MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC), Zitto Kabwe ameutaka Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma(PPF), kuwasilisha kwenye kamati yake taarifa ya kuwasaidia watoto na wanafunzi waliofiwa na wazazi wao,waliokuwa wanachama cha mfuko huo ifikapo Septemba mwaka huu ili iweze kupitiwa.
Akizungumza na watendaji wa PPF kwenye maonyesho ya 36 ya Mamlaka ya Biashara ya Kimataifa(TanTrade), yanayomalizika leo Dar es Salaama, Zitto alisema kuwa wanafunzi hao ni muhimu kusaidiwa kwa sababu ni viongozi watarajiwa.
Alisema hadi sasa mfuko huo unawasaidia wanafunzi 1,001 wa sekondari, ambao wazazi wao walikuwa wanachama wa mfuko na kwamba tayari wameshautumia Sh550milioni kama ada ya wanafunzi hao, hivyo basi kama mfuko wana wajibu wa kufuatilia maendeleo yao pamoja na kuwasaidia kupindi watakapofika elimu ya juu au sekondari.
“Kamati yangu ingependa kupata taarifa ya msaada wa wanafunzi ambao wamefiwa na wazazi wao ambao walikuwa wanachama, hii itaweza kuwasaidia wanafunzi kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu hadi vyuo vikuu, lakini kwa vigezo, jambo ambalo linaweza kwuashawishi wazazi wengine kujiunga na mfuko huu,”alisema Zitto.
Aliongeza kuwa changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa wanapanua wigo wa kibiashara ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kisasa Mkoani Mtwara ili waweze kupangisha na wawekezaji ambao wataweza kufika kwenye maeneo hayo ambayo mpaka sasa tayari wachimbaji wa gesi wameweka kambi.
Alisema, kutokana na hali hiyo PPF ina jukumu la kuhakikisha kuwa wanachama wanalipa michango yao ili fedha hizo ziweze kuwekeza kwenye miradi mingine ikiwem ya kilimo cha Korosho ambacho kina tija kwa maendeleo ya serikali na taifa kwa ujumla.
Alisema Mtwara ni mji unaokuwa, hivyo basi ataishauri mifuko ya hifadhi ya jamii kufika mkoani humo kwa ajili ya kufanya uwekezaji nasi kusubiri wageni kuchukua nafasi kama ilivyo kwenye sekta ya nishati na madini, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa malalamiko.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa PPF, William Erio alisema kuwa, tatizo linalojitokeza sasa ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango yao, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),Shirika la ugavi wa Umeme(Tanesco) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(Tanapa).
Alisema kutokana na hali hiyo mfuko huo unashindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo, na kwamba waajiri hao wanapaswa kuwasilisha michango yao kwa wakati.
“Tatizo ni kwamba, baadhi ya taasisi na mashirika ya serikali yanashindwa kuwasilisha michango yao ipasavyo, jambo ambalo linaweza kuturudisha nyuma katika uwekezaji, kutokana na hali hiyo tumewasiliana nao ili kuwakumbusha,”alisema Erio.
Aliongeza, mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, wanafika kwenye maeneo tofauti nchini ili kuwekeza, jambo ambalo linaweza kuongeza idadi ya wanachama.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment