Thursday, July 11, 2013

Slaa aparura Polisi


ALITAKA LIZUIE GREEN GUARD ZA CCM
SIKU moja baada ya Chama cha Demokarasia na Maendeleo (CHADEMA), kutangaza mipango ya kuwaandaa vijana wa chama hicho kwa kuwapa mafunzo maalumu ya ukakamavu, Jeshi la Polisi nchini limesema hatua hiyo ni kinyume cha sheria na litachukua hatua dhidi ya kauli ya viongozi wa chama hicho.
Wakati polisi wakijiandaa kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa CHADEMA, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, amelitaka jeshi hilo lianze kumkamata Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, aliyekipitisha na kukisajili.
Slaa alisema Katiba ya CHADEMA, iliyopitishwa na Tendwa inaelezea ukakamavu, hivyo anawashangaa polisi kwa kushindwa kutofautisha kati ya mafunzo ya ukakamavu na ya kijeshi yanayotolewa na vyombo vya dola.
Taarifa ya polisi
Taarifa ya polisi kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na msemaji wa jeshi hilo, SSP Advera Senso, ilisema kuwa kitendo cha chama chochote cha siasa, ikiwamo CHADEMA kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume cha sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Senso alisema kutokana na kauli iliyotolewa juzi na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Jeshi la Polisi linafanyia uchunguzi taarifa hiyo na likijiridhisha litachukua hatua kulingana na ushahidi utakaopatikana pasipo kujali wadhifa wa mtu.
Senso alipoulizwa na Tanzania Daima sababu ya kuchukua hatua hiyo sasa wakati vikundi hivyo vipo siku nyingi vikihusisha vyama vyote vya siasa, alisema hilo ndilo tamko la Jeshi la Polisi kwa sasa.
Slaa anena
Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alisema kauli ya Jeshi la Polisi inadhihirisha namna wahusika wasivyofahamu sheria kwa kile alichoeleza kuwa wao hawaundi majeshi bali vikundi vya ukakamavu.
Alisema ni heri msemaji wa jeshi hilo angekaa kimya kuliko kulifedhehesha Jeshi la Polisi kwa tamko lisilokuwa na ushawishi wa kisheria.
“Nawashauri hawa waanze na Tendwa…ila kwanini wameanza leo sisi tulishayalalamikia makundi ya CCM kwa barua na hata walipomaliza mafunzo yao kule Igunga tukapiga na picha wao hawakuinua mdomo kuliongelea,” alisema Dk. Slaa.
Alisema katika miaka minne iliyopita CHADEMA ilikuwa ikionyesha kwa ushahidi namna vijana wa CCM wanavyopewa mafunzo ya kijeshi, ikwamo silaha kutoka nje ya nchi huku wahusika wakiendelea kukaa kimya.
Aliongeza kuwa hali hiyo ya kuamka baada ya kauli ya CHADEMA inatia nguvu shaka yao, aliyodai kuwa makundi ya CCM yanafanya mafunzo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Dk. Slaa alitolea mfano kundi la vijana wa CCM walioweka kambi katika shule ya wazazi katika Kata ya Ivumwe, Mbeya mjini na kisha kuwateka katibu wa CHADEMA Mbeya mjini na baadhi ya wanachama wake.
Alisema katika tukio la Ivumwe wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani wa hivi karibuni, CHADEMA walitoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi wa Mbeya ambaye aliwajibu kuwa wapeleke ushahidi kama vijana hao ni wahalifu.
Alibainisha kuwa CCM imekuwa na kawaida ya kukusanya vijana kutoka maeneo tofauti na kisha kuwapa mafunzo ya kijeshi na silaha kwa ajili ya kuwadhuru wapinzani na kutolea mfano Kambi ya Ulemo aliyosema ilikuwa na vijana waliopewa mafunzo ya kijeshi.
“Tunawasubiri tuone hatima yao ni nini, sisi tunajua Jeshi la Polisi limeshajitoa kulinda viongozi wa CHADEMA sasa kwanini tusijilinde wenyewe,” alisema Dk. Slaa.
Juzi Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kikao cha dharura cha Kamati Kuu, kilichoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kimeridhia kuanzishwa kambi za mafunzo ya ukakamavu kwa vijana watakaowalinda viongozi.
Mbowe alisema Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua stahiki kuwalinda viongozi wa vyama vya siasa hususan wapinzani, hivyo Kamati Kuu ya CHADEMA imeamua kutoa mafunzo ya kujilinda.
Alibainisha kuwa sababu ya kuanzishwa kwa makambi ya ukakamavu ni kwa ajili ya kuwalinda viongozi wa CHADEMA, kwakuwa polisi wameshindwa kufanya kazi hiyo au wanafuata maelekezo ya viongozi wa CCM.
Alisema vikundi vya ulinzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na polisi wamekuwa wakiendesha zoezi la kuwadhuru wafuasi wa CHADEMA kwa kuwakata mapanga, kuwachoma visu au kuwapiga marungu pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.

No comments:

Post a Comment