Tuesday, August 21, 2012

Chadema yaibua mapya kudhuriwa viongozi wake


Chama  cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)  kimedai kukamata nyaraka za siri za uingizwaji wa silaha kutoka nje unaodaiwa kufanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwadhuru, huku  wakieleza kuwa na taarifa zaidi ya vijana 20 wakiwa na sumu,tindikali,sindano wamepangwa pia kuwadhuru viongozi wa chama hicho wanaofanya operesheni sangara inayoendelea nchi nzima.

Akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Morogoro jana, Katibu mkuu wa Chadema Dk. Willbrod Slaa, alidai kuwa silaha hizo zimeingizwa nchini kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa lengo la kuwafanyia vitendo vya kinyama viongozi wa chama hicho.

Alitaja baadhi ya silaha hizo ni bastola ambazo watapewa kundi la vijana linaloandaliwa na CCM ili kuwadhuru viongozi wa Chadema ambao watakaokuwa katika mikutano mbalimbali ya M4C ikiwa ni njia mojawapo ya kukidhoofisha chama hicho.

Alisema Chadema kupitia kitengo chake cha Interejinsia wamebaini kuwa CCM wameingiza silaha bila kulipia ushuru na kwamba nyaraka wanazo pindi zitakapohitajika watazitoa.

Alitolea mfano njama kama hizo ziliwai kufanywa katika uchaguzi wa jimbo la Igunga mkoani Tabora ambapo moja ya kambi hizo za vijana iliwekwa Iramba Magharibi na kwamba vijana waliandaliwa ili kufanya vurugu katika mikutano ya kampeni ya Chadema.

“Hivi sasa Morogoro, tumepata taarifa kuwa kuna kundi la vijana zaidi ya 20 ambao watavalia sare kama za Chadema wakiwa na sumu, tindikali, sindano na visu ili kuwadhuru viongozi na wanachama wa Chadema ili wananchi wajue kuwa waliofanya hivyo ni wafuasi wa Chadema,” alisema Dk. Slaa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment