Thursday, July 19, 2012

Mnyika, Lissu wasoteshwa Polisi Singida


LICHA ya Jeshi la Polisi mkoani Singida kumuita Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na vurugu zilizotokea katika Kijiji cha Ndago, jeshi hilo limewasotesha kituoni mchana kutwa.
Mnyika aliwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa saa 7:50 mchana akiwa na mwanasheria wake, Tundu Lissu na Dk. Kitila Mkumbwa, ambapo walikwenda moja kwa moja hadi kwa kamanda wa polisi wa mkoa huo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, aliandikiwa barua ya wito wa polisi kutoka kwa RPC Singida yenye Kumb. Na SR/C.5/4/4Vol.32/40, ya Julai 17, 2012, ikimtaka afike ofisini kwake jana kwa mahojiano.
Walipofika ofisini kwa RPC mchana, viongozi hao walielezwa kuwa hawawezi kuanza mahojiano mpaka kikosi maalumu cha wapelelezi kutoka Dar es Salaam kifike ofisini hapo kutoka kijijini Ndago, ambako kilikwenda kuchora michoro ya eneo la tukio la kifo cha mtu anayedaiwa kuuawa.
RPC wa Singida akawaambia wanaweza kwenda kupumzika popote pale, mpaka watakapoitwa tena, majira ya saa 10 ambapo kikosi hicho cha kutoka Dar es Salaam kitakuwa kimeshafika mjini Singida kutoka huko Ndago.
Hata hivyo, Mnyika akiwa kwa RPC alimtaka amweleze ameitwa kama mtuhumiwa au shahidi, swali ambalo kamanda alionekana kulikwepa akidai kuwa mahojiano ya kawaida tu.
Viongozi hao waliweka msimamo kuwa kama ingefika saa 11 jioni bila kikosi hicho kufika na kuwahoji, wangeondoka kurejea mjini Dodoma kuendelea na shughuli za vikao vya Bunge.
Katika hatua nyingine CHADEMA kimeelezea kusikitishwa kwake na jeshi hilo mkoani Singida kushindwa kuwakamata watu 12 waliowafungulia jalada kwenye kituo kidogo cha Ndago wakiwatuhumu kuhusika na vurugu hizo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari na kaimu katibu wa mkoa wa chama hicho, Shabani Limu, ni kwamba licha ya chama kufungua jalada la kesi dhidi ya watuhumiwa hao, lakini mpaka jana hakuna hatua zozote zile zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
“Kutokana na hali hiyo ya vurugu ilitolewa taarifa kwenye Kituo cha Polisi cha Ndago, kwa jalada NDG/RB/190/2012 na katika jalada hilo tuliwataja baadhi ya watu waliokuwa katika kundi lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano wetu mbele ya polisi,” alifafanua Limu.
Limu aliwataja watu hao kuwa ni Frank Yohana, Anthony John, Simeon Makacha, James Ernest, Martin Manase, Athumani Ntimbu, Abel John, Ernest Kadege, Yohana Makala Mpande, Bakili Ayubu, Tito Nitwa na Daniel Sima.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment