Sunday, July 22, 2012

CCM yapumulia mashine


AJALI YA MV SKAGIT, URAIS 2015 VYAITESA
UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa uliozikumba nchi nyingi duniani, unaelekea kukiathiri Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho sasa kinahaha kujinusuru kung’oka madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Chama tawala hivi sasa kina msuguano mkubwa wa kiuongozi ambapo baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakimshutumu Katibu Mkuu, Willison Mukama, kwa kukwamisha mikakati ya kujiimarisha na kurejesha matumiani yaliyofifia miongoni mwa wanachama wake.
Licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wiki hii kukanusha kutokuwa na msuguano na Mukama, makada wa chama hicho wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa vita ya makundi ya kuwania uongozi na ile ya ufisadi inakitesa chama hicho.
Mnyukano wa kisiasa unaonekana wazi hivi sasa ni baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, dhidi ya kundi linalomuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, anayetajwa kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakati hali ya mambo ikionekana kutokuwa nzuri ndani ya chama hicho, nguvu kubwa sasa imehamishiwa kwenye Bunge kwa lengo la kuwadhibiti wabunge wa CHADEMA ambao wanaelezwa kutishia uhai wa chama hicho.
Makada wa CCM wamedokeza kuwa wamebaini wabunge wa CHADEMA mwaka 2005-2010 walilitumia vizuri Bunge kujenga hoja za msingi ambazo ziliwasaidia kujijenga na hatimaye kupata wabunge 22 wa majimbo kutoka watano.
Waliongeza kuwa kutokana na kubaini jambo hilo, chama hicho kimeamua ‘kuzishughulikia’ hoja zinazotolewa na CHADEMA bila kujali kama zina masilahi kwa taifa au la.
Inadaiwa kuwa viongozi wa Bunge nao wamepewa maelekezo ya kukisaidia chama chao hasa wanapoona kuna hoja zinazoelekea kuwapatia umaarufu wabunge wa CHADEMA.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa pamoja na maelekezo hayo baadhi ya viongozi wa Bunge wameonekana kushindwa kukisaidia chama tawala kwa sababu ya kutozijua ipasavyo kanuni, hivyo kutumia ubavu kukataa jambo linalotolewa na wapinzani, hivyo kuwaongezea umaarufu.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, anatuhumiwa kutoa fursa zaidi kwa wabunge wa CCM kurudia maneno ya dharau na lugha ya kuudhi dhidi ya wapinzani.
Kiongozi huyo pia juzi alionesha ‘ukada’ wake pale alipojifanya kukosea jina la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili, kwa kumuita Rose Kamili Slaa, ilhali akijua mbunge huyo alishatarikiana na Dk. Slaa.
Hata hivyo CCM hivi sasa pia kinakabiliana na wakati mgumu wa kushutumiwa kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wake wanaobainika kufanya uzembe katika shughuli zao za kila siku.
Ajali ya mv Spice Islanders iliyotokea mwaka jana na mv Skagit iliyotokea wiki iliyopita inadaiwa ilichangiwa na uzembe wa wataalamu kwa kushindwa kukagua ubora wake.
Serikali ya CCM pia inalaumiwa kwa kushindwa kuwa na vifaa vya kisasa vya uokoaji licha ya kila mara kukumbwa na matukio ya ajali za baharini na ziwani.
Katika ajali hizo mbili za majini zilizopoteza maisha ya Watanzania zaidi ya 400, serikali ya CCM inalaumiwa kwa kushindwa kusimamia sheria za usafiri wa majini na kuficha taarifa ya uchunguzi wa ajali ya awali.
Mmoja wa wabunge wa CCM ambaye jina lake limehifadhiwa, aliilaumu serikali kwa kuunda tume kuchunguza ajali ya mv Bukoba na Spice Islanders, lakini haikutoa matokeo ya uchunguzi huo.
“Serikali iliunda tume kuchunguza ajali ya awali ya mv Spice Islanders na mv Bukoba lakini ikaficha matokeo ya uchunguzi wake. Leo imetokea ajali nyingine na binafsi naamini kama matokeo ya uchunguzi wa awali yangetolewa, bila shaka ajali ya juzi ingeepukika,” alisema kada huyo.
Kufichwa kwa matokeo ya uchunguzi wa ajali za awali za majini, kumeelezwa kuwa ndiyo sababu ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuzima hoja za wabunge wa kambi ya upinzani walioungana na wabunge wote wa Zanzibar kutaka kujadili ajali ya mv Skagit iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 150.

No comments:

Post a Comment