BUNGE LAIZUIA, WENYEWE WALIA RAFU
HALI ya mambo ndani ya Bunge jana haikuwa shwari baada ya kuzuka malumbano baina ya viongozi wa serikali, wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Malumbano hayo yalianza wakati msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Vicent Nyerere, alipozuiwa kusoma baadhi ya vipengele vilivyokuwepo kwenye hotuba hiyo kwa madai kuwa inagusa mashauri yaliyoko mahakamani.
Wakati Vicent akiendelea kusoma hotuba yake alisimama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuomba mwongozo wa Spika akitaka baadhi ya maneno kwenye hotuba ya Nyerere yasisomwe.
Lukuvi alitaka vipengele vilivyokuwa vikihusu ‘mauaji yenye sura ya kisiasa ya kisiasa’ visisomwe kwa sababu kesi zake ziko mahakamani hivyo kuzijadili ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Alitaja vipengele vilivyomo kwenye hotuba hiyo na mashauri yake yapo mahakamani kuwa ni pamoja na suala la mauaji, kupigwa, vitisho, kuteswa kwa viongozi wa CHADEMA Igunga, Usa River na kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Steven Ulimboka.
Lukuvi alibainisha kuwa baadhi ya watuhumiwa wa matukio hayo wamefikishwa mahakamani likiwemo lile la kuuawa kwa mwenyekiti wa UVCCM wilayani Iramba mkoani Singida.
Waziri huyo ambaye pia ni Mnadhimu wa Serikali, alisema kwa matukio ambayo yako katika uchunguzi wa polisi ni vema CHADEMA wakapeleka ushahidi huo polisi ili usaidie upelelezi.
Kabla ya Spika kutoa mwongozo wa jambo hilo Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, alisimama na kumtolea shutuma Spika wa Bunge Anne Makinda kuwaminya wapinzani kwa sababu ya uchache wao.
“Juzi wabunge wa CCM walizungumzia masuala haya bila kuzuiwa, jana baadhi ya wabunge waliwashutumu wa CHADEMA kuhusika katika mauaji. Mwanasheria Mkuu naye alitutisha kuwa baadhi ya viongozi waliokuwepo eneo la tukio wataitwa polisi kutoa maelezo.
“Hawa wote hawakuzuiwa lakini sisi tunazuiwa, nakiomba kiti chako Mheshimiwa Spika kitutendee haki hata kama tuko wachache,” alisema.
“Mheshimiwa Spika mimi sijawahi kuona msomaji wa hotuba iwe kwa upande wa serikali wala Kambi Rasmi ya Upinzani anakatishwa na kuzuiwa kusoma kile alichotakiwa kusona,” alidai Lissu.
Lissu alidai kuwa msomaji wa hotuba ya kambi ya upinzani anatakiwa apewe fursa ya kusoma na kile walichokiona ni maoni ya kambi hiyo kama ilivyokuwa kwa msemaji wa serikali.
Baada ya kauli hiyo ya Mwansheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema, alisimama na kudai CHADEMA wanapotaka haki itendeke kwao ni lazima nao watende haki kwa kuzifuata kanuni zinazoendesha Bunge.
Werema alikana baadhi ya wabunge wa CCM kuishutumu CHADEMA kuhusika na mauaji hayo kauli iliyozua kelele kutoka kambi ya upinzani ikionekana kugomea kile kilichokuwa kikisemwa na Werema.
Kelele hizo zilimfanya Werema kudai kuwa tatizo linalomkabili Lissu ni nidhamu ndogo aliyonayo ndiyo maana amekaa kwenye meza iliyovunjika.
Werema alifafanua kuwa juzi jioni alisema wabunge watakaoombwa kwenda kutoa maelezo polisi wafanye hivyo.
“Naunga mkono hoja ya Waziri Lukuvi, kuwa baadhi ya mambo yaliyomo kwenye hotuba ya kambi rasmi ya wapinzani yasisomwe,” alisema.
Baada ya kauli hiyo ya Werema, Spika Makinda alikanusha madai ya Lissu kuwa kiti chake kinawapendelea wabunge wa chama tawala bali kinachofanyika ni kufuatwa kwa kanuni.
Aliongeza kuwa mtu yeyote awe wa serikali au upinzani anaposoma hotuba inayokwenda kinyume na kanuni anaweza kuzuiwa asiendelee nayo.
“Yeyote atakayesema kitu ambacho ni kinyume na utaratibu na kanuni lazima ataingiliwa awe waziri au mbunge wa chama chochote huo ndiyo utaratibu wetu,” alisema Makinda.
Makinda alisema mbunge anaweza kujadili masuala yaliyopo kwenye upelelezi kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuisaidia polisi lakini hatoruhusiwa kujadili yaliyopo mahakamani.
Alitumia pia nafasi hiyo kusisitiza nidhamu kwa kiti chake na kuomba kuelezwa ni mambo yapi katika hotuba ya kambi hiyo yaliyopo mahakamani ili yaachwe kusomwa kwa mujibu wa kanuni ya 64 ya Bunge.
Alisema kumekuwa na lawama nyingi linazotupiwa Bunge kuwa limekuwa linaingilia na kutoa uamuzi katika masuala ambayo yako nje yake hususan yaliyo mahakamani.
Alitahadharisha kuhusu hotuba zinazotolewa na baadhi ya wabunge kuwa zimejaa mambo ya kisiasa na kuwataka waachane na mambo hayo kama hawana ushahidi nayo.
Waziri Lukuvi alisimama na kufafanua mambo hayo kuwa tayari vyombo vya habari vimeandika kuhusu kesi hizo ambapo alisema kuhusu suala la Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Peter Msigwa, kupigwa liko mahakamani.
Aliendelea kusema suala la Dk. Ulimboka nalo liko mahakamani kama inavyoshuhudiwa na hata lile la Iramba Magharibi nalo tayari watuhumiwa wameshafikishwa mahakamani.
“Kuhusu suala la Mwanza nalo lilifikishwa mahakamani na tayari mbunge mmoja aliyetajwa kuhusika naye akamtaja mwingine na aliyetendewa yuko humu na anaendelea vizuri,” alisema Lukuvi.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), alisimama na kuomba mwongozo akifafanua kuwa kikanuni hawapaswi kuzungumzia mienendo ya kesi zilizo mahakamani na si mazingira ya kesi hizo.
Alisema kuwa hotuba waliyoandaa ilikuwa inatoa maelezo ya awali tu kuhusu matukio ya vitisho na mauaji ya kisiasa.
Baada ya ubishani huo Lissu alisimama tena kupinga hoja ya Werema na Lukuvi akitaka hotuba hiyo isomwe kwa sababu upande huo haujaeleza kesi namba ngapi, zipo katika mahakama gani, zinawakabili watu gani.
Kuona mjadala umekuwa mkali Spika wa Bunge aliwataka wabunge waheshimu kiti chake na wamueleze ni mambo yapi yako mahakamani ili wasiyazungumze.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alimuomba Spika aahirishe shughuli za Bunge kwa muda kutokana na vurugu zilizopo.
Hata hivyo Spika alisema vurugu zilizotokea bungeni hapo si kubwa hivyo hatua hizo hazitoweza kuchukuliwa.
Baada ya kauli hiyo Spika Makinda alimpa nafasi, Waziri Lukuvi kueleza kile kilichopo mahakamani ili kisijadiliwe.
Waziri Lukuvi alianza kuyataja na alipolitaja suala la kukamatwa kwa aliyemteka Dk. Ulimboka zilisikika kauli “aliyekamatwa ni kichaa”.
“Hata kama ni kichaa mimi sijui, mahakama ndiyo yenye kuthibitisha jambo hilo, sisi wote tunajenga hapa,” alisema.
Baada ya malumbano hayo Spika Makinda alimtaka Vicent kusoma sehemu za hotuba hiyo isipokuwa vipengele hivyo ambavyo vinazungumzia mauaji yenye sura ya kisiasa.
Spika Makinda alisema suala hilo amelipeleka katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili iamue kama yasomwe au la.
“Kamati ikiamua yasomwe tukirudi jioni nitampa nafasi Vicent ayasome…., tujipe muda jamani,” alisema
CHADEMA wagonga mwamba
Akisoma taarifa ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Spika wa Bunge Anne Makinda alisema kuwa kamati hiyo ilipewa jukumu la kuipitia hotuba hiyo na imejiridhisha masuala matano kati ya sita kwamba kesi zake ziko mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya kudumu ya Bunge 64(1)c inaweka wazi kuwa mhimili wa Bunge haupaswi kuingilia mhimili wa mahakama.
Spika Makinda alisema kamati hiyo ilikaa jana mchana kwa lengo la kuchambua hotuba sehemu yenye kichwa cha habari ‘mauaji yenye sura ya kisiasa’.
Aliongeza kuwa kamati hiyo iliwaalika Werema, Tundu Lissu, Vicent Nyerere na baada ya kuwasikiliza ilibaini kuwepo kwa kesi tano mahakamani.
“Wajumbe wamekubalina kuwa suala la kada wa CHADEMA aliyeuawa Igunga haliko mahakamani bali liko chini ya upelelezi, tukio la kuuawa kwa kada wa CHADEMA USA River washtakiwa wameburuzwa mahakamani (Arusha).
“Kujeruhiwa kwa Highes Kiwia na Machemli liko mahakamani. Watuhumiwa 10 wameburuzwa mahakamani, Msigwa naye suala lake liko mahakamani mshtakiwa mmoja alifikishwa mahakamani; suala la Ulimboka nalo liko mahakamani na mtuhumiwa mmoja yuko mahakamani.
“Hili la Singida nalo liko mahakamani na watuhumiwa sita wameburuzwa kortini. Walikamatwa mahakamani.”
Makinda alisema kutokana na ushahidi huo kamati imeshauri mambo matano yasiruhusiwe kujadiliwa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment