Wednesday, September 4, 2013

Serikali yahofia ‘nguvu ya umma’

YAJIAPIZA KUTUMIA MABAVU DHIDI YA CHADEMA
SERIKALI jana ililazimika kutishia kutumia nguvu dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai kuwa kinatumia nguvu ya umma kuleta vurugu nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Hawa Ghasia baada ya wabunge watatu wa CHADEMA kuishambulia serikali wakiituhumu kuwakingia kifua viongozi wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kuiba na kujumu mali ya wananchi.
Wabunge hao; Mbunge wa Karatu, Israel Natse (CHADEMA), Mbunge wa Ngorongoro Kaika Telele (CCM) na Mbozi Mashariki, David Silinde, (CHADEMA), kwa pamoja waliishambulia serikali kwa tuhuma za kuwalinda watumishi wa vyama vya ushirika waliobainika kuiba na kufuja mali za wananchi.
Aliyeanza kuisakama serikali ni Natse ambaye katika kauli iliyoonekana kuwakera baadhi ya mawaziri, aliitaka serikali isiwalaumu wananchi watakapoamua kutumia ‘nguvu ya umma’ kuwaondoa wenyeviti wa vijiji na viongozi wengine wanaoiba rasilimali za wananchi.
Mbunge huyo alisema wananchi wamechoka kuongozwa na wezi wa mali ya umma wanaoonekana kulindwa na serikali, kama ilivyotokea katika Kijiji wa Chemchem mwaka 2011 walipoamua kuiondoa halmashauri ya kijiji  chao wakarudishwa kwa amri ya wakubwa.
“Hivi sasa wananchi wamechoshwa kulazimishwa kuongozwa na watu wasiowataka, hivyo wameamua kutumia nguvu ya umma, na serikali inaonekana kuwalinda wabadhirifu, je, wananchi wakiamua kutumia nguvu za umma serikali itawalaumu?” alihoji.
Mbunge wa Ngorongoro, Telele, alimshambulia moja kwa moja Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, akimtuhumu kumrejesha madarakani mwenyekiti wa kijiji aliyeondolewa na wananchi baada ya kubainika ni mwizi wa rasilimali zao.
“Hivi kwanini serikali inawalinda wezi? Mkuu wa  Wilaya ya Karatu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha wanajua wizi uliofanyika katika jimbo langu lakini wanawalinda wezi, hivi mnataka tufanye nini?” alihoji.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, David Silinde, alipigilia msumari wa moto baada ya kuhoji kama ni sera ya serikali ya CCM kulinda wizi unaofanywa na wenyeviti wa vijiji na watendaji wengine waliopewa dhamana ya kuongoza ofisi za umma.
Ghasia akionekana dhahiri kukerwa na kauli hizo, aliishambulia CHADEMA akidai haipendi kufuata sheria na taratibu zinazoongoza nchi na imekuwa ikitumia ‘nguvu ya umma’ kushinikiza mambo mbalimbali, hivyo serikali itaelekeza nguvu zake katika ‘kuwaelekeza’ (CHADEMA) namna ya kufuata taratibu na sheria za nchi.
“Sote tunajua CHADEMA inatumia kisingizio cha nguvu ya umma kukiuka sheria na taratibu za nchi, nyie endeleeni na utaratibu wenu, maana hata humu bungeni kuna mwenyekiti lakini hamfuati kinachotakiwa, sasa huko nje si ndiyo itakuwa zaidi, serikali tutawaelekeza cha kufanya,” alisema Waziri Ghasia, bila kueleza ni aina gani ya ‘uelekezaji’ utakaotumika dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Ghasia alisema wananchi wengi wamekuwa hawafuati taratibu na sheria katika kuwaondoa wanaotuhumiwa, ndiyo maana viongozi wa wilaya na mikoa wanashindwa kubariki kuondolewa kwao.
Alisema serikali haina kipingamizi chochote iwapo wananchi watafuata taratibu zinazotakiwa katika kuwaondoa madarakani viongozi wao.
Alisema ili kuuondoa uongozi wa kijiji ni lazima ufanyike mkutano mkuu wa kijiji ambao mwenyekiti wake ni mkuu wa wilaya hivyo kama utafanyika bila ya mkuu wa wilaya uamuzi utakaofikiwa ni batili.
Alisema wakazi wa Chemchem hawakufuata taratibu zinazostahili ndiyo maana uamuzi uliofikiwa na wananchi haukukubaliwa na serikali.
Hata hivyo, Waziri Ghasia, alisema mwizi yeyote lazima apate fursa ya kujitetea ndiyo ahukumiwe, hivyo ni vema wananchi wakafuata taratibu na sheria za nchi katika masuala mbalimbali.
Hatua ya CHADEMA inatokana na kukithiri kwa matukio ya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, hususan katika vyama vya ushirika karibu kote nchini, huku serikali kila mara ikiingilia kati hatua za wananchi kuwaondoa viongozi wa vyama hivyo madarakani.

No comments:

Post a Comment