Sunday, July 22, 2012

Chadema, CUF watimka


Wasusia uchaguzi Naibu Meya Kinondoni
Wanusa ufisadi, wahoji matumizi ya bil.80/-
Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF), jana walisusa kupiga kura ya kumchagua Naibu Meya wa Halmashauri ya Kinondoni na kutoka nje ya kikao hicho kwa madai kuwa mkutano huo umekiuka taratibu.
Aidha, madiwani wametangaza kuwa hawamtambui na hawatashiriki katika kamati zozote zilizopangwa na halmashauri hiyo.
Madiwani hao awali walitaka kikao hicho kijadili bajeti ya matumizi na mapato ya mwaka uliopita ya Sh bilioni 80 ambazo zilitengwa kwa ajili ya Halmashauri hiyo jambo ambalo halikufanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka katika kikao hicho, Mwenyekiti wa madiwani wa upinzani, Bonifance Jacob, alisema kuwa wameamua kutoka katika kikao hicho kwa kuwa kina dalili za kuwepo kwa ufisadi jambo ambalo hawakuwa tayari kulikubali.
Alisema wao wenyewe walishajua kuwa hawatashinda kutokana na idadi yao kuwa ndogo na kwamba walichokuwa wanataka ni kufuatwa kwa taratibu zilizopangwa kwa mujibu wa kanuni ambapo kikao cha nne cha mwisho wa mwaka kilikuwa ni kujadili matumizi na mapato ya fedha kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliomalizika.
Jacob alisema jambo la kwanza ambalo liliwashangaza ni kusainishwa posho kabla ya kuingia ndani na kuhudhuria mkutano huo.
Hata hivyo, alisema kikao hicho kiliitishwa kama kikao maalumu na ajenda ya kutaka kumchagua Naibu Meya badala ya kujadili taarifa ya matumizi na mapato ya mwaka uliopita kama kanuni inavyosema.
Alisema uchaguzi wa Naibu Meya ungeweza kufanyika kipindi kijacho kwa kuwa jambo hilo halikuwa na umuhimu sana kama la kujadili taarifa ya matumizi na mapato.
Alisema kikao cha jana kimefanikiwa kumpata Naibu Meya, Songolo Mnyonge na wenyeviti wa kamati jambo ambalo linawapa utata kwani watashindwa kuwauliza suala lolote kuhusiana na matumizi ya mapato ya mwaka uliopita kwa kuwa waliokuwepo katika kamati hizo kupangiwa eneo mengine.
Alisema kikao kama hicho hakiwezi kujadili agenda moja kwani hayo ni matumizi mabaya ya fedha na kwamba walimuomba Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Meya wa Kinondoni, Yusuf Mwenda, kukiahirisha kikao hicho mpaka hapo watakapopatiwa taarifa hiyo.
Alisema hawamtambui Naibu Meya huyo kwa kuwa kikao kilichoitishwa hakijafuata kanuni na pia wametangaza mgogoro na baraza hilo kwa kutoshiriki kamati walizopangiwa mpaka hapo watakapopatiwa taarifa ya matumizi na mapato ya mwaka uliopita kabla ya kuteuliwa kwa Naibu huyo.
Kwa upande wake Mwenda alisema kuwa hajaona sababu iliyowafanya wapinzani hao kutoka nje kwani kikao hicho kilifuata kanuni zote ikiwemo uchaguzi wa Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, uundaji wa kamati za kudumu za Halmashauri pamoja na kupitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri na kamati za kudumu za Halmashauri.
Alisema madiwani hao waliotoka katika kikao hicho wanajitafutia umaarufu na kwamba kila mmoja anajua kinachoendelea dhidi ya taarifa kwani wamekuwa wakiwapeleka katika miradi ili waweze kujua kinachoendelea.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment