Tuesday, August 21, 2012

Mbowe, Slaa wala pilau ya Iddi na wananchi Morogoro


Viongozi wa wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, juzi walilazimika kusimamisha ziara za vuvugu la mabadiliko (M4C) katika Operesheni Sangara wilayani Mvomero ili kushiriki na wananchi chakula cha sikukuu ya Eid El Fitri.

Aidha, Mbowe alitumia muda huo kuwaaga viongozi wenzake pamoja na makamanda wanaoshiriki operesheni hiyo mkoani Morogoro huku akieleza kuwa anatarajia kwenda Florida, Marekani wiki hii kwa shughuli za kuimarisha chama.

Mbowe aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Yusuph Mohamed, viongozi na makamanda wa chama hicho walioko Morogoro kwa shughuli za operesheni ya vuguvugu la mabadiliko.

Wote walishiriki chakula hicho katika mtaa wa Konga Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na wananchi baada ya chakula hicho, Mbowe aliwashukuru makamanda wa chama hicho kwa kushiriki vema katika kampeni za M4C mkoani humu na kueleza kuwa shughuli za ukombozi zinahitaji watu wenye moyo na kujituma.

"Nawapongeza sana makamanda kwa kazi mnayoifanya hapa Morogoro napenda kuwaongezea chachu katika harakati za ukombozi wa mkoa wa Morogoro ambao umeangukia mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi,” alisema.

Alisema baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Eid, wabunge wa Chadema wataungana na operesheni hiyo kwa awamu na kwamba kwa sasa wabunge hao wamerejea majimboni kwao kwa muda baada ya Bunge la Bajeti kumalizika.

Alisema baadhi ya wabunge sita wataungana na operesheni ya M4C mkoani Morogoro na wengine wataungana na timu ya operesheni mkoani Iringa ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na Mbunge wa Hai,  alisema chama chake kimejipanga kufanya mkutano mkubwa katika Jimbo la Morogoro na viongozi wote wa chama hicho watashiriki.

Aliwataka wakazi wa mkoa wa Morogoro kutoa ushirikiano kwa timu ya operesheni chini ya mkuu wa operesheni hiyo, Benson Kigaila, ili kuwezesha dhamira ya chama hicho ya kuwawezesha wananchi wa mkoa huu kubadilika na hatimaye kuona umuhimu wa kukichagua chama hicho katika uchaguzi ujao.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment