MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema wakati wa viongozi kuutumikisha umma umekwisha na kuwataka wananchi wazinduke na kudai haki zao za msingi ikiwamo maisha bora waliyoahidiwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Polisi Mburahati, Dar es Salaam, Mnyika alisema maana halisi ya nguvu ya umma ni wananchi kunufaika na rasilimali za nchi na si maandamano ya kudai haki peke yake.
“Leo hii viongozi wa serikali hawajali tabu wanazopata wananchi kwa kuwa wanadhani ninyi mna wajibu wa kuwatumikia licha ya kuwa kodi zetu tunazotoa ndizo zinapaswa kutupatia mahitaji yetu ya msingi,” alisema Mnyika.
Akizungumzia kero za wananchi, alisema Manispaa ya Kinondoni inapaswa kueleza sababu za kushindwa kumaliza kwa kiwango cha lami barabara ya Mburahati - Mabibo hadi NIT kwa kuwa ilishatengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2011/12.
Alisema barabara hiyo ilitengewa zaidi ya sh milioni 500, lakini katika hali ya kushangaza haijakamilika na hakuna jitihada za kuendelezwa.
Aliongeza kuwa kama barabara hiyo ingekamilika ingepunguza foleni wakati huu ambao kuna matengenezo ya barabara ya Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya magari ya mwendo kasi.
Kuhusu eneo la wazi la jirani na kituo cha Polisi Post Mburahati, Mnyika alisema lilitaka kuchukuliwa kiujanja na CCM, hali iliyoleta mzozo na sasa itajengwa shule ya sekondari ya ghorofa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment