Monday, March 4, 2013

Wabunge 47 kuhenyeshwa JKT


Yumo Halima Mdee, Godbless Lema
Pia Nassari, Silinde na Ester Bulaya
Wabunge 47 wa Bunge la Jamhuri leo wanaanza mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kwenye kambi mbalimbali za jeshi nchini wakiungana na wanafunzi 5,000 waliohitimu kidato cha sita Februari, mwaka huu.

Miongoni mwa wabunge watakaoshiriki mafunzo hayo ni vijana, wengi wakiwa wametikisa Bunge kwa hoja mbalimbali za moto na wamekuwa mstari wa mbele kuamsha uwajibikaji mpya ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Orodha ya wabunge hao ni pamoja na Godbless Lema wa Arusha Mjini (Chadema) na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki (Chadema), ambao wamekuwa mwiba mkali katika siasa za jukwaani hasa mkoani Arusha kutokana na kuendesha harakati zinazoibua hisia za vijana wengi.

Wabunge hawa kutoka Arusha  wameingia Bungeni kwa mara ya kwanza katika Bunge hili, Lema akishinda uchaguzi mwaka 2010, lakini ushindi wake umewatumbukia nyongo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumpinga mara mbili mahakamani, ingawa alishinda rufaa yake baada ya Mahakama Kuu kanda ya Arusha kumvua ubunge, makada wa CCM wamewasilisha maombi mahakama ya rufaa kuomba kupitiwa kwa hukumu yake upya.

Katika orodha hiyo, kuna mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, ambaye amepangiwa Ruvu. Silinde alisema “nipo njiani natoka jimboni naelekea kambini Ruvu nilikopangiwa, naenda mzigoni mwanangu.”

Yupo Zitto Kabwe ambaye atakuwa kambi ya Mgambo Tanga. Zitto pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya naye alisema kwamba aliondoka jana Dar es Salaam kuelekea Ruvu kwenye mafunzo hayo.

Halima Mdee wa Kawe (Chadema), alisema “mimi nilipangiwa Songea, lakini nimeomba nihamishiwe Ruvu au Tanga maana mama yangu anaumwa sana. Nimeona siwezi kukaa kwenye mafunzo mbali sana na mama kwa hiyo JKT wameniambia wanashughulikia watanijibu kesho (leo).”

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, alisema alipangiwa kambini Tabora lakini ameahirisha kushiriki mafunzo hayo kwa sababu ana dharura ya kifamilia.
“Nasikitika kwamba siwezi kushiriki kwa sababu nina dharura ya kifamilia … nilikuwa nimepangiwa Tabora lakini siwezi kwenda,” alisema.

Wabunge wengine ni wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine; Mtera (CCM) Livingstone Lusinde; Mchinga (CCM), Saidi Mtanda; Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu; Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba; na wa Viti Maalumu (CCM), Ritta Kabati.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi Nchini (JWTZ) Kanali Kapambala Mgawe, alisema leo yataanza mafunzo ya vijana waliomaliza kidato cha sita pamoja na baadhi ya wabunge.
Alisema mafunzo hayo ya JKT kwa wabunge yatakuwa kwa wiki tatu na wanafunzi yatakuwa kwa miezi sita.

Kanali Mgawe alisema kambi zitakazotumika katika kutoka mafunzo hayo ni pamoja na Ruvu (Pwani), Mgambo (Tanga), Oljoro (Arusha), Mafinga (Iringa), Mlale (Songea), Bulombora (Kigoma), Kanembwa (Kigoma) na Msange (Tabora).

Alisema kila mwaka zaidi ya wanafunzi 40,000 wa kidato cha sita wanahitimu masomo yao hivyo wameamua kuchagua wanafunzi 5,000 tu kwenda katika mafunzo hayo kutokana na ufinyu wa bajeti pamoja na kambi za mafunzo. Kadhalika, Mgawe aliongeza kuwa kutakuwapo na vijana wengine 5,000 wa kujitolea watakaojiunga na wanafunzi hao katika kupata mafunzo na kufanya idadi kufikia 10,000.

“Mbali na wanafunzi wa kidato cha sita na wabunge pia kutakuwapo na watu wa kutoka kada mbalimbali 5,000 wa kujitolea watakaopata mafunzo hayo,” alisema Mgawe.

Alisema kwa mwaka huu wameamua kuchagua shule za serikali tu pasipo kuchagua shule binafsi na kusema kuwa vigezo vilivyotumika katika kuchagua ni vya kawaida. Alisema kwa upande wa wabunge uchaguaji ulifanyika bungeni, hivyo vigezo vilivyotumika vilitoka bungeni na siyo JKT.

Alisema ni wanafunzi kutoka shule 25 za serikali nchi nzima zilizochaguliwa katika mafunzo hayo na zilichaguliwa pasipo kufuata utaratibu.

Kanali Mgawe alisema kwa wanafunzi watakaotoka katika vitongoji vyao watalazimika kutumia nauli zao wenyewe kufika makao makuu ya mkoa na baada ya hapo gharama za serikali zitatumika kuwasafirisha hadi katika kambi husika. Alisema, gharama za chakula na mengineyo yatakuwa kwa serikali na mzazi hatapaswa kuchangia chochote.

Mwaka jana, Waziri wa Ulinzi na JKT, Shamsi Vuai Nahodha, akiwasilisha hotuba ya makadirio ya Wizara yake bungeni alisema wabunge vijana  watakuwa sehemu ya kundi la kwanza la vijana 5,000 katika mafunzo yatakayoanza Machi mwaka huu.

Alisema gharama za kuendesha mafunzo hayo ni kubwa hivyo serikali haitakuwa na uwezo wa kuchukua vijana wote wanaostahili kupitia JKT kwa mujibu wa sheria na kwamba serikali inapanga kuchukua vijana 5,000 kwa kuanzia. Alisema vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu masomo ya kidato cha sita mwaka 2013 hivyo alisema kupata vijana 5,000 tu kati ya wahitimu wengi kiasi hicho ni kazi kubwa.

Kadhalika, Rais Jakaya Kikwete akiwa katika ziara yake Makao Makuu ya JKT Mlalakuwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, alisema serikali itatoa Sh. bilioni 18 kwa JKT kama sehemu ya mpango mkakati wa kufufua kambi za mafunzo na kuondoa changamoto zinazolikabili jeshi hilo. JKT ilianza mwaka 1963 wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo hayati Rashid Kawawa, walishiriki mafunzo hayo. Hata hivyo, mwaka 1966, mafunzo hayo yalipata changamoto kubwa kutoka kwa baadhi ya wasomi baada ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipogomea mpango huo, jaribio ambalo liligonga mwamba.

Wakati yanaanza, vijana wa kujitolea (volunteers) na wale wa lazima wenye elimu ya kidato cha nne na kuendelea, walifanya mafunzo ya miezi sita lakini baadaye yalirefushwa na kuendeshwa kwa mwaka mmoja.

Hata hivyo, mwanzoni mwa miaka ya 1990, mafunzo hayo ya JKT, yalisitishwa kutokana na sababu mbalimbali na sasa yamerejeshwa tena.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment