Jana tarehe 30 Julai 2012 baada ya Hotuba ya Waziri wa Afya ya Ustawi wa Jamii kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu Wizara husika na Maoni ya Kambi ya Upinzani nilitaka mjadala usiendelee mpaka kwanza wabunge tupewe nakala ya ripoti ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia mgogoro kati ya Serikali na madaktari na kuandaa mapendekezo ya kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Nilifanya hivyo kwa kunukuu Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii ambayo pamoja na kuwa mwezi Februari 2012 bunge lilikataliwa kujadili masuala husika mpaka kwanza kamati hiyo ikapate ukweli wa pande zote mbili na kuwasilisha mapendekezo kwa bunge, taarifa ya Kamati hiyo kuhusu bajeti iliyowasilishwa jana haikueleza chochote nini kamati ilibaini baada ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wala haikueleza ni ushauri gani iliutoa kwa serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro uliokuwepo wala haikuwasilisha bungeni mapendekezo yoyote yaliyotokana na kazi waliyopewa na bunge. Aidha, Nilinukuu pia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo yalieleza bayana kuwa mwezi Juni yalitolewa majibu yasiyokuwa ya kweli bungeni kuwa Taarifa ya Kamati hiyo iliwasilishwa bungeni.
Kufuatia hali hiyo, na kutokana na bajeti hiyo ya afya kuwa finyu huku ikiwa na utegemezi wa fedha kutoka nje kwa ziadi ya asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 wakati ambapo katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango cha fedha ambazo wahisani walileta ni asilimia 36 pamoja na kuahidi kuchangia zaidi ya 90 kwenye fedha za maendeleo; hali ambayo itaendeleza migogoro kwenye sekta ya afya.
Nikataka ili bunge liweze kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro kwenye sekta ya afya nchini; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia madai ya madaktari iwasilishwe na kujadiliwa bungeni, majibu ya Naibu Spika aliyoyatoa ni kwamba taarifa hiyo haiwezi kuwasilishwa kwa bungeni kwa kuwa kuna kesi mahakamani baina serikali na Madaktari. Majibu hayo yamenifanya niwakumbushe taarifa hii ambayo niliitoa tarehe 29 Julai 2012 ili wadau wa afya mshiriki katika kutaka hatua muafaka toka kwa Serikali na Uongozi wa Bunge:
BUNGE LISIZUIWE KUTUMIA HAKI, UHURU NA MADARAKA YAKE KWA MUJIBU WA IBARA ZA 63 NA 100 ZA KATIBA YA NCHI KUISIMAMIA SERIKALI KWA NIABA YA WANANCHI KUHUSU HALI YA SEKTA YA AFYA NCHINI NA MGOGORO KATI YA SERIKALI NA MADAKTARI WAKATI WA MJADALA WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Tarehe 30 na 31 Julai 2012 Bunge litajadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa zaidi ya miezi mitatu bunge limekuwa likizuiwa kutumia haki, uhuru na madaraka yake kwa mujibu wa ibara za 63 na 100 za Katiba ya Nchi kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kuhusu hali ya sekta ya afya nchini na migogoro kati ya Serikali na madaktari.
Hali hii ilianza mwezi Februari 2012 Bunge lilizuiwa kujadili suala hilo kwa kisingizio kwamba mpaka kwanza kamati ya bunge iende kukutana na wadau wote na kuwasilisha taarifa bungeni; ripoti ambayo mpaka sasa haijawasilishwa. Hali hii ikashamiri zaidi mwezi Juni na Julai mwaka 2012 ambapo bunge lilizuiwa kujadili masuala husika kwa kisingizio kwamba kuna kesi mahakamani.
Kwa chanzo cha hali duni kwenye sekta ya afya nchini na migogoro kati ya Serikali na madaktari ni udhaifu katika utekelezaji wa bajeti ya serikali na ufinyu wa kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya sekta husika kwa ajili ya madawa, vifaa tiba na maslahi ya watumishi wa umma kwenye sekta husika; mjadala kuhusu mapatio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013 iwe fursa ya bunge kuingilia kati kutafuta ufumbuzi.
Hivyo, natoa mwito kwa wananchi na wadau wa Sekta ya Afya kutaka ripoti ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia suala hilo kuanzia mwezi Februari 2012 iwasilishwe bungeni iweze kutumika kama rejea wakati wa mjadala husika. Maelezo yaliyotolewa bungeni na Naibu Spika Job Ndugai kuwa taarifa hiyo ilishawasilishwa bungeni hayakuwa ya kweli, kwa kuwa wabunge hatujapewa nakala wala kujadili ripoti husika na kama mbunge nimeomba nakala ya ripoti husika lakini imeendelea kufanywa kuwa siri.
Aidha, uongozi wa Bunge usiendelee kutumia visingizio vya suala kuwa mahakamani badala yake uliwezeshe bunge kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba na kanuni za bunge kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini na kushughulikia chanzo cha mgogoro ulioendelea kati ya serikali na madaktari wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi na hatimaye kuongeza bajeti kwa Wizara ya Afya kwenye mwaka wa fedha 2012/2013.
Ni muhimu uongozi wa bunge ukazingatia kwamba maamuzi ya Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa bunge kudhibiti mijadala kwa kisingizio cha masuala kuwa mahakamani tayari nilishayakatia rufaa toka tarehe 3 Julai 2012 hivyo kinachotakiwa katika hatua ya sasa ni kuitishwa kwa dharura kwa kikao cha kamati ya kanuni kuweza kubatilisha uamuzi huo ili wabunge watumie uhuru wa kikatiba wa ibara ya 100 kuwawakilisha wananchi katika kuisimamia serikali juu ya masuala husika
Niliwasilisha rufaa hiyo kwa katibu ambayo inapaswa kujadiliwa na kamati ya kanuni za bunge baada ya kutopokea majibu ya barua zangu mbili za kumshauri Spika kurekebisha miongozo iliyotolewa awali kuliwezesha bunge kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba na kanuni za bunge kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini, jaribio la mauji ya Dkt. Ulimboka Steven na kushughulikia chanzo cha mgogoro unaoendelea kati ya serikali na madaktari wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27, 28, na 29 Juni 2012, na tarehe 2, 3 na 4 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo, maamuzi, majibu na Mheshimiwa Spika Anne Makinda, Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge Sylvester Mabumba Jenister Mhagama kwamba suala la madai ya madaktari na mgogoro uliotokana na madai hayo ni masuala ambayo hayapaswi kujadiliwa bungeni kwa kuwa kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 inamkataza mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama.
Katika rufaa yangu kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 5 (4) niliwasilisha maelezo ya kutoridhika na maamuzi yaliyofanyika kwa sababu tatu zifuatazo:
SABABU YA KWANZA; Taarifa za Vyombo vya habari zimeeleza kwamba kesi iliyopo mahakamani imefunguliwa dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na si Jumuiya ya Madaktari Nchini pamoja na vyama vingine vya watumishi na wataalamu katika sekta ya afya na masuala mengine ya sekta husika. Aidha, ukiondoa suala la madai ya madaktari ambayo ni kati ya hoja zilizo mahakamani masuala mengine yanayoendelea si sehemu ya madai yaliyopo mahakamani, mathalani hali ya hivi sasa ya kudorora kwa huduma katika hospitali za umma nchini. Hivyo, Spika kukataza masuala husika ni kinyume na kanuni 5 (1) na ni kuingilia masharti ya ibara ya 100 ya katiba ya nchi yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge.
SABABU YA PILI; hata masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kanuni ya 5 (1) inaeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa na ibara ya 84 ya katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazijatoa mwongozo, basi spika atafanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.
Kwa kuwa maneno “jambo lolote linalosubiri uamuzi wa mahakama” hayajapewa tafsiri kwa mujibu wa kanuni, sijaridhika na miongozo ya Spika iliyotafsiri maneno hayo kudhibiti bunge kujadili masuala niliyoyaeleza. Hivyo, nimeiomba kamati ya kanuni itoe tafsiri sahihi kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba na sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kurejea pia maamuzi ya awali ya maspika wa bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.
Katika maelezo ya awali nimeiomba kamati irejee nyaraka toka maktaba ya Bunge la Uingereza ambalo lina utaratibu kama wetu wa kibunge ( “Separation of Powers- Standard Note: SN/PC/06053) ambayo katika ukurasa wa saba imeeleza yafuatayo kuhusu kanuni hiyo ya kukataza majadiliano bungeni kuhusu masuala yaliyo mahakamani ambayo kwa kiingereza huitwa “Sub Judice”:
“The Sub Judice rule is intended to defend the rule of the law and citizens’ right to fair trial. Where an issue is awaiting determination by the courts, that issue should not be discussed in the House in any motion, debate or question in case that should affect decisions of the court.
However, the sub judice rules are not absolute: The chair of proceedings of the House of Commons enjoys the discretion to permit such matters to be discussed. Morever, sub judice does not affect the right of parliament to legislate on any matter.
The 1999 Joint Committee on Parliamentary Privilege explained that sub judice rules are intended to “strike a balance between two sets of principles. On the one hand, the rights of parties in legal proceedings should not be prejudiced by discussion of their case in Parliament, and Parliament should not prevent the courts from exercising their functions. On the other hand, Parliament has a constitutional right to discuss any matter it pleases”
Maelezo hayo yanathibitisha kwamba bunge linaweza kujadili masuala yaliyo mahakamani ilimradi mjadala huo usilenge kuathiri maamuzi ya kesi iliyo mahakamani, na pia Spika anayo mamlaka ya kutoa uhuru wa majadiliano kwa masuala yaliyo mahakamani bila kuingilia uhuru wa mahakama na kwamba kesi kuwa mahakamani hakuwezi kulizuia bunge kutumia haki na madaraka yake ya kikatiba.
SABABU YA TATU; Spika badala ya kudhibiti mjadala huo bungeni kwa kutumia kanuni 64 (1) (c) angetoa muongozo wa kuwezesha kutolewa kwa hoja ya kutengua kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 150 kuruhusu mjadala kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 63 (2) na Ibara ya 100 ya katiba ya nchi.
HIVYO kwa kuzingatia sababu nilizozieleza niliomba kamati ibatilishe maamuzi hayo yaliyofanyika, kutoa pia muongozo wa kikanuni na pia itoe mapendekezo kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge ili kurekebisha udhaifu wa kuingiliwa visivyo kwa uhuru wa majadiliano bungeni na kuathiri haki, kinga na madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali kuhusu maslahi ya watumishi wa afya na hali ya sekta ya afya nchini hata kwa masuala yaliyo mahakamani. Hata kamati ya kanuni isipokutana na kushughulikia rufaa bado Spika wabunge anaweza kurejea ushauri niliotoa kwake kwa maandishi kwa kutumia njia nne za kikanuni zilizo kwenye mamlaka yake na ya bunge kuwezesha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kushughulikia vyanzo vya matatizo husika bila kuingilia maamuzi ya masuala yaliyo mahakamani.
Wenu katika kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
29/7/2012
No comments:
Post a Comment