Thursday, July 11, 2013

Lema asomewa mashtaka

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), jana alisomewa maelezo ya awali kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili, anayodaiwa kutoa kauli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alikwenda kwenye Chuo cha Uhasibu Arusha kama anakwenda kwenye sherehe za kuaga mtoto wa kike ‘send off’.
Akisoma maelezo, Wakili wa Serikali, Elianenyi Njiro, mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Msofe, anayesikiliza shauri hilo, alidai wanatarajia kupeleka mashahidi tisa akiwamo Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), John Nanyaro na Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Arusha (OCD), Gillis Mroto.
Aliwataja mashahidi wengine kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi akiwamo Mkaguzi Bernard Nyambanya na mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Jane, PC Godfrey, Joachim Mahanyu na wengine kutoka Chuo cha Uhasibu, ambao ni Faraji Mnepe, Benjamin Simkanga na Naibu Hamidu.
Awali akisoma maelezo hayo, Wakili Njiro aliieleza mahakama hiyo kuwa Aprili 24, mwaka huu, Lema akiwa eneo la Freedom Square ndani ya Chuo cha Uhasibu, alitoa maneno ya uchochezi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
Alisema kuwa maneno hayo yanayodaiwa kutamkwa ni kinyume cha kifungu cha 390 sura ya 35 cha sheria ya kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2002.
“RC anakuja (Chuo cha Uhasibu), kama anakwenda kwenye sendoff, hajui chuo kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hicho … (RC), ameshindwa hata kuwapa (wanafunzi) pole kwa kufiwa na amesema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu,” alinukuu baadhi ya maneno aliyodai kuwa yalitamkwa na Lema siku ya tukio.
Wakili Njiro alidai mahakamani hapo kuwa kauli hizo zilipandisha hasira za wanafunzi ambao walianza kumrushia mawe na chupa Mkuu wa Mkoa, Mulongo, alipokuwa akiwahutubia kuhusiana na tukio la kifo cha mwanafunzi, Henry Koga, kilichotokea Aprili 23, mwaka huu.
Lema kupitia kwa wakili wake, Method Kimomogoro, alikanusha madai hayo huku akikubali maelezo kuhusu jina lake, anwani, makazi na wadhifa wake, ambapo shauri hilo limepangwa kuanza kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 20-22, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment