Monday, March 4, 2013

Chadema yambeba Odinga

WAKATI wananchi wa Kenya leo wanatarajia kupiga kura kumchagua rais wa nchi hiyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeonekana kumbeba mgombea urais kupitia Chama cha ODM ambacho kimo ndani ya Muungano wa CORD, Raila Odinga, kwa kupeleka magari na timu ya wasanii kumsaidia wakati wote wa kampeni zake.

Chadema ambao wanadaiwa kuwa rafiki mkubwa wa Odinga, kilituma magari mawili aina ya Fuso kwa ajili ya kumpigia kampeni ambazo zimedumu kwa mwezi mmoja.

Mbali ya kutuma magari hayo, Chadema walituma kikundi cha wasanii kikiongozwa na mwimbaji maarufu wa chama hicho, Fulgance Mapunda 'Mwanakotide’.

Mbali ya chama hicho, Watanzania wengi ambao wanadaiwa kumuunga mkono Odinga na wamekuwa wakitajwa mara kwa mara ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Rostam Aziz. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Chadema, Boniphace Makene alikiri chama chake kupeleka magari hayo na wasanii kwa ajili ya kumsaidia Odinga na timu yake kuendesha kampeni zake kwa ufanisi.

“Ni kweli kwa kipindi cha miezi mitatu sasa, timu ya Chadema imekuwa ikizunguka katika miji mbalimbali nchini Kenya, kwa ajili ya kumsaidia mgombea wa Muungano wa CORD kupiga kampeni, kumekuwa na mafanikio makubwa mno.

“Tuliruhusu magari yetu mawili aina ya fuso, ambayo yalikuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya muziki na wasanii wawili, Mwanakotide na Pepe ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa, tunaamini mchango umeonekana,” alisema Makene.

Alisema magari hayo, yalitumiwa na Odinga katika mikutano yote ya kampeni, ambazo zilihitimishwa juzi katika Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi. 

“Kama ulifanikiwa kuangalia televisheni, juzi kwenye Uwanja wa Nyayo, magari yale yalikuwa kivutio kikubwa sana, yalikuwa yamepambwa picha nyingi za Odinga na Kalonzo Musyoka, ambaye ni mgombea mwenza wake,” alisema Makene.

Kwa upande wake, Mwanakotide alipoulizwa alisema wamekuwa Kenya kwa kipindi cha miezi mitatu kusaidia ODM, kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na chama chao.

“Tumekuwa na mafanikio makubwa, kazi yetu ilikuwa kuhubiri amani na kuwataka Wakenya kuachana na mambo ya ukabila na chuki, tunaamini wametuelewa…unajua wale ni jamaa zetu, lazima tuwasaidie,” alisema Mwanakotide.

UCHAGUZI LEO

Homa ya uchaguzi imepanda kwa kila mwananchi wa Kenya, huku macho na masikio yakielekezwa zaidi kwa wagombea wawili wa urais, Raila Odinga wa Muungano wa CORD na Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee.

Katika uchaguzi huo, kuna wagombea wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Musalia Mudavadi (Amani), Martha Karua (NARC Kenya), Peter Keneth (KNC), Profesa Ole Kiapi, Paul Muite, Mohamed Abdalaah Dida.

Hata hivyo, Odinga na Kenyatta ndio wanaopewa nafasi kubwa kwa mmojawapo kuibuka na ushindi na hivyo kutegua kitendawili cha kampeni za aina yake, zilizodumu kwa mwezi mmoja.

Katika viunga vya Jiji la Nairobi ambapo MTANZANIA limepiga kambi, kuna kila aina ya shamrashamra na majigambo ya hapa na pale kutoka kwa wapenzi wa wagombea hao wawili kila mmoja akitamba kuibuka na ushindi.

Jiji hilo, ambalo mara nyingi huwa ni safi, safari hii limechafuka kutokana na mabango ya wagombea ambayo yametanda kila kona.

Ufungaji kampeni 

Raila Odinga na mgombea mwenza wake, Kalonzyo Musyoka walikuwa Uwanja wa Nyayo, wakati wenzao wa Muungano wa Jubilee, Uhuru Kenyatta na William Rutto, walikuwa kwenye viwanja vya Uhuru Park, umbali wa kilometa 20 hivi. Katika mikutano yote miwili kulikuwa na umati mkubwa wa watu.

Hata hivyo, katika mkutano wa Kenyatta, kulikuwa na fujo za hapa na pale, zilizosababishwa na vijana walioonekana wamelewa pombe na kutishia kutaka kukaba watu, ambapo ililazimika polisi watumie nguvu za ziada kukabiliana nao.

Ujumbe wa wagombea wote, ulikuwa ni amani kutumia vyombo vya mahakama kama wakidhulumiwa.

Kwa upande wake, Odinga alisema yuko tayari kupokea matokeo yoyote halali, lakini kama akidhulumiwa atatumia mahakama kudai haki yake.

Aliwasihi mashabiki wake, kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Kenyatta, aliutumia muda mwingi kujibu tuhuma ambazo amerushiwa na wapinzani wake kuwa amejimilikisha ardhi kubwa kupita kiasi.

Alisema yuko tayari kuunda Serikali na kuwataka Wakenya wajitokeze kwa wingi, ili waweze kuwachagua.

Kalonzyo Musyoka, alitumia maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema kuwa ‘itaichukua miaka 1,000 dunia kumpata mtu kama Mahattma Gandhi (India) na itawachukua miaka 100 Wakenya kumpata kiongozi aina ya Odinga.

Mgombea mwingine ambaye ana umuhimu wake katika uchaguzi huo, ni Musalia Mudavadi wa Chama cha UDF, ambao ni (Muungano wa Amani), yeye ndiye mwenye kura ya turufu kama uchaguzi utarudiwa.

Kampeni zake kubwa amezifanyia huko Magharibi mwa Kenya karibu na Uganda, ambako aliwasihi Wakenya wamchague yeye kuwa rais wao, hata hivyo aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa Odinga wakati wa ODM.

Katika uchaguzi huu, awali alisaini mkataba wa ushirikiano na Kenyatta, kwamba yeye ndiye angekuwa mgombea urais kupitia Jubilee, lakini siku chache baadaye Uhuru alimgeuka na kusema kulikuwa na ushawishi wa kishetani.

Mudavadi kuona hivyo, aliamua kusimama mwenyewe. Hata hivyo, kiongozi huyo anaelezwa kuwa anaungwa na Rais Mstaafu wa nchi hiyo, Daniel arap Moi.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2002, Moi alimsimika Uhuru kuwa mgombea Urais kupitia KANU, wakati huo Mudavadi alikuwa Makamu wa Rais wa Moi ambaye alishindwa vibaya na Mwai Kibaki ambaye wakati huo alikuwa bega kwa bega na Odinga.

Swali la kujiuliza hapa ni je ikitokea kura zikarudiwa, Mudavadi atamuunga mkono nani kati ya Kenyatta na Odinga?

Habari zilizopatikana jijini Nairobi, zinasema Mzee Moi ameamua kumtosa Uhuru kwa sababu yeye amekitosa chama chake cha KANU, ambacho hakina nguvu kabisa katika uchaguzi huo. KANU imejiunga na Muungano wa Amani.

SUALA LA UKABILA

Kama ilivyo ada kwa Wakenya, suala la ukabila lipo juu kwenye kampeni za mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2007, wakati huo mchuano ulipokuwa kati ya Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga, ukabila huo pia ulisababisha kutokea machafuko.

Gharama za uchaguzi

Gharama zote za kampeni kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa Sh bilioni 24, lakini inakadiriwa mgombea wa Jubilee (Kenyatta), ametumia Sh bilioni 30 hadi 50 (sawa na zaidi ya trilioni 6 za Tanzania).

Katika kampeni hizo, Kenyatta alitumia jumla ya helkopta 10 na Odinga anakadiriwa kutumia Sh bilioni 10 mpaka 20 za Kenya.

MAANDALIZI 

Maandalizi ya aina yake yamefanyika ambapo, sehemu ya kujumlishia matokeo ya kura za kitaifa, (National tallying Centre), imeandaliwa vizuri, kuna sehemu maalum kwa ajili ya vyombo vyote vya habari. Vifaa vya kisasa vimesheheni katika eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa matokea kwa uwazi na urais zaidi.

Vyombo vya usalama viko tayari, kila mahali kuna ulinzi wa kutosha ikiwa ni pamoja na sehemu zote zenye mjumuiko wa watu wengi.

Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mtunga, alisema mahakama itakuwa tayari wakati wowote itakapohitajika hata kama kesi itatokea usiku.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya, Isaack Hassan alisema, tume yake ipo tayari kuendesha uchaguzi huo hata kama kutatokea uchaguzi wa marudio kwa wagombea kutokufikisha asilimia 51 inayotajwa na Katiba. Watu waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 14.3, kuna majimbo 290, kata 1,450 na vituo vya kupigia kura 33,000 na Kaunti 47.

No comments:

Post a Comment