Monday, September 10, 2012

Mbowe: Hakuna wa kuzuia M4C


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuuawa kwa mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi katika mkutano wa chama hicho mkoani Iringa ni njama za polisi kuzima mikutano yake ya kujinadi kwa wananchi.
Akifungua Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kwa dharura Dar es Salaam jana  kujadili hali ya siasa nchini, Mbowe alisema hakuna mkakati wowote utakaozima Operesheni ya Chadema ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) nchini.
Mwangosi aliuawa katika vurugu zilizotokea wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chadema waliokuwa katika sherehe za uzinduzi wa tawi la chama hicho, Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi.
Alisema Chadema kimeshangazwa na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya kuhusu kifo cha Mwangosi  wakati ni tukio ambalo limegusa hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi.
“Chadema tumeshangazwa na ukimya wa Rais Jakaya Kikwete ambaye ni kiongozi wa nchi na mwepesi wa kushiriki katika matukio mbalimbali na msiba. Lakini hili la kifo cha mwandishi wa habari lililogusa jamii nzima ndani na nje ya nchi na kuibua hisia kali, hajatoa tamko hadi leo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Viongozi wa Serikali wakikaa kimya, wanasukuma polisi kuzuia mikutano ya Chadema. Sisi tunasema, mkakati wowote wa kuzia Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko la Chadema hautafanikiwa.”
Mbowe alisema kwa sasa taifa linakabiliwa na migogoro mbalimbali ikiwamo ya migomo ya walimu, madaktari na hivyo mauaji haya ya raia yanayotokea katika mikutano ya vyama vya siasa yanawafanya wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi.

Amshukia Tendwa, Dk Nchimbi
Katika ufunguzi huo, Mbowe pia aliwashutumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi  na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuwa ofisi zao zimetumika kupotosha ukweli wa tukio na kudanganya umma wa Watanzania.
Alisema kauli ya Tendwa ya kutishia kukifuta Chadema ililenga kuvuruga hali ya amani na utulivu iliyopo nchini na kumtaka akitaka kufanya hivyo aanze na chama tawala, CCM.
“Chadema si chama cha mfukoni, kina wanachama zaidi ya milioni mbili, kauli ya Tendwa inahatarisha usalama wa taifa, asiwe kibaraka wa CCM kwa kutoa matamko yanayolinda chama tawala... Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) itaendelea,” alisema Mbowe.
Apongeza vyombo vya  habari
Mwenyekiti huyo wa Chadema alipongeza juhudi na ujasiri wa waandishi wa habari waliokuwapo Nyololo, ambako Mwangosi aliuawa, kwa kutoa habari za ukweli alizodai kuwa zimekinusuru chama chake.
Alisema kama siyo habari na picha zilizoonyesha ushahidi wa wazi, propaganda zingepotosha umma juu ya vurugu zilivyotokea na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari.
Katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu na Baraza la Udhamini Chadema, walitoa machozi, baada ya kuonyeshwa picha za mnato na video za matukio ya vurugu zilizosababisha kifo cha mwandishi huyo.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene ndiye aliyekuwa akifanya kazi ya kufafanua hatua kwa hatua matukio ya picha hizo.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment