BARAZA la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), limesisitiza kuwa halitarudi nyuma katika kutetea na kupigania haki za Watanzania, ikiwemo ile ya kuishi hasa wakati huu ambapo chama kilichoko madarakani kimeanza kuonesha dalili za kushindwa kuongoza nchi.
Baraza hilo pia limesisitiza msimamo wa CHADEMA juu ya mauaji yanayoendelea nchini, huku vyombo vya dola vikituhumiwa kuhusika na kusema vijana wa chama hicho hawako tayari kuona Jeshi la Polisi likitumika kunyanyasa, kutesa na kuua Watanzania kwa nia ya kukilinda Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya Kamati ya Utendaji ya BAVICHA inayofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili, Mwenyekiti wa baraza hilo taifa, John Heche, alisema vijana wa CHADEMAa kama ilivyo kwa wanachama wengine wa chama hicho, wanalo jukumu la kusimamia itikadi, falsafa na malengo ya chama hicho kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Tunakutana hapa na wenzetu wa KAS kutoka Ujerumani ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa muda sasa... na ushirika huu unatokana na namna zilivyo familia za ushirikiano wa vyama vya siasa duniani. Wakati sisi tunashirikiana na KAS, CCM wao wanashirikiana na shirika la Ujerumani liitwalo FES, CUF wao wanashirikiana na FNS.
“Msaada tunapata kutoka KAS ambao kwa kweli hawatoi fedha mkononi, tofauti na propaganda za akina Nape Nnauye… tunashirikiana na KAS kwa namna ile ile ambayo FES wanashirikiana na CCM na FNS wanashirikiana na CUF, msaada tunaopata ndiyo wao pia wanaupata kutoka kwa mashirika wanayoshirikiana nayo kutoka huko Ujerumani,” alisema Heche.
Aliongeza kuwa, vyama vyote duniani vimegawanyika katika familia za ushirikiano kutokana na milengo ya kiitikadi, akisema kuwa zipo familia maarufu tatu, ambazo ni vyama vya Kisoshalisti, Kiliberali na mlengo wa kati, ambapo chama hicho kipo katika familia hiyo ya mlengo wa kati.
Akizungumzia mauaji aliyodai yanafanywa na Jeshi la Polisi kwa nia ya kuilinda CCM, Heche alisema hizo ni dalili za mwisho za utawala wa chama chochote unapoelekea mwisho.
Aliongeza kuwa msimamo wa CHADEMA, ni kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kuchunguza mauaji ya Arusha, Igunga, Singida, Morogoro na Iringa.
“Tunataka (Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel) Nchimbi, IGP Said Mwema, Paul Changoja na RPC Faustine Shilogile wajiuzulu au wafukuzwe kazi kupisha uchunguzi huru. RPC wa Iringa na Kamanda wa FFU Morogoro wakamatwe haraka na kushtakiwa kwa mauaji yaliyofanyika katika maeneo yao chini ya usimamizi wao,” alisema Heche.
Naye Mwakilishi Mkazi wa KAS, Stefan Reith, mbali ya kutoa shukrani kwa kukaribishwa katika ufunguzi huo ambapo viongozi wa BAVICHA kutoka mikoa yote nchini wanakutana, alitumia fursa hiyo kusema kuwa shirika hilo halitoi fedha kwa chama chochote cha siasa, bali kushirikiana navyo katika kujengeana uwezo na kupeana uzoefu.
Reith alitumia nafasi hiyo kutoa rambirambi kwa mauaji yaliyotokea hivi karibuni na kusema vitendo vyovyote vile viovu vyenye nia ya kudhibiti raia wasitimize haki na wajibu wao wa kikatiba, vinapaswa kulaaniwa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment