SERIKALI imehamanika. Vijana wanasema imepaniki! Nawatazama usoni, nasikiliza kauli zao; nachunguza matendo yao.
Ni hamaniko la kisiasa. Linatokana na mkanganyiko unaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinapita katika wakati mgumu kuliko wowote tangu kiasisiwe.
Hamaniko hili la CCM na serikali linawafanya watawala na wapambe wao wawe wakali mithili ya dume la ng’ombe lililojeruhiwa. Wanataka kufa na mtu.
CCM hakijawahi kujeruhiwa kisiasa kwa viwango hivi. Hakina uzoefu wa kuona watu wakichukua fomu kugombea uongozi wa ndani ya chama, halafu wanaingia mitini – hawarudishi fomu. Inatokea sasa!
Hakina uzoefu wa kuona baadhi ya viongozi wanaotumainiwa wakiachia ngazi na kutangaza kutogombea tena nafasi hizo, huku wakijua kuwa wana uwezo wa kushinda. Inatokea vijijini.
Ni wakati mgumu kwao, kwa maana kwamba viongozi wengi wa kuchaguliwa katika nafasi za uwakilishi, wanahesabu siku wamalize “wajivue gamba.” Na wanasema wazi; wanasikika juu ya mipango yao hiyo.
Haijawahi kutokea viongozi wa juu wa CCM kulalama kila mara mikutanoni na kwenye vyombo vya habari, kwamba “hata wakihama wanachama wote, nitabaki peke yangu, na CCM haitakufa.” Imetokea sasa.
Mambo haya yanayotokea kwa CCM sasa, tumekuwa tunasikia yakiwatokea wapinzani. Wamekuwa wakiumana na kuumizana, CCM inapita katikati yao.
Sasa hivi wana CCM wanaumana na kuumizana, wapinzani wanapita katikati. Ni wakati mgumu kwa CCM; na hawawezi kuficha hili.
Ndiyo maana unakuta viongozi wa serikali wanaungana na viongozi wa Bunge kutukana wapinzani, na kutetea matusi hayo. Hasira za viongozi wa Bunge dhidi ya wabunge wa upinzani, hasa wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi, ni ishara ya uchovu wa watawala.
Hoja zimefika kikomo. Sasa wameamua kutumia mabavu. Lakini naona na Mungu hayuko upande wao. Maana wakifunika hili, linazuka lile.
Kwa wanaoona mbali, hasira hizi za serikali zinajenga hasira kubwa zaidi kutoka kwa wananchi. Iwapo wananchi wataamua kuonesha hasira hizo, kwa wakati wao, serikali itabaki kujilaumu kwa kuwapatia wapinzani wake silaha nzito.
Si mimi tu ninayeliona hili. Hata baadhi ya wana CCM makini wanaona. Na baadhi yao wanasema. Majuzi tu, nimekutana na wanachama na viongozi wengi wa CCM ambao wanaamini kwamba chama chao kipo njia panda. Wanaona nyuma. Hawaoni mbele.
Mmoja aliyeniambia kwamba anaona mbele, amesema anaona damu! Ana nafasi nzito katika mfumo wa utawala wa sasa wa nchi. Ameshiriki kuusimika mfumo huu; na amekuwa akiulinda.
Lakini sasa amefika mahali naye amepoteza imani na mfumo ule ule aliouzaa. Anasema, kwa jinsi anavyoona mambo, zamu ya CCM kushinda uchaguzi na kutawala nchi hii kwa ridhaa ya wananchi imepita.
Anaona kama wapinzani wanakaribia kuiondoa CCM madarakani. Hata hivyo, anadhani kwamba CCM hawako tayari kuwapisha watawala wapya.
Anasisitiza: “Naona kama hatutaweza kushinda uchaguzi. Nguvu ya CHADEMA inazidi kuongezeka; wanaweza kushinda. Lakini sioni kama sisi tupo tayari kuondoka na kuwaachia nchi. Na kama hili litatokea, CHADEMA nao hawatakubali; damu itamwagika...”
Ana wasiwasi wa ziada. Hajui kama CHADEMA wamejiandaa vya kutosha kuziba ombwe la uongozi linaloonekana sasa. Anakiri kwamba hawajui vema viongozi na wataalamu wa mikakati katika CHADEMA.
Anajua chama kinakubalika kwa wananchi; hivyo kinaweza kushinda kwa kura. Hofu yake ni kwamba iwapo CHADEMA hawatakuwa wamejiweka tayari mapema kuongoza nchi, CCM inaweza kushindwa ikakubali kuachia madaraka, lakini wao wakaingia kwenye giza nene.
Silazimiki kukubaliana na kila hoja yake. Lakini dalili zote zinaonesha kwamba watawala wameshajua kwamba mambo si mazuri kwao, na sasa wanagombana na ukweli kwamba inawezekana wakaweka mgombea urais ambaye ndiye atakuwa wa kwanza kushindwa.
Wanagombana na hisia kwamba huenda Rais Jakaya Kikwete akakabidhi nchi kwa kiongozi asiye wa CCM. Wanaumizwa na ukweli kwamba hadi sasa hawajakubaliana kimkakati ni nani ateuliwe na chama chao kupeperusha bendera ya CCM 2015.
Wanasukumwa na tetesi zilizozagaa kwamba Rais Kikwete anaona ni heri aikabidhi nchi kwa wapinzani kuliko kwa wagombea wa CCM asiowaamini wala kuwakubali. Kama atafanikiwa au la, ni suala jingine.
Na hisia zao zinachochewa na hali ya mgawanyiko mkubwa wa makundi ndani ya CCM, unaozidi kupanuka kadiri wanavyopiga hatua katika uchaguzi wa ndani.
Kinachowachoma zaidi ni habari kwamba wanachama wengi wa CCM, wakiwamo viongozi wao, wanajipanga kuhamia upinzani.
Nimeshuhudia katika baadhi ya maeneo, wanaondolewa mabalozi wa nyumba 10 wa CCM, wanasimikwa wa CHADEMA. Nimeshuhudia katika baadhi ya vitongoji, uongozi mzima unahamia CHADEMA.
Nimezungumza na baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanasema walishaacha siku nyingi kuzungumzia “imani, ilani na maadili ya CCM.” Wanachofanya ni kuzungumzia matatizo ya wananchi, si kusifia au kujibanza kwa CCM na serikali.
Wanaona aibu, maana wanajua kwamba wananchi wana uelewa mpana wa mambo hayo kwa kutazama matendo ya viongozi wa CCM katika maeneo yao.
Wana CCM wa vijijini wanatambua kwamba kwa sehemu kubwa, sifa mbaya ya chama chao haitokani na wao, bali viongozi wa CCM wanaoitwa vigogo; ambao wamepewa dhamana ya uongozi wakaitumia vibaya kujinufaisha na kuumiza wananchi.
Na katika mazingira ya Katiba mpya inayoandaliwa, kama kweli itakuwa kama wananchi wanavyotaka, hakuna dalili za CCM kubaki madarakani.
Ndiyo maana baadhi ya wana CCM wanaojua maana ya madai ya Katiba mpya wamekuwa wakigoma kuunga mkono mchakato huu, kwa kuhofia kwamba ukifanikiwa ndiyo utakuwa mwisho wa utawala CCM.
Na kwa kuliona hili, CCM ambao kwa miaka zaidi ya 15 wamekuwa wakipinga hoja ya wapinzani kuhoji matokeo ya kura za urais mahakamani, sasa nao wameibuka na pendekezo hilo.
Walianza wakikataa Katiba mpya. Baadaye wakalazimishwa na rais, wakakubali kwa shingo upande. Sasa wametafakari na kukubaliana kwamba Katiba mpya iseme wazi kwamba mgombea urais atakayeshinda apingwe mahakamani.
Mtu mmoja akaniuliza: “Ina maana wamegundua kwamba hawatashinda urais?”
Ansbert Ngurumo
No comments:
Post a Comment