MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), jana alirejea kwa kishindo bungeni na kupokewa kwa vifijo na wabunge wenzake, baada kupata nafuu kutokana na ajali mbaya ya gari aliyoipata hivi karibuni.
Nderemo hizo na vifijo vilianza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika jana asubuhi na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuriarifu Bunge kuwa mwenzao huyo amerejea.
“Waheshimiwa wabunge natambua kurejea kwa mwenzetu, Joseph Selasini, ambaye alikuwa amelazwa baada ya kupata ajali mbaya iliyomsababishia majeraha makubwa yeye na mkewe na ndugu zake wengine, lakini vile vile katika ajali hiyo alimpoteza mama yake mzazi, mama mkwe wake, shangazi na dada yake, kweli hilo ni pigo kubwa,” alisema Makinda.
Hata hivyo pamoja na Makinda kuonesha masikitiko makubwa kwa tukio hilo baya, wabunge wa pande zote mbili walionekana kumshangilia Selasini kwa nguvu wakipiga makofi kwa kugonga meza zao.
Makinda alimkaribisha mbunge huyo akisema kuwa wamefurahi kumuona kwani hiyo ni neema ya Mungu kufuatia ajali aliyoipata.
Spika alimpatia nafasi ya kutoa neno la shukrani na kisha kumfanya mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya bajeti yaWizara ya Mambo ya Ndani ya Nnchi, iliyokuwa ikiendelea kujadiliwa.
Selasini alitumia nafasi hiyo kuwashukuru watu wote waliomsaidia kwa namna moja au nyingine wakati wote akiwa kitandani na kwenye mazishi ya ndugu zake, akianza na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri, viongozi wa chama chake na vyama vingine, wabunge na Watanzania kwa ujumla.
“Nawashukuru wote kwa ushirikiano wenu, upendo wenu mliouonyesha katika familia yangu wakati nilipopata matatizo na nikiwa hospitalini kwa kweli nimeuona upendo wenu na sina cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayewalipa, asanteni sana,” alisema Selasini.
Akizungumzia hali ya afya yake pamoja na ya mke wake alisema kuwa anawahakikishia wabunge pamoja na Watanzania wote na hasa wananchi wa Rombo kwamba afya zao zimetengamaa kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa pamoja na kutengamaa kwa afya zao lakini kuna kitu kimoja tu ambacho bado kinamsumbua katika mkono wake wa kushoto ambapo bado amefungwa vyuma.
“Afya yangu na ya mke wangu imetengamaa kwa kiasi kikubwa na kama alivyosema mbunge mwenzangu Joshua Nassari kuwa ubunge si kubeba zege, hivyo kama mnavyoniona pamoja na tatizo la mkono ila mdomo wangu unaongea vizuri na ninawambia wananchi wa Rombo wasiwe na wasiwasi kwani naendelea kuwawakilisha vema,” alisema Selasini.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, alisema Jeshi la Polisi bado linakabiliwa na tatizo kubwa la kasma ya kutokuwa na mafuta kwa ajili ya magari, hali ambayo ni ya hatari sana, ikizingatiwa ukubwa wa kazi yao ya kuzunguka na kubeba wahalifu.
Tanzania Daima
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment