Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Kambi ya upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe, amekuja na mikakati ya kutatua kero ya msongamano wa magari
katika Jiji la Dar es Salaam.
Akichangia mjadala wa hotuba ya
bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Mbowe alishauri Serikali namna ya kupunguza foleni
wakati ikiandaa mipango ya kudumu katika kutatua tatizo hilo.
Alisema tatizo la foleni Dar
linatokana kitovu cha biashara kuwa katikati ya jiji kwamba serikali ingepaswa
kutengeneza miundombinu ya katikati ya mji ili kufanya magari yanayoingia
katika maeneo hayo kutembea na kufika bila kusababisha msongamano mkubwa.Ili
kupunguza wingi wa magari kuingia katikati ya jiji, mbunge huyo wa Hai, alishauri
kuwepo udhibiti wa magari yanayoingia katika maeneo hayo tofauti na ilivyo sasa
ambapo kunakuwa na magari yanaingia kirahisi siku hadi siku na kufanya
msongamano mkubwa.Akilinganisha suala hili na jiji la London aliitaka Wizara ya
Ujenzi kuanzisha ada ya kuruhusu magari kuingia katikati ya jiji.
Mbowe alisema ada hiyo si tu
kwamba itaondoa foleni bali pia jiji litaweza kukusanya mapato ambayo
yatasaidia katika kupanua na kukarabati miundombinu na huduma mbalimbali kwa
wakazi wake.
Mbowe alisema kutokana na
mashimo yaliyoko katika baadhi ya barabara jijini humo, magari mengine
hulazimika kutembea kwa mwendo mdogo hivyo kusababisha magari hayo kujazana na
kusababisha msongamano mkubwa.
Pia alizungumzia kuhusu
maegesho ya magari ambapo alishauri kurekebisha sehemu hasa katikati ya jiji
kwani mara nyingi vyombo hivyo vimekuwa vikiegeshwa katika barabara za watembea
kwa miguu na kufanya kupita katikati ya barabara na kuhatarisha usalama wao.
“Kama watembeao kwa miguu
wakiachwa wapite sehemu yao, magari yakipaki panapostahili tutafanya mtiririko
mzuri wa magari, hivyo tutapunguza msongamano wa magari na tatizo hili la
watembao kwa miguu wakipita barabarani ajali zitazidi kutokea,” alisema.
Mbowe alishauri kuwe na vivukio
vya watembea kwa miguu ambavyo vitakuwa vya juu au chini kwani daraja la
Manzese pekee halitoshi.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter
Serukamba (CCM) alisema fedha imekuwa tatizo katika ujenzi wa barabara hivyo
alishauri Serikali kukopa ili kuweza kujenga barabara na si tu kutegemea bajeti
inayopangwa kwani hivyo hatupaswi kuogopa kukopa katika masuala ya maeneleo.
Pia Serukamba alizungumzia
suala la kuchakaa kwa barabara ambapo alibainisha kuwa tatizo kubwa ni
kuelemewa kwa miundombinu hiyo kwa kuwa magari mengi yanapita na kusababisha
uharibifu mkubwa.
Alisema Serikali inapaswa
kufufua miundombinu ya reli ili barabara zisielemewe kwa magari kupita kwa
wingi kwani mara nyingi magari makubwa hutumia barabara kusafirisha mizigo
mikubwa na mizito na kupita katika barabara zetu.
Kwa upande wake mbunge wa kuteuliwa
na Rais James Mbatia (NCCR-Mageuzi) alisisitiza juu ya kuwepo kwa usafiri wa
majini katika Pwani ya Bahari ya Hindi hasa katika maeneo ya Bagamoyo hadi
katikati ya Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari.
Mbatia alisema suala la msongamano
limekuwa ni janga hivyo lazima wizara za Ulinzi, Mambo ya Ndani, Utawala Bora
zikae pamoja na kuzungumzia suala hilo kwani janga halisubiri kesho bali lazima
tulifanyie kazi leo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment