BUNGE LISIZUIWE KUINGILIA KATI MGOGORO KATI YA WALIMU NA WANAFUNZI DHIDI YA SERIKALI KWA KISINGIZIO CHA KESI KUWA MAHAKAMANI
Tarehe 1 Agosti 2012
niliieleza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia swali langu la msingi bungeni
kwamba serikali hutoa ruzuku (capitation grants) kwa wanafunzi wa Shule za
Msingi na Sekondari za Umma zikiwemo za Jimbo la Ubungo, japo utekelezaji wa
sera husika huwa unasuasua sana kwa kiwango kilichowekwa kutokulingana na
mahitaji halisi ya wanafunzi; viwango vinavyotengwa katika Bajeti ni chini ya
vinavyotajwa kwenye Sera na Fedha hazitolewi zote isipokuwa hutolewa kidogo
kidogo na hazifiki kikamilifu mashuleni; nikahoji ni lini serikali
itarekibisha hali hiyo ili kuboresha elimu nchini.
Ofisi ya Waziri Mkuu
katika majibu yake imekiri kwamba kweli viwango vya ruzuku kwa ajili ya
uendeshaji wa shule za msingi na sekondari havijafikiwa mpaka sasa na hata
fedha zinazotengwa kwa mujibu wa bajeti hazitolewi kwa kiwango kilichopitishwa
na bunge kwa kile alichoeleza kuwa ni makusanyo ya Serikali.
Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini serikali itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma ni kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji wa shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye vyombo vya habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba hali hiyo ni kati ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali itoe kauli bungeni ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.
Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini serikali itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma ni kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji wa shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye vyombo vya habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba hali hiyo ni kati ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali itoe kauli bungeni ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.
Hata hivyo Spika wa
Bunge alimkataza Naibu Waziri asijibu swali kuhusu mgogoro kati ya walimu na
wanafunzi dhidi ya serikali na kutaka kujibiwa kwa swali ya lini ruzuku itaanza
kutolewa kwa kuzingatia viwango vya sera hata hivyo serikali ilitaja kiwango
cha fedha ya ruzuku kwa mwaka wa fedha 2012/2013 bila kueleza iwapo viwango kwa
mujibu wa sera vitafikiwa kwenye ngazi zote ikiwemo katika shule za
msingi.
Kwa mara nyingine tena
Bunge limezuia kupewa taarifa kuhusu masuala hayo kwa kisingizio cha kesi kuwa
mahakamani hatua ambayo inadhihirisha kwa mara nyingine tena umuhimu wa
kusikilizwa kwa rufaa niliyokata tarehe 31 Julai 2012 ili suala la mgomo wa
walimu, madai ya wanafunzi na hatma ya sekta ya elimu lijadiliwe kwa dharura
bungeni.
Nimefanya hivyo kwa
niaba ya walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu katika Jimbo la Ubungo na
Tanzania kwa ujumla ili bunge lipewe fursa ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba
kuisimamia serikali itekeleze madai ya walimu na kuepusha athari za migogoro
inayoendelea katika shule za umma nchini.
Tarehe 30 Julai 2012 kwa
nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo na maamuzi na Mheshimiwa Naibu Spika Job
Ndugai ya kukataa hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 47 ya kuahirishwa kwa
Shughuli za Bunge kujadili jambo la dharura la mgomo wa walimu na yatokanayo na
mgomo huo kwa kutumia kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 ambayo
inamkataza mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa
mahakama.
Nimewasilisha rufaa kwa
mujibu wa kanuni ya 5 (4) kueleza kutoridhika na uamuzi wa Naibu
Spika wa kutumia kanuni ya 64 (1) (c) kudhibiti Bunge kutumia uhuru na mamlaka
yake kwa mujibu wa katiba ya nchi; sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge
na kanuni nyingine za Kanuni za Kudumu za Bunge kwa sababu tatu.
Mosi, Suala la
yatokanayo na mgomo wa walimu hususani hali tete ya sekta ya elimu kwenye shule
za umma haliko mahakamani, kilichopo mahakamani ni mgogoro kati ya Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) na serikali kuhusu madai ya walimu:
Pili, hata masuala
yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni
64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu
utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa
kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Tatu; izingatiwe
pia kuwa masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa
mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo
na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa
mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kwa kuzingatia sababu
nilizozieleza, nimeomba kamati ya kanuni ibatilishe maamuzi yaliyofanyika na
kutoa pia muongozo wa kikanuni; hivyo nimeomba Katibu wa Bunge amtaarifu
Spika kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya
kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na
kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Wako katika
kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
Mbunge wa Jimbo la
Ubungo, CHADEMA
01 Agosti, 2012
No comments:
Post a Comment