Wednesday, July 10, 2013

Dk. Salim atoa kauli nzito

MMOJA wa wanasiasa wanaoheshimika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, Dk. Salim Ahmed Salim, ametoa kauli yenye mwelekeo wa kumpinga Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akionya matumizi ya nguvu za dola dhidi ya wananchi kwamba ni mwanzo wa anguko la amani nchini. 

Dk. Salim ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu, Katibu wa Umoja wa nchi za Afrika (OAU), mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) na wakati fulani akikaribia kuupata Ukatibu Mkuu wa UN, aliitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kongamano la kutafakari amani nchini, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD). 

Dk. Salim ambaye ni Mwanadiplomasia aliyebobea, kauli yake hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tu tangu Waziri Mkuu, Pinda aviagize vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kauli hiyo ya Pinda, ilitafsiriwa kuwa ni yenye mwelekeo wa kuvichochea vyombo vya dola kujichukulia sheria mkononi. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Salim ambaye ni Mwanadiplomasia aliyebobea alieleza kusikitishwa na viashiria vya uvunjifu wa amani vilivyoanza kujitokeza nchini hususani kupitia kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa pamoja na viongozi wengine mbele ya jamii. 

Katika hilo Dk. Salim 

aliitaka jamii kutokubali viashiria vya kuwavuruga na kusisitiza kuwa njia pekee ya kukabiliana navyo ni kuvumiliana ikiwa ni pamoja na kila mmoja kuheshimu misingi ya amani ambayo ni upendo na kuheshimiana. 

Dk. Salim alivikumbusha vyombo vya dola kwamba siku zote vinapotaka kutumia nguvu basi vifanye hivyo kwa maslahi ya wananchi, kinyume na hapo ni kuvuruga amani.

“Lazima tufike mahali tujifunze toka kwa wenzetu, kwamba bila amani nchi haitafanya chochote. Amani ni jambo muhimu, tusibaguane …hili ni muhimu katika maendeleo yetu na jamii kwa ujumla,” alisisitiza Dk. Salim ambaye pia alipata kuwa Waziri wa Ulinzi.

Dk. Salim pia alionya siasa kufanywa ndani ya madhabahu za kidini, hivyo kuwataka viongozi wa dini pamoja na wanasiasa watimize wajibu wao bila kuingiliana.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Pinda aliviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Pinda alitoa kauli hiyo baada ya Chadema kuingia kwenye mgogoro na Jeshi la Polisi siku chache baada ya tukio la bomu lililorushwa kwenye mkutano wake wa kampeni za udiwani katika viwanja vya Soweto jijini Arusha. 

Akizungumza katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma, Pinda alisema watu wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola.

Pinda alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia, kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo. 

Katika hilo alisema, Serikali imedhamiria kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali ifanye kazi hiyo. 

“Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema.

Wakati huo huo jana Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, amesema ameshangazwa na kitendo cha Chadema, kukataa kuhudhuria kongamano hilo la amani.

Kongamano hilo la siku mbili ambalo limeanza jana na kumalizika leo, lilikuwa na lengo la kutafakari amani ya nchi na demokrasia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mbatia alisema hajui sababu za Chadema kugoma kuhudhuria kongamano hilo, kwani wakati wakiwa Dodoma walikubaliana kuitisha makongamano ya aina hiyo yakiwashirikisha wadau mbalimbali kwa awamu.

“Mimi mwenyewe sijajua sababu hasa ya Chadema kutowasili siku hii ya leo, kwani lengo la TCD kuwaita hapa ni jema tu la kujadili mustakabali wa taifa na masuala ya itikadi yakae kando katika hili,” alisema Mbatia.

Juzi Chadema walitangaza kususia mkutano huo kwa kuwa aliyepanga, aliyefadhili na aliyeitisha mkutano huo kwa mgongo wa TCD ni Waziri Mkuu, Pinda ambaye walidai kuwa ndani yake haonekani kuwa na dhamira ya dhati ya kudumisha amani katika nchi yetu.

Mbatia alikiri mkutano huo kufadhiliwa kwa kiasi fulani na Serikali, huku fedha nyingine zikitoka kwa wafadhili wa TCD jambo ambalo alisema kuwa si baya.

Jana akizungumza kwenye kongamano hilo, Mbatia aliwataka viongozi waliopo madarakani kulinda amani iliyopo nchini ili yasije kutokea machafuko ya kisiasa kama yanayotokea katika nchi za Misri na Syria.

“Mfano baadhi ya mataifa kama Misri ambayo jeshi lake limegawanyika hadi sasa, Zimbabwe, Kenya na hapa kwetu kumekuwa na mauaji, hii yote ni kwa kuwa amani haijadiliwi mapema,” alisema Mbatia.

Mbatia pia aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini nchini wafanye kazi yao ya kuhubiri amani, upendo na mshikamano wa nchi bila kusimamiwa na askari polisi kwani haitaleta picha nzuri kwa taifa.

Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Tanzania bara, Julius Mtatiro alisema nchi inatakiwa iwe na mifumo mizuri ya uongozi kwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka katika kila sekta.

“Tumeshuhudia jinsi wananchi wa Mtwara walivyoteswa na wanajeshi kwa kukusanywa na kuambiwa wakumbatie miti kama wake au waume zao, hali hii siyo ya kawaida tunahitaji iangaliwe kwa upana wake.

“Serikali inatakiwa itende haki kwa wananchi wake bila kuangalia dini au wadhifa wa mtu, kwani hata tukifanya makongamano mara elfu kumi kama misingi ya amani isipolindwa ni kazi bure,” alisema Mtatiro.

No comments:

Post a Comment