KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, jana walikutana ana kwa ana katika mazishi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Moses Kulola (85).
Wanasiasa hao maarufu walikuwa ni miongozi mwa viongozi mbalimbali waliongozwa na Rais Jakaya Kikwete katika mazishi hayo yaliyofanyika jana eneo la Bugando jijini Mwanza.
Viongozi hao ambao walisalimiana kwa kushikana mikono walikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wengi waliohudhuria mazishi hayo kwa kushangiliwa kwa nguvu.
Akitoa salamu zake za rambirambi, Rais Jakaya Kikwete, mbali na mambo mengine alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuendeleza amani, upendo na utulivu.
Aliwataka wananchi kumuenzi kwa vitendo Askofu Kulola katika kupigania haki, amani na utulivu nchini.
Rais Kikwete aliongeza kuwa mbali na kuwa na urafiki na kiongozi huyo wa kiroho, askofu huyo alikuwa mshirika mzuri wa kuhubiri na mambo ya amani nchini, na kwamba kila walipokutana alikuwa akimsisitiza suala la amani ya nchi.
“Ni majonzi makubwa sana kumpoteza kiongozi huyu wa kiroho. Askofu Kulola alikuwa rafiki yangu sana na siku zote tulipokutana naye alikuwa akinishauri sana mambo ya amani ya nchi.
“Kwa maana hiyo, nawaombeni sana Watanzania tumuenzi kwa vitendo kiongozi huyu na tuwe washirika wazuri wa kulinda amani na upendo wa nchi. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe,” alisema rais.
Naye Lowassa alitoa rambirambi ya sh milioni moja huku Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mwanza alitoa pole kwa wafiwa akisema Askofu Kulola alikuwa ni mpenda maendeleo na amani.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na maaskofu, wachungaji na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya Kikristo kutoka Tanzania, Burundi, Kenya, Msumbiji na Malawi huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, naye akiwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria.
Katika mazishi hayo, watu wengi walianguka na kuzirai, hivyo kulazimika kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupewa huduma ya kwanza.
Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, mwaka 1930 katika Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza. Alifariki dunia Agosti 29, mwaka huu kwa ugonjwa wa mapafu na moyo. Ameacha mjane, watoto saba, wajukuu 46 na vitukuu 16.
No comments:
Post a Comment