Na George Maziku
WAKATI akitoa salamu zake za mwaka mpya kwa taifa Desemba 31, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alituhakikishia kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi unaoendelea sasa utakamilika kwa wakati uliopangwa, na kwamba Katiba hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 26, 2014 wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
WAKATI akitoa salamu zake za mwaka mpya kwa taifa Desemba 31, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alituhakikishia kuwa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi unaoendelea sasa utakamilika kwa wakati uliopangwa, na kwamba Katiba hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 26, 2014 wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ili kuhakikisha dhamira hiyo inafanikiwa, Rais Kikwete alituambia kuwa mapema mwaka huu, ataanza vikao vya mashauriano na vyama vya siasa na makundi na taasisi mbalimbali za kiraia kuhusu muundo mzuri wa Bunge la Katiba, ili hatimaye kuifanyia marekebisho sheria ya marejeo ya Katiba kuhusu kipengele hicho.
Bila shaka hii ni dhamira njema ya rais kwa nchi yake na wananchi kwa ujumla, ni kielelezo cha utashi wa kisiasa alionao kiongozi wetu katika kuhakikisha taifa letu linapata Katiba mpya ikiwa ni hoja ya Watanzania walio wengi.
Bila shaka Rais Kikwete asingependa kuona nchi yetu ikitumbukia kwenye machafuko na umwagaji damu kwa sababu za kudai Katiba mpya, na anataka astaafu vizuri na kuacha alama ya kukumbukwa kwake binafsi na uongozi wake kwa ujumla.
Mimi naungana na Watanzania wengine wanaotaka muundo wa Bunge la Katiba urekebishwe kwani kwa namna ulivyo sasa ni mbovu sana, unawapa nafasi kubwa mno wanasiasa kuunda Bunge la Katiba, maana zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa Bunge hilo watakuwa wanasiasa, na baya zaidi ni kwamba wanasiasa wengi watatoka chama kimoja tu cha siasa, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa maneno mengine muundo wa sasa unaipatia CCM fursa ya kuhodhi Bunge la Katiba na mchakato wote kwa ujumla. Unaipatia CCM fursa ya kutunga Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa sheria ya Marejeo ya Katiba ya mwaka 2011, wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na watu wengine 116 ambao watatokana na vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kidini, wanataaluma, na makundi ya watu wenye mahitaji maalumu.
Sasa ukiangalia sheria hii utaona wazi kabisa kuwa wajumbe wengi wa Bunge la Katiba watakuwa ni wanasiasa kwa sababu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 354, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni 74, na katika wajumbe wengine 116 waliotajwa na sheria, baadhi yao watakuwa wawakilishi wa vyama vya siasa, na hapa tukisie kuwa vyama vya siasa kwa ujumla wake vitapata wajumbe 50 kutoka miongoni mwa hawa wajumbe 116, kwa hiyo hapa jumla kuu ya wanasiasa itakuwa 478 kati ya wajumbe 544 wa Bunge la Katiba wanaohitajika kisheria.
Na katika hawa wajumbe 478 wanasiasa, wajumbe zaidi ya 300 watakuwa ni viongozi na wanachama wa CCM.
Ndiyo maana nikasema kuwa kwa namna sheria ilivyo sasa ni kwamba CCM ina fursa ya kulidhibiti Bunge la Katiba, sheria hii isiporekebishwa maana yake ni kwamba tutakuwa tumewapa kibali Wana CCM kututungia Katiba mpya. Hali hii haikubaliki, ni lazima sheria hii irekebishwe haraka.
Mimi ninapendekeza kuwa Bunge la Katiba liundwe na wananchi, kwa maana kuwa idadi ya Watanzania wasiokuwa wanasiasa iwe kubwa zaidi kuliko wanasiasa, na Bunge hilo linafaa kupanuliwa kwa kuongezwa idadi ya wajumbe wake ili kuleta uwakilishi wa kutosha na wenye manufaa kwa makundi mbalimbali ya kijamii, hivyo kuwezesha kupata Katiba bora na yenye kukubaliwa na wananchi walio wengi.
Kwa hiyo, napendekeza kuwa idadi ya wabunge wa Bunge la Katiba iwe 3,000 na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wasiwe wajumbe wa Bunge la Katiba moja kwa moja ila wanaweza kuwa wajumbe wa Bunge hilo kupitia kwenye vyama vyao. Mgawanyo wa wajumbe hawa kwa makundi mbalimbali ya kijamii napendekeza uwe hivi:
Asilimia 50 ya wajumbe wa Bunge la Katiba watokane na asasi za kiraia (yaani vyama vya wakulima, wafugaji, vyama vya wafanyakazi, vyama vya walemavu, vyama vya wanawake, vyama vya vijana) sawa na watu 1,500.
Vyama vya siasa kwa ujumla wake (vyama vyenye usajili wa kudumu tu) vipatiwe asilimia 30, ambayo ni sawa na wajumbe 900, dini na madhehebu yake ziwakilishwe na wajumbe asilimia 10, ambayo ni sawa na wajumbe 300, na NGOs (watetezi wa haki za binadamu, watetezi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, n.k) wapatiwe asilimia 10, sawa na wajumbe 300.
Ninapendekeza asasi za kiraia kuhodhi Bunge la Katiba kwa kuwakilishwa na nusu ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba kwa sababu zinawakilisha masilahi ya Watanzania walio wengi kuliko makundi mengine.
Na hapa ningependa kutofautisha kati ya asasi za kiraia na NGOs (yaani Civil Societies na NGOs), asasi za kiraia si NGOs, ni miungano ya watu wenye masilahi ya pamoja, wakati NGOs zinazoundwa na wanaharakati wanaotetea mambo mbalimbali.
Asasi za kiraia zina wanachama wengi, wakati NGOs zinaundwa na watu wachache tu wanaoanzia 10 na kuendelea.
Sheria inapaswa kutoa uhuru kwa kila kundi kuwachagua wawakilishi wake bila kuingiliwa na mtu au mamlaka yoyote, ili mradi tu iwekwe ratiba ya kukamilisha uchaguzi wa wajumbe.
Hata hivyo, ili kuhakikisha hapatokei migongano baina ya makundi wakati wa kuchagua wawakilishi wao, ni vema sheria ikaweka utaratibu maalumu wa mgawanyo wa wajumbe hususan katika makundi ya vyama vya siasa na vyama vya kidini.
Baada ya makundi yote kuchagua wawakilishi wake, majina ya yawasilishwe Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo nayo itayawasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ayatangaze rasmi kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba na wataanza kutekeleza majukumu yao baada ya kula kiapo cha uaminifu na utii kwa Jamhuri ya Muungano mbele ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufaa.
Itakumbukwa kuwa utaratibu kama huu umetumiwa na nchi jirani za Uganda na Kenya wakati wanaandika katiba zao.
Huu ni utaratibu unaowezesha wananchi wenyewe kushiriki kuandika Katiba yao na si kuwakilishwa.
No comments:
Post a Comment