Mwangosi ni aibu kwa taifa.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Professa Ibrahimu Lipumba, alisema kuwa mauaji hayo yamelichafua taifa zaidi na ni ishara ya serikali kuwafanya wananchi waogope kueleza mambo yanayowaumiza.
“Kuuawa kwa mwandishi wa habari kwa nchi isiyo na vita ni aibu kwa taifa na kuwafanya wananchi wasiweze kupata habari zinazoendelea katika taifa lao,” alisema.
Kumburuza Nape kortini
Mbowe alisema watamburuza mahakamani Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kutokana na kauli yake kuwa CHADEMA kinapewa mabilioni ya fedha na wafadhili nje ya nchi.
Alisema watampeleka Nape mahakamani ili aende kuithibitisha kauli hiyo na ukweli uweze kubainika.
“Ukifumbia macho hoja hii inaweza kuonekana kuwa ni ya kweli, sasa atakwenda kuithibitisha mahakamani, mahakama ikitenda haki ukweli utajulikana. Wanasheria wetu wanalifanyia kazi suala hili,” alisema.
Kwa muda sasa Nape amekaririwa akisema kuwa chama hicho kimekuwa kikipewa mabilioni ya fedha na wafadhili nje ya nchi na kuwahadaa Watanzania kupitia harambee mbalimbali.
CHADEMA kilimpa siku saba Nape kuthibitisha madai hayo, lakini hakufanya hivyo na kusema kuwa ana ushahidi kuhusu kauli yake dhidi ya chama hicho.
Dk. Slaa afafanua SMS
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa inawezekana IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Nchimbi ni mbumbumbu wa sheria kutokana na kudai ujumbe wake mfupi wa maandishi (SMS) ni wa kichochezi.
Alisema kama si mambumbumbu wa sheria, basi hawajui maana ya neno uchochezi na kuhoji kama ujumbe huo ni wa uchochezi kwa nini mpaka sasa hawajamkamata.
“Nilimtumia ujumbe ule IGP, lakini aliupeleka kwa Waziri Nchimbi maana yake anaomba ushauri ambao pia waziri ameshindwa kumpa mpaka mauaji yametokea.
“Nchimbi ameshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo anatakiwa kujiuzulu kwa kushindwa kuufanyia kazi ujumbe wa thadhari,” alisema.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment